Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Bukoba

Kwa muda mrefu nimeandika mara kadhaa nikipinga harakati katika siasa na mara nyingi nikiwaeleza wanasiasa vijana, hasa hawa wadogo zetu akina John Heche na wenzake kuwa siasa za dunia hii si za kupambana kwa mikuki, mawe, mishale na bunduki.

Nimeeleza mara kadhaa kuwa siasa za Tanzania ni tofauti na za nchi jirani ya Kenya, hivyo zinaweza kuleta hisia kwa muda, lakini haziwezi kufanya kazi sawa sawa.

Sitanii, inawezekana sisi kizazi chetu cha Tanganyika African National Union (TANU), kina tofauti kubwa na kile cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), na sasa kuna tofauti kubwa zaidi na kizazi kilichotokana na upepo wa mabadiiko uliovuma kwa kasi kuanzia mwaka 1992. Nafahamu hapo katikati somo la historia halikupewa umuhimu, hivyo tukazalisha kizazi chenye utumwa wa kutofahamu.

Naishukuru serikali kwa kuanzisha somo maalumu la Historia ya Tanzania, ambalo sasa linafundishwa kwa vijana wetu hadi ngazi ya chuo kikuu.

Kwa hakika bila kuifahamu historia ya nchi yetu, tutaishia kufanya siasa za kwenye mitandao na TV kisha tunashangaa mbona hawatuelewi tunaowaambia? Nigusie kidogo tu, kisha nirejee kwenye mada ya leo.

Wakati sisi Tanzania kwa upande wa Tanganyika tulipata uhuru kwa njia ya mazungumzo, huku Zanzibar wakifanya mapinduzi ambayo vita yake ilidumu kwa saa 6 hivi. Ni wazi kufikia siku ya Uhuru wa Zanzibar kutoka Uingereza, kwa maana ya Desemba 10, 1963 hata huyo Sultani Jamshid bin Abdullah, alikuwa tayari ameishakosa amani kutokana na matokeo ya masanduku ya kura kuanzia miaka ya 1959.

Sitanii, Sultani alifahamu fika kuwa hata kwa kutumia ‘Gerrymandering’, ushindi kwao ilikuwa vigumu. Alikwishalegezwa na kauli za Mwalimu Julius Nyerere na yakatokea.

Ukitaka kufahamu mapinduzi ulizia Kenya mkakati wao wa Mzungu Arudi Ulaya na Mwafrika Apate Uhuru (MAUMAU). Ulizia, mapinduzi ya Ufaransa yalichukua miaka 10. Yalianza Julai 14, 1789 hadi Novemba 9, 1789. Nadhani sasa msomaji nikisema Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar nayo yalikuwa sehemu ya mazungumzo utanielewa. Wala siyadogoshi, ila kwa ujumla Tanganyika na Zanzibar, ni nyumbani kwa mazungumzo, ni nyumbani kwa siasa za amani.

Hapo katikati nilioni vyama vya upinzani hasa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakijaribu ku-copy na ku-pest siasa za Kenya hapa Tanzania.

Nikasema hili halitawezekana. Tanzania tunaendesha siasa zetu kwa hoja si kwa matusi, vitisho na kejeli. Tunayo mifano ya wanasiasa waliojenga hoja na wakafanikiwa kisiasa bila kujali wanatokea kwenye chama tawala au kwenye upinzani, mmoja wao akiwa Edward Ngoyai Lowassa.

Sitanii, kuna wakati katika maisha ya chama cha siasa ambapo wananchi huanza kujiuliza: Je, chama hiki kinataka kubadilisha nini katika maisha yangu? Na jibu la swali hilo haliwezi kupatikana kwenye makelele, matusi au kauli za kuwashambulia wapinzani au chama tawala. Linapatikana katika sera na mipango inayogusa maisha ya wananchi.

 Ndiyo maana kauli za Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, kuhusu umuhimu wa vijana na vyombo vya habari kuanza kuzungumzia zaidi uchumi kuliko michezo inastahili mjadala mpana.

Hapa ndipo CHADEMA inaweza kuanza kujijenga kama chama cha sera, badala ya kubaki katika taswira ya chama cha harakati.

Ni jambo moja kuipinga serikali au kukosoa chama tawala; ni jambo jingine kuwaeleza wananchi utakachofanya ukipata dhamana ya kuongoza nchi.

Mwananchi anataka kujua: Utatengeneza vipi ajira? Utawezaje kuongeza kipato cha mkulima? Vijana watawezaje kupata mitaji? Viwanda vitajengwaje? Biashara ndogo zitalindwaje? Kodi zitakuwaje? Na Tanzania itawezaje kuongeza uzalishaji na ushindani wa kimataifa? Hayo ndiyo maswali ya sera.

Kwa hiyo, kama Heche anaanza kusukuma mjadala wa uchumi wa wananchi, huo ni mwelekeo unaopaswa kuungwa mkono. CHADEMA inaweza kuwa na nafasi kubwa zaidi katika siasa za Tanzania ikiwa itaonyesha kwamba ina uwezo wa kugeuza malalamiko kuwa sera, na sera kuwa mipango ya utekelezaji.

Kwa muda mrefu, baadhi ya kauli za viongozi wa vyama vya upinzani zimekuwa zikijikita katika kuwashambulia viongozi wa CCM, hata kutumia neno kama “Ma-CCM” kama lugha ya kisiasa.

Wakati mwingine watoto wa viongozi nao wameingizwa katika mashambulizi ya kisiasa. Lakini ni lazima tuseme ukweli: kumtukana mtoto wa kiongozi au kumdhalilisha mpinzani si sera ya kumkomboa mwananchi kiuchumi.

Siasa za kisasa zinahitaji ushindani wa hoja, si mashindano ya matusi. Ukiona sera ya chama tawala haifai, ionyeshe haifai kwa nini. Kisha leta sera mbadala na ueleze itatekelezwaje. Hapo ndipo chama kinapokuwa na maana zaidi kwa mwananchi.

Hoja nyingine ya Heche kuhusu vijana kutumia muda mwingi kujadili michezo, wakati uchumi haujadadiliwi kwa kiwango kinachostahili, nayo inahitaji kutafakariwa. Michezo ni muhimu. Inaburudisha, inaunganisha jamii na ni sekta yenye fursa kubwa za ajira na biashara. Lakini nchi haiwezi kujenga uchumi wake kwa mijadala ya mpira pekee.

Hapa ndipo kauli ya Mshauri wa Rais wa Masuala ya Habari, Tido Mhando, inapopata uzito. Ameeleza kuwa alipokuwa akiendesha kipindi cha michezo Radio Tanzania, muda wa michezo ulikuwa takribani dakika 15, lakini leo michezo inaweza kuchukua hadi saa sita kwenye baadhi ya redio. Kama jamii tunapaswa kujiuliza: tunatumia muda wetu wa mijadala kwa mambo gani?

Tatizo si mpira. Tatizo ni uwiano. Tunahitaji mijadala ya michezo, lakini pia tunahitaji mijadala ya kilimo, viwanda, teknolojia, biashara, elimu ya fedha, masoko, ajira, ujasiriamali na uzalishaji. Vijana wanapaswa kujua matokeo ya ligi, lakini pia wajue kwa nini thamani ya bidhaa fulani inapanda, namna ya kuanzisha biashara, namna ya kupata masoko na kwa nini viwanda vinafunguliwa au kufungwa.

Vyombo vya habari vina wajibu mkubwa hapa. Kama taifa tunahitaji vyombo vya habari vinavyoburudisha, lakini pia vinavyofundisha na kuelimisha wananchi kuhusu uchumi.

Kwa hiyo, CHADEMA inapozungumza kuhusu uchumi wa wananchi, isirudi nyuma. Huu ndio mjadala ambao wananchi wanauhitaji. Lakini mjadala huo lazima uende mbali zaidi ya kauli. Ugeuke kuwa sera, mipango, vipaumbele na majibu yanayopimika.

CHADEMA ikifanikiwa kuacha siasa za matusi na kujenga utamaduni wa kushindana kwa sera, inaweza kupata heshima mpya katika siasa za Tanzania. Kwa sababu mwisho wa siku, mwananchi hataki tu kusikia nani amemtukana nani. Anataka kujua nani ana mpango wa kumsaidia yeye kuongeza kipato, kupata ajira, kuanzisha biashara na kuishi maisha bora.

Hapo ndipo siasa zinapokuwa na maana. Na hapo ndipo chama cha siasa kinapoacha kuwa cha harakati pekee na kuanza kuwa chama cha sera na maendeleo ya wananchi.

Narudi, mkondo wa kuzungumza maendeleo ya uchumi uliouanza Heche, naomba uuedeleze. Hii itawapa nafasi vijana na Watanzania kupata mawazo mbadala ya jinsi ya kujikomboa kiuchumi. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827