Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Kwa mara ya kwanza, nchi yetu inajiandaa kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya soka barani Afrika, AFCON 2027.

Ni fursa kubwa kwa Tanzania. Ni nafasi ya kuitangaza nchi, kukuza shughuli za kiuchumi na kuacha urithi wa miundombinu utakaoendelea kutumika hata baada ya mashindano hayo.

Licha ya maandalizi yanayoendelea, kuna jambo ambalo halipaswi kupuuzwa, yaani maandalizi ya wananchi wenyewe. Kuna matukio mengi yanayoashiria kuwa Watanzania tumegawanyika. Tumefikia hatua ya baadhi yetu kuiona Taifa Stars kama ni mali ya Serikali, na si ya nchi! Hili lipo. Tusijidanganyane.

Kwa sasa, kuna dalili zinazoonyesha kuwa uhusiano kati ya Taifa Stars na mashabiki wake si ule uliokuwapo miaka ya nyuma. Ukisikiliza mazungumzo ya mashabiki, ukafuatilia mijadala katika mitandao ya kijamii na kuangalia mwitikio wa wananchi katika baadhi ya mechi za timu ya taifa, utaona kwamba hamasa ama imepungua, au haipo.

Taifa Stars, ambayo ilipaswa kuwa timu inayowaunganisha Watanzania, wakati mwingine imekuwa ikionekana kana kwamba ni timu ya watu au taasisi fulani. Inaonekana ni kama timu ya watawala. Hili ni jambo la kutafakari, hasa tunapokaribia AFCON 2027.

Soka si mchezo wa miguu pekee. Soka ina hisia, ina uzalendo na ina uwezo wa kuwaunganisha watu. Mchezaji anapokuwa uwanjani, anahitaji kuona nyuma yake kuna taifa linalomwamini na linasubiri awape furaha.

Ndiyo maana uhusiano kati ya timu ya taifa, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wizara inayosimamia michezo na wadau wengine wa michezo ni muhimu sana. Pale ambapo taasisi hizi hazionekani kuwa na mwelekeo mmoja, madhara yake yanaweza kufika hadi kwa mashabiki.

Tunapaswa kujiuliza kwa nini baadhi ya mechi za Taifa Stars hazina tena mwitikio uliokuwa ukionekana miaka ya nyuma? Kwa nini shabiki ambaye anaweza kujaza uwanja kuishangilia timu yake ya klabu, hana msukumo huo huo anapokuja kuishangilia timu ya taifa?

KWA HABARI ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 6-12, 2026