Na Mwandishi Weu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kwa mara nyingine Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) imeweka wazi msimamo wake kuhusu uongozi wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), baada ya kumpokea Anthony Mtaka katika makao yake makuu Lausanne, Uswisi, kama Rais wa TOC.
Mtaka na ujumbe wake alitembelea Olympic House Septemba 29, mwaka huu, katika ziara rasmi ya TOC na kufanya mazungumzo na Rais wa IOC, Kirsty Coventry, pamoja na maofisa wa taasisi hiyo na Olympic Solidarity.
Ujumbe wa Tanzania ulihusisha Makamu wa Rais wa TOC, Nassra Juma Mohammed; Kaimu Katibu Mkuu, Khalid Rushaka; na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Wachezaji, Andrew Mlugu.
Mazungumzo yaligusa utambuzi na uendelezaji wa vipaji, ufadhili wa mafunzo kwa wanamichezo, makocha na waamuzi, kuimarisha taasisi pamoja na maandalizi ya Tanzania kuelekea Michezo ya Olimpiki ya Los Angeles 2028.
Ziara hiyo inakuja takribani miezi mitatu baada ya uchaguzi wa TOC wa Julai 5, mwaka huu, ulioacha sintofahamu kubwa baada ya matokeo yaliyotangazwa kutofautiana na kura ambazo wajumbe na mawakala walisema zilihesabiwa hadharani.
Kamisheni ya Uchaguzi ilimtangaza Leonard Thadeo kuwa mshindi kwa kura 19, ikisema Mtaka alipata kura 11 na Henry Tandau kura sita. Wajumbe walipinga matokeo hayo, wakisema hesabu waliyoishuhudia ilimpa Mtaka kura 29, Tandau kura sita huku Thadeo akiambulia kura moja tu.
KWA HABARI ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI OKTOBA 6-12, 2026


