Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

MBUNGE wa Jimbo la Kibaha Mjini, Silvestry Koka, ameiwasilisha kwa Serikali kero ya upatikanaji wa maji katika Kata ya Pangani na maeneo mengine ya jimbo hilo, akilalamikia kusuasua kwa utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Pangani–Kibaha wenye thamani ya Sh bilioni 9.8 ambao hadi sasa umefikia asilimia 13 pekee.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Stendi ya Zamani ya Maili Moja, Kibaha, Novemba 18, 2026, mbele ya Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Koka alisema mradi huo uliosainiwa mwaka 2023 umepitia changamoto mbalimbali na kuchelewa kukamilika licha ya wananchi kuwa na matumaini makubwa ya kupata huduma ya maji.

Alisema mradi huo sasa una takribani miaka mitatu tangu kusainiwa, lakini maendeleo yake hayaridhishi, hali inayowafanya wananchi kuendelea kukabiliwa na changamoto ya maji.

“Wananchi wamekata tamaa, mbali na Kata ya Pangani kukosa maji, wananchi wa Lulanzi, Viziwaziwa na Kilimahewa wanataabika kwa maji,” alisisitiza Koka.

Mbunge huyo alitaja pia changamoto nyingine kuwa ni uhitaji wa huduma ya usafiri wa mwendokasi, ujenzi wa barabara ya Kongowe–Soga–SGR kwa kiwango cha lami pamoja na kukamilishwa kwa sehemu iliyobaki ya barabara ya Tamco–Mapinga, akieleza kuwa ni miundombinu muhimu katika kukuza uchumi na kurahisisha usafirishaji.

Aliongeza kuwa hakuna sababu ya wananchi kusubiri hadi tenki likamilike ndipo wapate maji, hivyo akamuagiza Mkurugenzi wa DAWASA kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili huduma ianze kupatikana kadri miundombinu inavyokamilika.

Kwa upande wake, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba alisema kuchelewa kwa mradi huo hakukutokana na uzembe wa mbunge wala taasisi husika, bali Serikali ilielekeza fedha katika baadhi ya miradi mikubwa ya kimkakati.

Alieleza baada ya kukamilika kwa miradi hiyo ya kimkakati, Serikali inaendelea kuelekeza nguvu katika kukamilisha miradi mingine na kuhakikisha wakandarasi wanalipwa ili kazi ziendelee, huku akiwaomba wananchi kuwa na subira wakati hatua hizo zikiendelea.