Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) Prof. Ephata Kaaya ameongoza kikao cha Bodi kilichofanyika hivi karibuni jijini Mbeya kwa lengo la kujadili na kutoa mwelekeo wa kimkakati kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Taasisi katika kuimarisha huduma za saratani nchini.
Kikao hicho kimewakutanisha wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya ORCI ambapo masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa mipango na shughuli za Taasisi yalijadiliwa.
Miongoni mwa masuala yaliyopewa uzito katika kikao hicho ni utekelezaji wa mipango ya Taasisi, uboreshaji wa huduma za saratani, usimamizi wa rasilimali pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na zenye ufanisi.
Bodi ilipataa taarifa kutoka kwa Menejimenti kuhusu utekelezaji wa shughuli za Taasisi na maendeleo katika maeneo mbalimbali ya kimkakati huku wajumbe wakitoa maoni na miongozo yenye lengo la kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya ORCI.
Akiongoza kikao hicho, Mwenyekiti wa Bodi Prof. Kaaya amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji, ufanisi na usimamizi madhubuti katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi, sambamba na kuendelea kuweka maslahi ya mgonjwa katika kiini cha huduma zinazotolewa.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dkt. Diwani Msemo aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Taasisi na kueleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa katika kuimarisha huduma za saratani na kufikia malengo yaliyowekwa.
Kikao hicho ni sehemu ya utaratibu wa Bodi ya Wadhamini wa ORCI wa kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Taasisi na kutoa mwelekeo wa kimkakati katika kuimarisha utoaji wa huduma za saratani nchini.
Kupitia vikao hivyo Bodi inaendelea kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha Taasisi inasimamiwa kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji huku ikizingatia azma ya Serikali ya kuimarisha huduma za saratani na kuboresha afya za wananchi.
Kabla ya kuanza kwa kikao hicho, wajumbe wa Bodi walipata fursa ya kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo cha Saratani cha ORCI Mbeya kinachojengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 11, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kusogeza huduma za kibingwa na kibobezi za saratani karibu na wananchi wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na nchi jirani.




