Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

WAZIRI Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesema maboresho ya Kitambulisho cha Taifa (Toleo la 2026) yatachangia kurahisisha upatikanaji wa huduma za kijamii na kiuchumi, kupunguza usumbufu kwa wananchi, kuimarisha utawala bora na kuongeza ufanisi katika shughuli za maendeleo nchini.

Nchemba ameyasema hayo Novemba 18,2026 mkoani Pwani wakati akizindua kitambulisho hicho kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa uwekezaji huo wa kisasa unalenga kuboresha mfumo wa utambulisho na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.

Amesema mradi huo ni uwekezaji mkubwa utakaowezesha vitambulisho kuunganishwa na mifumo ya taasisi mbalimbali, hivyo kuwawezesha wananchi kupata huduma nyingi kupitia mfumo mmoja wa utambulisho.

“Vitambulisho hivi vitapunguza usumbufu na kuongeza ufanisi.”

” Uwekezaji huu utaleta matokeo ya kuhakikisha Mtanzania anapata kitambulisho kwa wakati, hili ni suala muhimu na la msingi,” anasema Nchemba.

Aliongeza kuwa kitambulisho hicho kitakuwa nyenzo muhimu katika kurahisisha upatikanaji wa huduma na shughuli za kijamii na kiuchumi, pamoja na kuchochea maendeleo kwa kuwawezesha wananchi kutambulika kwa urahisi katika mifumo mbalimbali.

Kadhalika alisema mradi huo una maana pana zaidi ya kutoa vitambulisho, kwani unajenga utambulisho wa pamoja, mshikamano na udugu miongoni mwa Watanzania, huku ukiwa sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayosisitiza matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma na kuharakisha maendeleo ya nchi.

SALAMU ZA MKUU WA MKOA WA PWANI

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, ameishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi pamoja na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa kuuchagua Mkoa wa Pwani kuwa mwenyeji wa uzinduzi wa kitambulisho kipya cha Taifa kilichoboreshwa, Toleo la 2026, akieleza kuwa mkoa huo umekuwa wa kwanza kunufaika na huduma hiyo bila changamoto ya foleni.

Alieleza uzinduzi huo ni hatua muhimu katika kuboresha mfumo wa utambulisho wa Taifa, kuongeza ufanisi wa utambuzi wa watu, kuimarisha usalama wa taarifa za wananchi na kurahisisha upatikanaji wa huduma zinazohitaji utambulisho rasmi.

Anasema Serikali ya Mkoa itahakikisha viongozi wanashirikiana na NIDA katika utekelezaji wa mpango huo ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa urahisi na kujikinga na vitendo vya utapeli.

MKURUGENZI MKUU NIDA NA KATAMBI

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, James Kaji, alisema idadi ya magari ya kuhudumia wananchi imeongezeka kutoka 28 hadi 140 tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani, pamoja na kupatikana kwa boti za kisasa zinazowezesha kufikisha huduma katika maeneo ya ziwa na visiwani.

Alisema pia bajeti ya mamlaka hiyo imeongezeka mara tatu, huku akiwataka wananchi ambao hawajachukua vitambulisho vyao kuvifuata ndani ya miezi mitatu.

Kaji alisisitiza kuwa vitambulisho vya zamani havitafutwa wala kusitishwa kutumika, bali vitatumika sambamba na vitambulisho vipya, ambavyo vitatolewa pia kwa wananchi waliopoteza vyao au wanaohitaji kubadilishiwa kwa hiari.

Alieleza kuwa kitambulisho hicho kimeboreshwa ili kurahisisha uhusishaji wa huduma mbalimbali, zikiwemo bima ya afya, vyeti vya kuzaliwa, namba za utambulisho wa mlipa kodi (TIN), pasipoti na taarifa za ndoa.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, alisema kitambulisho hicho kitaimarisha ulinzi na usalama wa wananchi, akibainisha kuwa hadi sasa NIDA imezalisha vitambulisho milioni 21.5, ambapo milioni 19.6 vimechukuliwa na wananchi, huku vingine 1,832,683 vikiwa bado havijachukuliwa.

Aidha, alizitaka kampuni za simu kuhakikisha zinazima namba ambazo hazijasajiliwa au kuingizwa katika mfumo wa NIDA, akieleza kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti vitendo vya wizi na uhalifu unaofanyika kupitia mitandao ya simu.