Salumu Abdallah Yazidu (pichani)hatosahaulika kamwe katika ulimwengu wa muziki. Alikuwa mtunzi, mwimbaji wa bendi ya Cuban Marimba iliyokuwa na maskani yake katika mji wa Morogoro. 

Wakati wa uhai wake alileta ushindani mkubwa katika muziki wa dansi mjini humo akishindana na bendi ya Morogoro Jazz iliyokuwa ikiongozwa na Mbaraka Mwinshehe Mwaruka.

Kwa bahati mbaya wanamuziki hao wamekwishatangulia mbele ya haki ambapo vifo vyao vilitokana na ajali za magari. Mbaraka Mwishehe alifariki katika ajali ya gari nchini Kenya Januari 12, 1979.

Mwaka huu Novemba 19, 2015 Salumu Abdallah ametimia miaka hamsini tokea kifo chake. Sababu zilizoleta kifo chake zilielezwa kuwa alikuwa akiendesha gari usiku, akielekea ukumbini kupiga muziki. Akiwa katika mwendo ghafla taa za gari hilo zilizimika.

Gari hilo likatoka nje ya barabara na kumtupa nje akapasuka kibofu na kufariki siku hiyo.

Wasifu wa nguli huyo unaeleza kuwa alizaliwa Mei 5, 1928. Baba yake alikuwa Mwarabu na mama yake alikuwa wa kabila la Waluguru kutoka mkoani  Morogoro. 

Salumu Abdallah alisoma mpaka darasa la sita huko Msamvu mkoani humo. Baadaye alichaguliwa kuendelea na shule jijini  Dar es Salaam. Licha ya kufaulu huko, baba yake aliamua abakie nyumbani kumsaidia katika shughuli za biashara. Katika kipindi hicho Salum alianza kuonesha kupenda kwake muziki. 

Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa maarufu kwa kuitwa kwa namba zake. Gv1, GV2, GV3 na kadhalika. Pamoja na baba yake kutokupenda aina ya muziki aliokuwa anaupenda mwanaye, aliona ni heri amnunulie gramafoni ya kupigia hizo santuri ili atulie. 

Haukupita muda mrefu Salum Abdallah alitoroka nyumbani kwao ili aende nchini Cuba kujifunza muziki. Alienda katika mji wa Mombasa akiwa na madhumuni ya kupanda meli kwenda nchini Cuba mwaka 1945.

Kwa kuwa wakati huo kulikuwa bado na vuguvugu la Vita ya Pili ya Dunia na safari yake ikaishia Mombasa. Akiwa mjini Mombasa, alipatwa na matatizo ya kuibwa fedha zake. Kufuatia hali ngumu ya maisha iliyomkumba, akalazimika kuanza kuchoma mishikaki mjini humo.

Umoja wa Waarabu wa Mombasa wakamtaarifu baba yake ambaye hatimaye alimrudisha Morogoro. Baada ya kurudishwa, baba yake akamfungulia mgahawa ili atulie, lakini Salum Abdallah Yazidu, maarufu kama SAY tayari alikuwa keshapata mzuka wa muziki. Alikuwa ameanza kuhudhuria madansi na kupendezwa sana na vifaa vya muziki vya bendi ya Dar es Salaam Jazz.

Wakati huo yeye na wenzake walikuwa tayari wameanzisha kikundi ambacho kilikuwa na vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili, wakikiita jina la La Paloma. Jina hilo lilikuwa toka wimbo mmoja katika santuri za GV. Wimbo huo ni mzuri kiasi kwamba mpaka leo bado unapigwa duniani kote.

Bendi hiyo ya La Paloma  ilikuwa na viongozi akiwamo Rais wa bendi Juma Said, Abubakar Hussein alikuwa mweka hazina, Ramadhan Salum ambaye alikuwa Katibu Mkuu, Ali Waziri akawa Naibu Katibu Mkuu na Salum Abdallah mwenyewe akiwa ndiye kiongozi wa bendi.

Katika kuiona Dar es Salaam Jazz Band, hamu ya kuwa na vyombo kama vya Dar Jazz ilikuwa kubwa kiasi cha Salum kuuza kwa siri nyumba mojawapo ya baba yake na kununua vyombo kama vya Dar es Salaam Jazz band. 

Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi rasmi. Wanamuziki waliounda bendi hiyo walikuwa ni Salum Abdallah, Kibwana Seif, Juma Kilaza, Ligongo, Mgembe, Juma Kondo, Waziri Nzige, Daulinge. La Paloma mwaka 1952 ilibadili jina ikawa Cuban Marimba Jazz. 

Salum Abdalla alitunga nyimbo nyingi hususani za mapenzi ambazo ziliwavutia wapenzi na mashabiki kujaa popote alipokuwa akipiga muziki. Baadhi ya nyimbo hizo ni pamoja na Naumia, Cuban yaleta Chacha, Beberu, Nalia, Shemeji na Ngoma iko huku.

 Mungu ailaze roho yake pahala pema peponi, amina.

 

Mwandishi wa makala haya anapatikana kwa namba: 0784 331200, 0767 331200 na 0713 331200.

By Jamhuri