Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia, Dodoma
SERIKALI imewataka watafiti nchini wafanye tafiti zinazojibu maswali ya wananchi na zinazoonyesha namna ya kuongeza ajira, kuongeza uzalishaji, kupanua soko, na kuboresha maisha ya watu.
Hayo yamesemwa leo mkoani Dodoma na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Dk Pius Chaya kwenye ufunguzi wa kongamano la tano la kimataifa la usimamizi wa biashara na maendeleo ya kiuchumi lililoandaliwa na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA).
Alisema ukuaji wa uchumi una maana tu pale unapogusa maisha ya Mtanzania wa kawaida kwa hiyo ni vyema mikakati ikajikita kujenga uchumi shindani na jumuishi na kuhakikisha kila Mtanzania anashiriki na kunufaika na ukuaji wa uchumi, kupitia ajira, biashara na uzalishaji.
Alisema tafiti zinapaswa kujikita kuangalia namna ya kukuza viwanda na kilimo tija, kuongeza thamani ya mazao yetu hapa nchini, kuongeza ajira vijijini na mijini, na kupunguza utegemezi wa kuuza malighafi.
Alisema kuna umuhimu mkubwa kuendeleza rasilimali watu, kuandaa vijana wenye ujuzi, nidhamu na ubunifu, wanaoweza kuyakabili mazingira ya ushindani wa kimataifa na ndiyo maana wanaipongeza TIA kwa kuwa na kampasi nane nchini, katika Mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya, Singida, Mwanza, Kigoma, Mtwara, Tanga na Zanzibar.
Alisema kuna umuhimu mkubwa wa kupambana na umaskini kupitia uwekezaji katika elimu, afya, maji, nishati, ulinzi wa jamii na uwezeshaji wa wanawake na vijana kiuchumi.
“Kwenye usimamizi na urahisishaji wa biashara tunahitaji kujua namna ya kupunguza urasimu, gharama za uzingatiaji wa sheria na taratibu na kuongeza ufanisi wa taasisi za udhibiti. Pili, uwekezaji na ushindani,” alisema.
“Tunahitaji tafiti zitakazobainisha namna ya kuvutia uwekezaji wenye tija, kuongeza mitaji katika sekta za uzalishaji na kuimarisha ushindani wa biashara za ndani.
“Tunahitaji teknolojia na ubunifu, tunahitaji kujua namna ya kutumia teknolojia, mifumo ya kidijitali na akili unde (Artificial Intelligence) kuongeza tija na kuboresha usimamizi wa biashara,” alisema.
Aidha, alisema serikali inahitaji kuona tafiti zitakazosaidia kuunganisha elimu na mafunzo na mahitaji ya soko la ajira, hususan kwa vijana na uzalishaji na masoko.
“ Tunahitaji kujua namna ya kuongeza thamani ya bidhaa, kuimarisha minyororo ya thamani na kupanua masoko ya ndani na nje ya nchi” alisema.
Alisema takwimu za Utafiti Jumuishi wa Nguvu Kazi wa mwaka 2025 zinaonesha kuwa kilimo kinaajiri asilimia 54.4 ya watu wote walioajiriwa nchini hali inayotoa ujumbe kuwa tunahitaji tafiti zitakazosaidia kuongeza tija ya kilimo, kuongeza thamani ya mazao na kuimarisha uhusiano kati ya kilimo, viwanda na masoko.
“Sekta binafsi ina mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi, uzalishaji na ajira. Kwa hiyo, hatuwezi kufikia malengo ya Dira ya 2050 bila kuwa na sekta binafsi yenye tija, yenye ushindani na inayofanya kazi katika mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji. Kwa msingi huo, Serikali inatambua sekta binafsi si mdau wa maendeleo pekee, bali ni mshirika muhimu wa Serikali katika kujenga Uchumi wa Taifa,” alisema.






