Na Kulwa Karedia, JamhuriMedia, Zanzibar

Bastola, kitambaa cheusi usoni na mateso ya zaidi ya saa saba. Huo ndio mkasa anaosimulia Mwinyi Salmin Amour (50), mtoto wa sita wa Rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour, anayedai kutekwa na watu watatu mjini Unguja.

Tukio hilo limeibua sura mpya ya matukio yanayodaiwa kuwa ya utekaji ambayo kwa miaka kadhaa yameripotiwa zaidi Tanzania Bara, safari hii yakivuka upande wa pili wa Muungano na kuingia Zanzibar, ambako tofauti na Bara, mwathirika ni mtoto wa mtu aliyewahi kushika wadhifa wa juu zaidi serikalini.

Mwinyi ameliambia JAMHURI kuwa watu waliomchukua, waliodai kuwa maofisa wa vyombo vya dola, walimpeleka katika nyumba iliyopo Chukwani na kumtaka awape Dola za Marekani 300,000.

Anadai alipowaeleza kuwa hana fedha hizo, mateso yakaanza.

“Wakanifunga miguu, mmoja wao akaninyanyua, wakanigeuza kichwa chini miguu juu, wamefunga kamba kwenye nondo ya dirisha. Yalikuwa mateso mabaya sana kuwahi kuyapata maishani mwangu,” amesema.

Jeshi la Polisi Zanzibar limethibitisha tukio la Mwinyi kuchukuliwa Septemba 23, 2026, katika mgahawa wa Safari Café karibu na Uwanja wa Ndege wa Zanzibar na kupelekwa Chukwani.

Polisi wamesema uchunguzi unaendelea, huku gari aina ya Toyota RAV4 nyeupe yenye namba za usajili zilizohifadhiwa, inayodaiwa kutumika katika tukio hilo, ikishikiliwa.

Akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Mombasa, Unguja, mwishoni mwa wiki, Mwinyi amesema anaamini tukio hilo linahusiana na shughuli zake za biashara na ametekwa na mmoja wa mashemeji zake, aitwaye (jina linahifadhiwa).

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI INAENDELEA KWENYE GAZETI LA JAMHURI OKTOBA 6-12, 2026