Watu wasiopungua watatu wamekufa na wengine 20 wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi ya Urusi yalioulenga mji mkuu wa Ukraine, Kyiv mapema leo.

Meya wa Kyiv, Vitali Klitschko, ameandika kwenye mtandao wa Telegram kwamba mashambulizi makubwa ya makombora yaliofanyika usiku wa kuamkia leo yalilenga maeneo ya makaazi na maghala, na kusababisha vifo pamoja na majeruhi na kuziacha baadhi ya sehemu za mji mkuu wa Ukraine bila umeme.

Klitschko alisema jengo la ghorofa tisa limeporomoka huku moto ukizuka katika maeneo kadhaa kufuatia mashambulizi hayo. Aidha, kulikuwa na taarifa za watu kunaswa ndani ya majengo.

Urusi na Ukraine zimeongeza mashambulizi katika miezi ya hivi karibuni, huku Moscow ikiongeza mashambulizi yake ya masafa marefu ikilenga miji na maeneo ya makaazi katika sehemu mbalimbali za Ukraine.

Jeshi la anga la Ukraine pia limeonya kuhusu uwepo wa mashambulizi ya makombora ya Urusi aina ya Kalibr karibu na kijiji cha Kagarlyk, katika Mkoa wa Kyiv, yakielekea katika mji mkuu.

Ingawa Kyiv imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi karibu kila usiku, Ukraine nayo imeongeza mashambulizi yake ya kulipiza kisasi dhidi ya Urusi katika miezi ya hivi karibuni. Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuishinikiza Moscow kurejea kwenye meza ya mazungumzo ya amani, baada ya karibu miaka minne na nusu ya vita.