Benki ya Absa Tanzania imeongeza kiwango cha juu cha mikopo kwa watumishi wa umma kutoka Sh milioni 200 hadi Sh milioni 300, hatua inayolenga kuwawezesha kupata fedha zaidi kwa ajili ya mahitaji binafsi na shughuli za maendeleo.

Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za benki hiyo kuboresha huduma za mikopo kwa kurahisisha upatikanaji wa fedha, kuongeza kasi ya utoaji wa huduma na kuboresha mifumo ya ukopaji.

Akizungumzia maboresho hayo, Mkurugenzi wa Huduma za Kibenki kwa Wateja Binafsi na Wateja Maalumu wa Absa Tanzania, Ndabu Swere, amesema mpango huo unaendana na dhamira ya benki hiyo ya kutoa huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wateja wake.

Amesema ongezeko la kiwango cha mkopo, muda mrefu zaidi wa marejesho pamoja na uwezo mkubwa wa kukopa vitawawezesha watumishi wa umma kupata fedha kwa ajili ya elimu, uwekezaji katika biashara na shughuli nyingine za kiuchumi.

“Vigezo hivi vipya vya mikopo vitawapa wakopaji unyumbufu zaidi wa kifedha na kuwawezesha kutekeleza mahitaji muhimu pamoja na mipango yao ya maendeleo,” amesema.

Aidha, benki hiyo imeongeza uwiano wa makato ya mshahara kwa ajili ya marejesho ya mikopo (Debt Service Ratio – DSR) kutoka asilimia 50 hadi 67, hatua itakayowawezesha watumishi wanaokidhi vigezo kutenga sehemu kubwa zaidi ya mishahara yao kulipia mikopo na hivyo kupata mikopo mikubwa zaidi.

Ameongeza kuwa huduma hizo zitaambatana na mipango ya bima inayolenga kuwalinda wakopaji dhidi ya changamoto zisizotarajiwa, hivyo kuongeza usalama katika mikopo wanayoipata.

Kwa upande wake, Mkuu wa Bidhaa na Mikakati ya Huduma za Rejareja wa Absa Bank, Heristraton Genesis, amesema maboresho hayo yamekuja wakati muafaka kuelekea msimu wa sikukuu, ambapo watumishi wa umma wanahitaji uwezo mkubwa wa kifedha kukidhi mahitaji mbalimbali.

Amesema huduma hizo zimeandaliwa kuwafikia watumishi wa umma katika kada mbalimbali zikiwemo walimu, madaktari, wauguzi na maprofesa wa vyuo vikuu, ili kuwawezesha kugharamia mahitaji kama kodi ya nyumba, ada za shule na majukumu mengine ya kifamilia.