Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Khatib Mwadin Khatib amesema Wizara hiyo imejipanga kupambana na vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kupitia Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia (PAMOJA) kwa kuwawezesha Wanawake Kichumi kupitia kikundi vya Ujasiria mali vya Wanawake.

Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya kufungua kikao cha baina ya Maafisa watendaji wa Mradi wa huo na Watendaji wa Benki ya Dunia, kikao kimefanyika katika Ukumbi wa Mradi wa PAMOJA, Kinazini, Unguja.

Amesema Mradi wa PAMOJA utasaidia kupunguza vitendo vya Ukatili na Udhalilishaji wa Kijinsia kwa kuwainua wanawake kiuchumi kupitia vikundi vya Ujasiria Mali kwani watapatiwa elimu pamoja na kupewa mkopo ya fedha.

Alifahamishwa kwamba huo ni utekelezaji wa sehemu ya kwanza ya Mradi lakini sehemu ya pili ya Mradi huo, katika kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji, Mradi utajenga Nyumba Salama mbili, Unguja na Pemba pia Mradi utajenga kituo cha Ushauri nasaha wa kisaikolojia kitajengwa Unguja.

Pia alisema sehemu ya tatu ya Mradi huo imejikita katika Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ambapo vituo vya malezi ya Kutwa vitajengwa vituo 16 katika wilaya nane zinazotekeleza Mradi ili wazazi waweze kuwapeleka Watoto kulelewa wakati wao wakiwa katika shughuli za Ujasiriamali.

“Mradi huu una sehemu nne za utekelezaji sehemu ya nne ni sehemu ya usimamizi wa Mradi, lakini sehemu ya Kwanza, ya pili na yatatu zitasaidia kutokomeza vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa Kijinsia, kwani umasikini unachangia udhalilishaji kwa mujibu wa wataalam wanavyosema lakini mzazi akiwezeshwa kiuchumi itasaidia kupungunza vitendo viovu” Alisema Khatib.

Naye Mratibu wa Mradi wa PAMOJA Aisha Abbas Seif amesema zaidi ya vikundi elfu nne vya Ujasiriamali vya Wanawake vimefanyiwa utambuzi (maping), vikundi hivyo vitapatiwa mafunzo hivyo kikundi ambacho kitafaulu katika mafunzo hayo kitapatiwa mkopo wa fedha, lakini wataanza kutoa mafunzo kwa vikundi mia mbili kwanza.

Amesema katika hatua nyingene ya utekelezaji wa Mradi sehemu ya pili wamefanya pia zoezi la utambuzi (maping) kuwatambua watoa huduma wa masuala ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji ili kujua mahitaji yao na changamoto zinawakabili.

Aidha Mratibu huyo alisema sehemu ya tatu ya utekelezaji wa Mradi huo inahusu Ujenzi wa Vituo vya Malezi ya Kutwa ya mtoto mungozo umeshatengenezwa na ripoti yake imeshawasilishwa kwa viongozi wa simamizi wa Mradi na Mfadhili wa Mradi ambae ni Benki ya Dunia (World Bank).

“Maping ni Utambuzi na Uainishaji wa wadau, rasimali na maeneo muhimu ya utekelezaji wa Mradi. Katika usimamizi wa Mradi, maping ni zoezi la kukusanya, kutambua, kuchambua na kuweka taarifa muhimu katika mpangilio unosaidia kupanga na kutekeleza shughuli za mradi kwa ufanisi” Alisema Aisha.

Kwa upande wa Benki ya Dunia akizungumza Msimamizi wa watendaji wa Mradi wa PAMOJA Ndugu Tanya D’Lima  amesema lengo la kikao hicho ni katika utaratibu wa Benki ya Dunia kufuatilia utendaji wa Miradi wanayoifadhili kwaajili ya kuona mafanikio na changamoto zilizowakabili watendaji ili waweze kutoa msaada wa kutatua changamoto hiyo.

Katika Nyakati tofauti akizungumza Mwenyekiti wa Kikundi cha El Bahsany Modest Fashion Cooperative Nassara Khatib Hamad amesema kikundi chao kipo Chake lakini hakijabahatika kuingia katika zoezi la utambuzi ila wanaamini kwamba zoezi hilo litakapofanyika kwa mara ya pili kikundi hicho kitatambuliwa na kupata mafunzo na mkopo wa fedha.

“Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania- PAMOJA unatekelezwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Kushirikiana na Wakala wa Uwezeshaji Wananchi kiuchumi (ZEEA) na unafadhiliwa na Benki ya Dunia, Mradi huo ulipangwa kutekelezwa kwa miaka mitano lakini Wizara hiyo imeamua kutekeleza kwa miaka mitatu”