Mlipuko wa Ebola unaoenea kwa kasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umeua watu 2,325 na kuwa mbaya zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa watu 4,945 wameambukizwa. Katika saa 24 zilizopita pekee, visa vipya 101 na vifo 33 viliripotiwa.

Shirika la Afya Duniani, WHO, linasema mlipuko huo unasambaa kwa kasi isiyo ya kawaida na unaweza kuvuka vifo zaidi ya 11,000 vilivyorekodiwa Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016.

Juhudi za kuudhibiti zinakabiliwa na ukosefu wa chanjo na tiba iliyoidhinishwa dhidi ya aina ya Bundibugyo , pamoja na barabara mbovu, ukosefu wa usalama, migomo ya wahudumu wa afya na taarifa potofu. Umoja wa Mataifa umetenga dola milioni 30.5 zaidi kukabiliana na mlipuko huo.