Rais Hakainde Hichilema ameshinda uchaguzi wa urais Zambia kwa asilimia 60 ya kura, huku mpinzani wake Brian Mundubile akipata asilimia 38 na kudai kuwapo kwa dosari.

Rais Hakainde Hichilema amechaguliwa tena kuiongoza Zambia kwa muhula wa pili baada ya kupata karibu asilimia 60 ya kura katika uchaguzi mkuu uliofanyika Agosti 13.

Tume ya Uchaguzi ya Zambia ilitangaza matokeo hayo mapema Jumanne, ikisema mpinzani mkuu Brian Mundubile alipata karibu asilimia 38 ya kura.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Mwangala Zaloumis, amesema matokeo ya majimbo matano kati ya 226 yalikuwa bado hayajawasilishwa, lakini hayawezi kubadilisha matokeo ya jumla.

Katika ujumbe wake baada ya ushindi huo, Hichilema, mwenye umri wa miaka 64, alisema amenyenyekezwa na imani ambayo wananchi wameweka kwake. Pia aliahidi kuwahudumia hata wale waliounga mkono wagombea wa upinzani.

Mamia ya wafuasi wa chama chake cha UPND walimiminika katika mitaa ya mji mkuu Lusaka, wakiwa wamevalia mavazi mekundu, kuimba, kucheza na kurusha fataki kusherehekea ushindi huo.