Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema safari ya Kiongozi Mkuu wa Madhehebu ya Kiislamu ya Bohora Duniani (Da’i al-Mutlaq), Syedna Mufaddal Saifuddin, kwa kutumia treni ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Morogoro ni ishara kubwa ya kuaminiwa kwa huduma za reli nchini pamoja na mafanikio ya miundombinu ya kisasa inayojengwa na Serikali ya Tanzania.

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha TRC kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, imeelezwa kuwa kiongozi huyo wa 53 wa kiroho wa dhehebu la Bohora, akiwa ameambatana na viongozi na waumini zaidi ya 70, alisafiri Mei 16, 2026 kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya kutembelea waumini wa dhehebu hilo.

TRC imeeleza kuwa hatua ya kiongozi huyo mwenye heshima kubwa duniani kuchagua kutumia usafiri wa SGR, ni uthibitisho wa kiwango cha usalama, ubora, utulivu na hadhi ya huduma zinazotolewa kupitia reli ya kisasa nchini Tanzania. Aidha, safari hiyo imeelezwa kuwa ni sehemu ya “diplomasia ya usafiri”, ambapo wageni wa kimataifa wanakuwa mabalozi wa kuitangaza Tanzania na huduma zake kupitia uzoefu wao binafsi.

“Kutumika kwa SGR na viongozi wa kimataifa kunaonyesha kuwa Tanzania imefikia kiwango cha miundombinu kinachoweza kuaminiwa na watu wa hadhi mbalimbali duniani,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

TRC pia imebainisha kuwa ujio wa viongozi na waumini wa Bohora mkoani Morogoro kupitia SGR unachochea shughuli za kiuchumi ikiwemo hoteli, usafiri wa ndani, biashara ndogondogo pamoja na huduma mbalimbali za kijamii, huku ukikuza utalii wa kidini na uchumi wa ndani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, SGR sasa imeendelea kuonekana si tu kama njia ya usafiri, bali chachu ya maendeleo inayounganisha jamii, dini, biashara na diplomasia ya Tanzania. Shirika hilo limeongeza kuwa matumizi ya reli na viongozi wakubwa wa dini yanaendelea kujenga imani kwa wananchi kuhusu ubora wa huduma zinazotolewa na TRC kupitia treni za kisasa za SGR.