Na Manyerere Jackton, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Kifo cha bilionea Wicknell Chivayo kimeibua mambo mengi, kila mmoja akimjadili kwa namna anavyoweza.
Wengine wamejikita katika maisha aliyoishi, utajiri aliokuwa nao na namna alivyoutumia, huku wengine wakikitumia kifo chake kama somo la maisha, wakisisitiza kwamba mwisho wa mwanadamu ni kifo, bila kujali amekusanya mali kiasi gani.
Nimeona kauli zinazoweza kuwa na mchango mkubwa katika kudumaza fikra za maendeleo ikiwa zitatumika kama falsafa ya jamii.
Baadhi wameandika, “Usihangaike sana kujenga, kutafuta mali au kubadilisha maisha, kwa sababu mwisho wa yote utakufa na utaviacha…”
Kweli, kifo ni sehemu ya maisha. Mali, nyumba, cheo na umaarufu haviwezi kuzuia mwanadamu kufa. Hilo halina ubishi wala mjadala. Kwa hiyo, kumkumbusha mtu kwamba kifo kipo, na kwamba utu, upendo na wema ni muhimu kuliko kujilimbikizia mali pekee, si jambo baya.
Ni vema pia kukumbushana kwamba tamaa isiyodhibitiwa inaweza kuisukuma jamii katika rushwa, uporaji, unyonyaji na maovu mengine mengi. Hivyo, kauli ya “Tafuta pesa, lakini usipoteze utu” ndiyo inayofaa hapa.
Katika kujadili suala hili, nianze na swali moja: Kwa nini baadhi ya jamii zimefanikiwa kujenga viwanda, taasisi, shule, hospitali, teknolojia na kuwa na mitaji mikubwa?
Bila shaka, ni kwa sababu watu hao wamekubali kutumia sehemu kubwa ya maisha yao kujenga vitu ambavyo wao wenyewe huenda wasivione vikikamilika au vikitumika; bali wanafanya hivyo kwa ustawi wa wajao mbele yao.
Mjasiriamali anajenga kiwanda ambacho kinaweza kubaki baada ya kifo chake. Mtafiti anafanya utafiti ambao kizazi chake kitautumia. Waliogundua ndege wasingehangaika kufanya hivyo kama wangekuwa na akili ndogo ya kwamba si wao watakaofaidi. Mwalimu anawafundisha watoto ambao watakuwa viongozi baada yake, na huenda wakawa wanasayansi, wahandisi au wataalamu wakubwa.
KWA HABARI ZAIDI INAENDELEA KWENYE GAZETI LA JAMHURI LA OKTOBA 6-12, 2026



