Dkt.Kiruswa Ataka Ujenzi Kuharakishwa, Asisitiza Uongezaji Thamani Nchini

Tayari WanaKigamboni 278 Wameajiriwa, Zaidi ya Asilimia 90 ni Watanzania

Mwezi Julai Pekee Mkoa wa Kimadini Dar/Pwani Umekusanya Bil 4.06

📍 Kigamboni,Dar Es Salaam

Tanzania imeingia katika Hatua Mpya ya Uendelezaji wa Madini Tembo (Heavy Mineral Sands), huku shughuli za uchimbaji zikiendelea kupitia Mradi wa Fungoni- Kigamboni na Tajiri sambamba na ujenzi wa Kiwanda cha Uchakataji wa Madini hayo Mkoani Tanga.

Uchimbaji na uchakataji wa Madini Tembo unatekelezwa kupitia Kampuni ya Ubia ya Nyati Mineral Sands Limited, ambapo Serikali inamiliki hisa zisizofifishwa za asilimia 16.

Akizungumza leo, Agosti 18, 2026, alipotembelea na kukagua shughuli za uzalishaji wa madini hayo katika Mradi wa Fungoni- Kigamboni, pamoja na kupata taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa kiwanda cha uchakataji Tajiri- Tanga, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ameitaka kampuni hiyo kuharakisha ujenzi wa kiwanda hicho, akisisitiza dhamira ya Serikali ya kuongeza thamani ya madini nchini kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Dkt. Kiruswa amesema Serikali imetoa kibali cha muda wa miaka miwili kwa kampuni hiyo kusafirisha madini ghafi nje ya nchi, hatua inayolenga kuipa kampuni nafasi ya kukamilisha ujenzi wa kiwanda na kukuza zaidi mtaji wa mradi.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kampuni hiyo kuimarisha uhamishaji wa maarifa na ujuzi kwa Watanzania, kuongeza ushiriki wa Watanzania katika shughuli za mradi na kuendelea kuwajibika kwa jamii zinazozunguka maeneo ya mradi.

Vilevile, Dkt. Kiruswa, amesisitiza kampuni kutekeleza Mpango wa Ufungaji wa Mgodi (Mine Closure Plan) kwa kurejesha maeneo yaliyotumika katika hali salama na yenye tija, huku athari kwa mazingira zikidhibitiwa.

Akielezea maendeleo ya Sekta ya Madini Mkoa wa Kimadini wa Dar es Salaam na Pwani, Dkt. Kiruswa amesema umeendelea kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali ambapo katika mwaka wa Fedha 2025/26 ulikusanya Shilingi bilioni 27.07 dhidi ya lengo la Shilingi bilioni 24. Kwa mwaka wa fedha 2026/27, mkoa huo umepewa lengo la kukusanya Shilingi bilioni 33, huku tayari imekusanya Shilingi bilioni 4.06 kwa mwezi Julai pekee ambayo ni asilimia 147.50 ya lengo la mwezi ( bilioni 2.75).

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Nyati Mineral Sands Limited, Wei Huang, amesema kampuni mama, Shenghe Resources Holding Co. Ltd, imechagua Tanzania kuwa kitovu cha uchakataji wa Madini ya Tembo, ambapo madini yatakayozalishwa katika miradi yake nchi mbalimbali, ikiwemo Madagascar, yatachakatwa Tanzania.

Amesema tangu mwaka 2024, jumla ya tani 85,000 za Madini Tembo zimezalishwa kupitia mradi wa Kigamboni, ambapo tani 14,793.35 tayari zimesafirishwa.

Akizungumzia thamani ya uwekezaji, Wei amesema miradi ya Kigamboni na Tajiri ina uwekezaji wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 30, huku uwekezaji wa kampuni ya Shenghe nchini Tanzania ukifikia takribani Dola milioni 600, ukijumuisha mradi wa uchimbaji na uchakataji wa madini adimu (Rare Earth Elements) unaotekelezwa Mkoani Songwe.

Ameongeza kuwa zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi katika miradi hiyo ni Watanzania, huku wakazi wa Kigamboni pekee wanaonufaika na ajira wakifikia 284. Kwa Mradi wa Kigamboni, uhai wa mgodi unakadiriwa kuwa miaka minne, huku mradi wa Tajiri, Tanga ukiwa na muda wa miaka 23 ya uwekezaji.

“Shenghe ina uzoefu wa kufanya shughuli hizi katika nchi mbalimbali duniani na tayari tumewekeza Australia, Canada, Nigeria, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na nchi nyingine. Tumeichagua Tanzania kutokana na mazingira ya uwekezaji na historia ya ushirikiano kati ya nchi hizi,” amesema Wei.

Naye, Afisa Tarafa wa Kigamboni, Augusta Safari, aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, amesema mradi huo umeanza kuleta manufaa kwa Wilaya hiyo kupitia mapato, ajira na utekelezaji wa shughuli za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR). Amesema tayari fidia imelipwa kwa wakazi wote waliopisha mradi na Wilaya itaendelea kuhakikisha mazingira salama kwa uwekezaji.

Madini ya Tembo hutumika katika utengenezaji wa bidhaa mbalimbali, zikiwemo rangi za nyumba, vigae vya sakafu na ukutani pamoja na vipuri vya ndege, hivyo kuifanya Tanzania kuwa na fursa kubwa ya kuongeza thamani na kujenga mnyororo wa thamani wa madini hayo ndani ya nchi.