Na Jackline Minja, WMJJWM – Loliondo, Arusha
Serikali imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuwawezesha wanawake na makundi maalum katika jitihada za kuwaletea maendeleo, ikiwemo kutoa elimu katika masuala ya umiliki wa mali na ardhi, mafunzo ya ujasiriamali na usimamizi wa fedha.
Akizungumza kwa nyakati tofauti, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema Serikali itaendelea kutoa huduma za msaada wa kisheria na kijamii kwa wajane na wanawake wanaokutana na changamoto za unyanyasaji au migogoro ya mirathi, huku akiziasa familia kuacha kuwanyanyasa wanawake wajane wanapopatwa na madhila ya kuondokewa na wenza wao na badala yake kuwasaidia kupata haki zao na kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Aidha, Mhe. Mahundi amewapongeza wajane na wanawake wa Wilaya ya Ngorongoro kwa kuanzisha na kuendeleza mitandao yao pamoja na vikundi vya wanawake, hatua ambayo imewawezesha kuungana, kusaidiana na kupata fursa za kiuchumi, huku akiwasisitiza kuendelea kukemea mila potofu ikiwemo ukeketaji wa watoto na kuwaasa kwamba kila mzazi ana wajibu wa kulea watoto wake na vijana waliofanikiwa wanapaswa kuwahudumia wazazi wao badala ya kuwaacha waje kulelewa na Serikali.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo hilo, Mhe. Yannick Ndoinyo, amesema atahakikisha kila changamoto iliyowasilishwa na vikundi vya wajane na wazee inafanyiwa kazi kwa kushirikiana na mamlaka husika, ili kuendelea kuwawezesha wazee kushiriki katika shughuli za maendeleo na kutumia uzoefu wao katika kulijenga taifa, hususan katika kutoa ushauri na malezi kwa kizazi cha sasa na kijacho.
Katika taarifa iliyowasilishwa na wajane hao, imeelezwa kuwa baadhi yao wamejiunga katika vikundi vya kiuchumi na kijamii vinavyofanya shughuli mbalimbali, ikiwemo biashara ndogo ndogo, ufugaji, kilimo na ushonaji huku vikundi hivyo tayari vimeanza kupata mikopo ya Serikali, hatua inayosaidia kuimarisha shughuli zao za uzalishaji na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi.
Ziara hiyo imehusisha pia kutembelea baadhi ya vikundi vya wanawake na shughuli za kuwawezesha wazee, ikiwemo Kikundi cha Tupendane Loliondo, Mradi wa Wazee wa WASSO pamoja na Kikundi cha Naretu Sukenya.








