Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Wiki iliyopita, siasa za Uchumi wa Afrika Mashariki zilichemka tena katika mitandao ya kijamii, baada ya Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni na Kampuni ya Vitol Bahrain E.C kutiliana saini makubaliano ya awali ya kuiendeleza Tanga kuwa kitovu cha nishati cha kikanda kwa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta. Hii ni fursa ambayo Tanzania haipaswi kuichezea.
Sitanii, ukubwa wa mshirika aliyeingia katika mpango huu unaifanya Tanga iangalie mbele kwa matumaini makubwa. Kampuni ya Vitol si kampuni ya kawaida katika biashara ya mafuta duniani. Vitol ni miongoni mwa makampuni makubwa sita duniani yanayojihusisha na biashara ya nishati.
Kwa mujibu wa taarifa za kampuni hiyo, mwaka 2024 Vitol ilisafirisha wastani wa mapipa milioni 7.2 ya mafuta ghafi na bidhaa za mafuta kwa siku, ikiwa na uwezo wa kusafisha zaidi ya mapipa 850,000 kwa siku. Kampuni hiyo pia ina mtandao mkubwa wa vituo vya mafuta na biashara katika masoko mbalimbali duniani.

Sitanii, Tanzania inapokaa mezani na Vitol, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Taifa la Mafuta Uganda (UNOC), haipaswi kuangalia tu saini zilizowekwa kwenye Hati ya Makubaliano. Inapaswa kuangalia mtandao mkubwa wa biashara, mtaji, utaalamu, miundombinu na masoko unaoweza kuunganishwa na Tanga.
Tanga tayari ina faida kubwa ya kijiografia. Ni kituo cha mwisho cha Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), linalounganisha Hoima nchini Uganda na Chongoleani, Tanga.
Hivyo, kuiendeleza Tanga kuwa kitovu cha nishati kunaweza kuifanya Tanzania isiwe tu nchi inayopitisha mafuta, bali kuwa kituo muhimu cha kuhifadhi, kusindika, kusafirisha na kufanya biashara ya nishati kwa soko la Afrika Mashariki na masoko mengine.
Lakini hapa ndipo serikali inapaswa kuwa makini. Mradi wenye thamani ya karibu dola bilioni 20 hauwezi kubaki kwenye mikutano, picha za viongozi na hati zinazowekwa kwenye mafaili.
Tanzania inahitaji kuona ratiba ya utekelezaji, uwekezaji, ujenzi wa miundombinu, ajira na shughuli za kibiashara zikianza kuonekana. Kwa lugha rahisi, Tanga inahitaji magreda, mitambo, mabomba na vituo vya kuhifadhia mafuta; si makabrasha pekee.
Sitanii, kuna jambo jingine linalovutia katika mpango huu. Kumekuwa na taarifa kwamba mfanyabiashara mkubwa wa Afrika, Aliko Dangote, ambaye aliwahi kuhusishwa na wazo la kujenga kiwanda kikubwa cha kusafisha mafuta Tanga, baadaye alielekeza macho yake nchini Kenya.
Zipo taarifa kwamba Dangote aliona uwepo wa mazungumzo ya mradi huu mkubwa kati ya Tanzania, Uganda na Kampuni ya Vitol kuwa ni tishio. Hii ingeleta ushindani mkubwa kwake. Akakimbia! Hii ndiyo Waswahili husema: “Kuvuja kwa pakacha, nafuu kwa mchukuzi.”
Hata hivyo, hoja hii inapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari hadi sababu hizo zithibitishwe rasmi. Kilicho muhimu zaidi si kujadili nani anamshinda nani, bali kutambua kwamba uwepo wa wawekezaji wakubwa kama Vitol kunaonyesha thamani ya kimkakati ya Tanga katika biashara ya nishati.
Serikali inapaswa kuhakikisha makubaliano haya hayaishii kuwa kumbukumbu nzuri ya hafla ya Ikulu. Yanapaswa kufuatiwa na hatua za haraka, mpango wa utekelezaji wenye muda maalumu, mazingira rafiki ya uwekezaji, miundombinu bora, uwazi katika utekelezaji na ulinzi wa masilahi ya taifa.

Tanzania pia inapaswa kuhakikisha wananchi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla wanafaidika na mradi huu kupitia ajira, biashara, kodi, huduma na fursa za uwekezaji kwa wazawa.
Tanga ikifanikiwa, haitakuwa tu bandari ya Tanzania, bali inaweza kuwa moyo wa biashara ya nishati wa Afrika Mashariki, na Tanzania inaweza kuwa lango muhimu la nishati kwa ukanda mzima.
Sitanii, ukiacha uwezekano mkubwa wa bei za mafuta kushuka, naomba nieleze kwa uchache faida 15 za kiwanda cha kusafisha mafuta, ili msomaji upate mwanga kuwa kiwanda cha kusafisha mafuta si suala dogo kama linavyotajwa na baadhi ya watu.
Baadhi ya bidhaa zinazotokana na kiwanda cha kusafisha mafuta ni:- 1. Petroli (Gasoline/Petrol) – kwa magari, pikipiki na mitambo. 2. Dizeli (Diesel) – kwa magari, malori, mabasi, mitambo ya viwandani na jenereta. 3. Mafuta ya taa (Kerosene) – kwa matumizi mbalimbali ya nishati. 4. Jet fuel/mafuta ya ndege – kwa ndege. 5. Mafuta mazito (Fuel oil) – kwa viwanda, meli na mitambo mikubwa.
Nyingine ni:- 6. LPG (gesi ya kupikia) – kwa matumizi ya majumbani, biashara na viwandani. 7. Naphtha – malighafi muhimu kwa viwanda vya petrochemical. 8. Lami (Bitumen/Asphalt) – kwa ujenzi wa barabara na paa. 9. Mafuta ya kulainishia mitambo (lubricating oils) – kwa magari, mashine na mitambo. 10. Parafini (Paraffin wax) – hutumika katika mishumaa, vifungashio, vipodozi na viwanda mbalimbali.
Faida bado zipo:- 11. Petroleum coke (Petcoke) – hutumika kama nishati na katika baadhi ya viwanda, ikiwamo saruji na uzalishaji wa alumini. 12. Sulfur (Salfa) – hutumika kutengeneza mbolea, asidi ya sulfuriki na bidhaa nyingine za viwandani. 13. Petrochemical feedstocks – malighafi zinazotumika kutengeneza kemikali mbalimbali.
Nimesema angalau nitaje faida 15, hivyo faida ya 14. Plastiki – kwa kawaida plastiki haitoki moja kwa moja kwenye refinery; hutengenezwa zaidi katika viwanda vya petrochemical vinavyotumia bidhaa kama ethylene, propylene na naphtha zinazotokana na mafuta. 15. Mbolea – refinery yenyewe si lazima itengeneze mbolea moja kwa moja, lakini bidhaa zake za petrochemical zinaweza kuwa sehemu ya mnyororo wa uzalishaji wa kemikali; hasa ammonia na urea hutengenezwa zaidi kwa kutumia gesi asilia kama malighafi.
Sitanii, bidhaa hizo 15 nilizozitaja zinazotokana na usafishaji wa mafuta, huchukua sehemu kubwa ya pato la taifa letu. Ni kwa mantiki hiyo, nasema kiwanda cha kusafisha mafuta Tanga, mbali na kuwa tanuri la ajira kwa wingi wa viwanda vinavyotokana na usafishaji huo, kinayo nafasi ya kuliingizia taifa letu fedha za kigeni na kupunguza matumizi ya fedha zetu za kigeni kwani bidhaa hizi muhimu sasa tutazipata Tanga.
Naamini Waziri wa Nishati, Deogratias Ndejembe atafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha kiwanda hiki kinajengwa. Ndiyo, ninapongeza hatua ya kusaini makubaliano, lakini sasa natamani kuona vitendo zaidi kuliko maneno. Mungu ibariki Tanzania.



0784 404827

