Na Stella Aron, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Licha ya kuwa miongoni mwa makundi yaliyo katika hatari kubwa wakati wa majanga, watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali nchini bado wanakabiliwa na changamoto ya kupata elimu na taarifa za tahadhari kuhusu mafuriko yanayosababishwa na mvua kubwa za El Niño.
Hali hiyo inazua wasiwasi kuhusu ushirikishwaji wao katika mipango ya kukabiliana na majanga, ikizingatiwa kuwa kupata taarifa sahihi kwa wakati ni hatua muhimu katika kuokoa maisha na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Mvua kubwa zinazosababisha mafuriko zimeendelea kuwa tishio kwa maisha ya wananchi, makazi na shughuli za kiuchumi. Wakati mamlaka mbalimbali zikiendelea kutoa elimu na tahadhari kuhusu athari za mvua hizo, bado kuna uwezekano wa baadhi ya wananchi kushindwa kupata ujumbe huo kutokana na mifumo ya mawasiliano kutokuzingatia mahitaji yao.
Miongoni mwa makundi hayo ni watu wenye ulemavu wa kusikia, kuona, viungo, akili na watu wenye ualbino pamoja na aina nyingine za ulemavu.
Kwa makundi hayo, kupata taarifa kuhusu mvua kubwa, maeneo yanayoweza kukumbwa na mafuriko, muda wa kuhamia maeneo salama na hatua za kujikinga si jambo la kawaida tu, bali ni suala linalohusiana moja kwa moja na usalama wa maisha yao.
Kwa mfano, mtu mwenye ulemavu wa kusikia anaweza kushindwa kupata ujumbe unaotolewa kupitia redio au matangazo ya televisheni endapo hakuna mkalimani wa lugha ya alama au maandishi yanayoambatana na matangazo hayo.
Kwa upande wa mtu mwenye ulemavu wa kuona, taarifa zinazotolewa kupitia mabango, picha na machapisho zinaweza kuwa vigumu kuzifikia endapo hazijaambatana na maelezo ya sauti au teknolojia saidizi zinazomwezesha kuelewa ujumbe uliokusudiwa.
Hali ni tofauti kidogo kwa watu wenye ulemavu wa viungo, hasa wanaotumia viti vya magurudumu, magongo au wanaohitaji msaada katika kutembea. Kwa kundi hili, changamoto haiko katika kupata taarifa pekee, bali pia uwezo wa kutekeleza maelekezo ya kujiokoa.
Kwa mfano, mtu anaweza kupata taarifa kwamba anatakiwa kuhama eneo analoishi kutokana na hatari ya mafuriko, lakini akakosa msaada wa kumwezesha kufika eneo salama. Hali inaweza kuwa mbaya zaidi pale barabara zinapofunikwa na maji, madaraja yanapoharibika au njia za kupita zinapokuwa na matope.
Kwa watu wenye ulemavu wa akili au changamoto za utambuzi, ujumbe wa tahadhari unahitaji kutolewa kwa lugha rahisi, sentensi fupi, picha na maelekezo ya hatua kwa hatua. Taarifa ngumu za kitaalamu kuhusu mwenendo wa mvua, viwango vya maji na maeneo hatarishi zinaweza kuwa vigumu kueleweka bila kufafanuliwa.
Hali hizo zinaonesha kuwa kutoa taarifa kwa umma pekee hakutoshi kuhakikisha kila mwananchi anapata elimu na kuchukua hatua za kujilinda. Mifumo ya utoaji taarifa inapaswa kuzingatia mahitaji tofauti ya wananchi ili kusiwe na kundi linaloachwa nyuma.
Akizungumza na Jamhuri Digital, Mwenyekiti Msaidizi wa Chama cha Watu wenye Ualbino Tanzania (TAS), Alfred Kapole, amesema bado kuna changamoto katika kuwafikishia watu wenye ulemavu elimu kuhusu namna ya kujikinga na athari za mvua za El Niño.
Amesema Serikali, mamlaka husika, wadau, taasisi na mashirika yanapaswa kuunganisha nguvu katika kutoa elimu kwa makundi hayo badala ya kuyaacha nyuma.
“Nina imani kuwa bado elimu haijawafikia makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu. Hivyo, mamlaka husika, Serikali, wadau, taasisi na mashirika washirikiane katika kutoa elimu kwa makundi hayo, kwani nao wanastahili kupata elimu kama wengine,” amesema.
Akifafanua changamoto zinazowakabili baadhi ya makundi hayo, Kapole amesema watu wenye ulemavu wa kuona wanaweza kupata ugumu wa kutambua mwelekeo wa maji wakati wa mafuriko na kuchukua tahadhari zinazofaa.
Vilevile, watu wenye ulemavu wa viungo wanaweza kushindwa kuondoka kwa haraka katika maeneo hatarishi kutokana na changamoto za kutembea.
Amesema upatikanaji wa elimu mapema utawasaidia watu wenye ulemavu kujua hatua za kuchukua kabla ya mvua kuanza kunyesha na hali kuwa mbaya.
“Kama kundi hili litapata elimu mapema, itawasaidia kujua namna ya kuondoka katika maeneo hatarishi kabla ya kuanza kwa mvua ambazo Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari zake. Tayari tumeanza kushuhudia baadhi ya mikoa ikipata mvua kubwa na kusababisha madhara,” amesema.
Ameongeza kuwa watu wenye ulemavu wa kusikia nao wanahitaji kuelimishwa mapema ili waweze kuondoka katika maeneo hatarishi kabla ya mvua kuanza, badala ya kusubiri mpaka mafuriko yatokee.
MAFURIKO YA EL NIÑO NA ATHARI ZAKE

Tanzania tayari imewahi kushuhudia madhara makubwa yaliyotokana na mvua nyingi zilizohusishwa na hali ya El Niño katika msimu wa mwaka 2023/2024.
Kwa mujibu wa taarifa ya Benki ya Dunia kuhusu mwitikio wa Tanzania dhidi ya athari za El Niño na Kimbunga Hidaya, mvua zilizozidi wastani katika misimu ya Oktoba hadi Desemba 2023 na Machi hadi Mei 2024 zilisababisha mafuriko, maporomoko ya ardhi na uharibifu wa miundombinu katika maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa maporomoko ya matope yaliyotokea eneo la Mlima Hanang, mkoani Manyara, Desemba 2023 yalisababisha vifo vya watu 94 na kuathiri zaidi ya watu 1,700.
Aidha, taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kuhusu hali ya hewa ya mwaka 2023 inaonesha kuwa mvua kubwa za Novemba mwaka huo zilisababisha mafuriko katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam, Zanzibar, Mafia na Tanga.
Madhara hayo yanaonesha umuhimu wa kuwa na mifumo madhubuti ya tahadhari za mapema inayohakikisha kila mwananchi anapata taarifa na kuwa na uwezo wa kuchukua hatua za kujikinga, hususan watu wenye ulemavu ambao wanaweza kukabiliwa na vikwazo vya ziada wakati wa majanga.
ELIMU YA MAJANGA IZINGATIE MAHITAJI YA WENYE ULEMAVU

Akizungumza na mwandishi wa makala haya, Mwanasheria Emmanuel Majeshi, ambaye ni mtu mwenye ulemavu wa kuona na Mkuu wa Dawati la Watetezi la Watu wenye Ulemavu katika Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), amesema wataalamu wa masuala ya kupunguza athari za majanga wanapaswa kuhakikisha mifumo ya utoaji taarifa inatumia njia mbalimbali za mawasiliano.
Amesema kufanya hivyo kutasaidia kuhakikisha taarifa za tahadhari zinawafikia watu wenye ulemavu wa aina zote kwa wakati na kwa namna wanayoweza kuzielewa.
Kwa mujibu wa mwongozo wa CBM kuhusu usambazaji wa taarifa za tahadhari za majanga, mifumo ya mawasiliano inapaswa kutumia njia zinazochanganya sauti na picha, lugha ya alama, maandishi ya nukta nundu (Braille) na ujumbe rahisi kueleweka.
Akifafanua umuhimu wa njia hizo, Majeshi amesema elimu kuhusu athari za El Niño haipaswi kutegemea redio, televisheni au mikutano ya hadhara pekee, bali inapaswa kutolewa kwa kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
“Kwa mfano, matangazo ya televisheni kuhusu tahadhari za mvua yanapaswa kuambatana na wakalimani wa lugha ya alama na maandishi. Kwa watu wenye ulemavu wa kuona, taarifa hizo zinapaswa kupatikana kupitia sauti na teknolojia zinazowawezesha kusikiliza maudhui,” amesema.
Majeshi ameongeza kuwa mikutano ya kutoa elimu kwa wananchi inapaswa kuandaliwa katika maeneo yanayofikika kwa urahisi, hasa kwa watu wanaotumia viti vya magurudumu na wale wenye changamoto za kutembea.
Amesema kutokuwepo kwa mazingira rafiki kunaweza kuwazuia watu hao kushiriki katika mikutano inayolenga kuwapa elimu muhimu ya kujikinga na majanga.
Kwa mantiki hiyo, ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu unapaswa kuanzia katika hatua za kupanga na kuandaa mikakati ya kukabiliana na majanga, badala ya kusubiri mpaka mafuriko yatokee ndipo waanze kutafutiwa msaada.
SERIKALI, TMA NA WADAU WANALO JUKUMU
Ili kupunguza hatari zinazowakabili watu wenye ulemavu wakati wa mafuriko, kuna umuhimu wa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia masuala ya maafa, TMA, mamlaka za Serikali za Mitaa na mashirika ya watu wenye ulemavu kushirikiana katika kuhakikisha elimu ya majanga inawafikia wananchi wote.
Hatua muhimu ni kuwashirikisha watu wenye ulemavu katika kuandaa mipango ya kukabiliana na mafuriko, badala ya kuwachukulia kama wapokeaji wa misaada pekee.
Vilevile, maeneo yanayotengwa kwa ajili ya hifadhi ya muda wakati wa mafuriko yanapaswa kuwa rafiki kwa watu wenye ulemavu, yakiwa na njia zinazorahisisha kuingia na kutoka pamoja na huduma zinazozingatia mahitaji yao.
Elimu ya kujikinga na mafuriko inapaswa pia kutolewa kupitia vyama vya watu wenye ulemavu, shule, vituo vyao na maeneo wanayoishi ili kuhakikisha wanapata taarifa mapema.
Jambo jingine muhimu ni kuweka utaratibu maalumu wa kuwafikia watu wenye ulemavu wanaoishi peke yao au wasiokuwa na watu wa kuwasaidia wakati wa dharura.
Akizungumzia suala hilo, Majeshi amesema haki ya kupata taarifa za tahadhari za majanga haipaswi kutegemea uwezo wa mtu kusikia, kuona, kutembea au kuelewa ujumbe unaotolewa kwa njia moja pekee.
Amesema watu wenye ulemavu ni sehemu ya jamii na wanapaswa kupata elimu ya kutosha kuhusu athari za mvua za El Niño, namna ya kujikinga na hatua za kuchukua wakati wa mafuriko.
Ameonya kuwa endapo mifumo ya utoaji elimu na tahadhari haitazingatia mahitaji ya makundi hayo, juhudi za kukabiliana na mafuriko zinaweza kuyaacha nyuma baadhi ya makundi yanayohitaji ulinzi zaidi.
FDH YATOA WITO WA KUWAPA KIPAUMBELE WENYE ULEMAVU

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH), Maiko Salali, amewataka wadau mbalimbali kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapewa kipaumbele katika maandalizi ya kukabiliana na majanga yanayosababishwa na mvua za El Niño.
Salali, amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kupata elimu na taarifa za tahadhari kwa wakati ili waweze kujiandaa na kuchukua hatua za kujilinda.
Amesema FDH linaendelea kufuatilia taarifa na utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na TMA kuhusu mvua na madhara yanayoweza kujitokeza, huku likishirikiana na Serikali pamoja na mamlaka husika katika kutoa elimu na tahadhari kwa watu wenye ulemavu.
“Wenye ulemavu ni miongoni mwa makundi yanayoweza kuathirika zaidi wakati wa majanga kutokana na changamoto zinazohusiana na aina mbalimbali za ulemavu. Ni muhimu taarifa za tahadhari kuhusu El Niño na majanga mengine ziwafikie watu wenye ulemavu kwa wakati na kwa namna inayowawezesha kuzifahamu na kuchukua hatua stahiki za kujilinda,” amesema.
Salali amesema ni muhimu wadau kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata elimu na msaada unaowawezesha kukabiliana na athari za majanga.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali, wazazi, walezi na Watanzania kwa ujumla kushirikiana kuhakikisha kundi hilo haliachwi nyuma katika mipango ya kukabiliana na athari za El Niño.
Amesema baadhi ya watu wenye ulemavu wanaweza kukabiliwa na vikwazo vya kupata huduma, taarifa na fursa mbalimbali wakati wa majanga, hivyo programu za tahadhari, uokoaji na utoaji wa misaada zinapaswa kuzingatia mahitaji yao.
Aidha, amewataka watu wenye ulemavu kufuatilia kwa karibu taarifa zinazotolewa na TMA pamoja na mamlaka nyingine zinazohusika ili waweze kuchukua hatua mapema pale tahadhari zinapotolewa.
“FDH itaendelea kutoa elimu na kushirikiana na Serikali na mamlaka husika kuhakikisha taarifa muhimu zinawafikia watu wenye ulemavu na kuwawezesha kujiandaa kukabiliana na athari za majanga.
“Tunawaomba Watanzania tushirikiane kulisaidia kundi hili ili liweze kupata uelewa wa kutosha na namna ya kukabiliana na changamoto hizi, ili tujenge jamii ambayo haimuachi mtu nyuma,” amesema Salali.
Kwa ujumla, suala la usalama wakati wa mafuriko haliwezi kutenganishwa na haki ya kila mwananchi kupata taarifa na huduma zinazomwezesha kujilinda. Watu wenye ulemavu hawapaswi kuwa watazamaji katika mipango ya kukabiliana na majanga, bali washirikishwe kikamilifu katika maandalizi, utoaji wa elimu na hatua za uokoaji.
Ni muhimu Serikali na wadau kuhakikisha mifumo ya tahadhari za mapema inazingatia mahitaji ya watu wote, kuanzia namna taarifa zinavyotolewa hadi hatua za kuwahamisha walio katika maeneo hatarishi.
MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU (NOVEMBA, 2026 HADI APRILI 2027)
Mvua za Msimu ni mahususi katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kanda ya kati, nyanda za juu kusini magharibi, kusini mwa nchi, ukanda wa pwani ya kusini pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro. Maeneo haya yanapata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, unaoanza mwezi Novemba na kuisha kati ya mwezi Aprili na Mei ya mwaka unaofuata.
Kutokana na mifumo ya hali ya hewa inayotarajiwa (kama inavyoelezwa katika kipengele cha 2 cha taarifa hii), mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa pamoja na maeneo ya kusini mwa mkoa wa Morogoro. Hata hivyo, mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani
zinatarajiwa katika mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi.
Mvua za Msimu zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma, Lindi na Mtwara na kusambaa katika maeneo mengine mwezi Novemba 2026. Mvua hizi zinatarajiwa kuisha kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Aprili, 2027 katika maeneo mengi.
Mvua nyingi zinatarajiwa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2026 – Januari, 2027), ikilinganishwa na nusu ya pili (Februari – Aprili, 2027). Maelezo ya kina juu ya mwelekeo wa mvua hizo za msimu ni kama ifuatavyo:
