Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dodoma

Ndugu zangu Watanzania salamu. Leo ni Dominika. Nimetoka Kanisani hapa Kanisa Kuu la Paulo wa Msalaba, hasa baada ya Injili ya leo ya Mt 25:1-13 kuhusu wanawali kumi – werevu (wenye busara) watano na watano wapumbavu.

Hawa walichukua taa zao kwenda kumlaki Bwana Harusi. Werevu watano taa zao zilikuwa na mafuta, na wapumbavu watano taa zao hazikuwa na mafuta.

Sitanii, baada ya kumsubiri Bwana Harusi kwa muda mrefu taa zilizokuwa na mafuta kiduchu ziliishiwa. Wenye taa hizo wakafanya jaribio la kuwaomba wale ambao taa zao zilikuwa na mafuta. Hawa wenye busara, wakasema mafuta waliyonayo yanawatosha wao tu.

Msigano huo umenifumbua macho juu ya mnyukano wa kisheria katika hukumu aliyopewa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Baada ya hukumu kutolewa Novemba 6, 2026 siku hiyo nilikuwa na kazi pale jijini Dar es Salaam, lakini nikawa ninafuatilia na maandiko yaliyokuwa yanatumwa kutoka mahakamani. Baadaye niliambiwa ni timu ya CHADEMA iliyokuwa inatuma maandiko hayo kuufahamisha umma mwenendo wa hukumu siku hiyo. Andiko lililosomeka Part 499, aya ya kwanza ilisomeka hivi:

“Jaji Ndunguru anasema kwamba Mahakama inaamini kwamba mshtakiwa alikuwa na notice ya kosa dogo, hivyo alikuwa na nafasi ya kujitetea na ushahidi wote uliotolewa umejikita kwenye uchochezi na alichochea umma kuzuia uchaguzi wa 2025.”

Baada ya kusoma kauli hii nilifanya mahojiano na kusema: “Kama Lissu alipelekewa notisi ya kosa dogo na akakaa kimya bila kuijibu, basi ni wazi alijitia hatiani.”

Kilichofuata baada ya hapo ni historia. Mjadala umekuwa mkubwa na mpana. Ajenda imehama kutoka kwenye hukumu, kwenda kwenye aina ya adhabu. Nimefafanua mara kadhaa, lakini naona baadhi ya watu wanaendelea kuhoji kwa nini Lissu hakupigwa faini badala ya kifungo cha miaka minne? Hoja sasa si kutiwa hatiani, bali ni kwa nini hakupigwa faini badala yake akafungwa.

Ukirejea nia ya watunga sheria, adhabu anayopewa mtuhumiwa inakuwa na lengo la kumrekebisha. Nimetoa mfano sehemu. Mtu akikutwa na kosa la ulevi, ukampa adhabu ya kunywa bia kreti mbili, sidhani kama atapata nafasi ya kujutia. Nawaelewa wanaotaka faini badala ya kifungo, swali ni je, Lissu alikuwa na uwezo wa kulipa faini na asisikie majuto au la?

Sitanii, naandika makala hii nikiwa na masikitiko makubwa. Siasa au mijadala katika nchi yetu imehama kutoka kwenye masilahi kwenda kwenye matakwa. Watu hawataki kusikia kisichotimiza masilahi yao.

Ndiyo maana utakuta hata wengi nilioonyesha usahihi wa mahakama katika kutumia Kifungu cha 319 kuwa ni kwa mujibu wa sheria, badala ya kujibu hoja kwenye mitandao ya kijamii wanavurumisha matusi.

Kwa kuwa mjadala huu umeelekea kuwa mgumu, nimeona bora nichukue mitazamo inayokinzana, kutoka kwa walionitumia na makundi sogozi, niiweke pamoja hapa, kisha wewe msomaji upime kama Mahakama ilikuwa sahihi au la kwa mujibu wa sheria.

Wakati naweka mitazamo hii, narudia, Watanzania turejeshe utamaduni wa kujenga hoja badala ya matusi. Kesi ya Lissu imetugawa, ila sasa inabidi ituunganishe. Tukae meza moja kama Watanzania, kisha tuamue jinsi ya kusonga mbele. Maoni ni haya:

Daniel Mjema: This is totally misconception (hii si sahihi kabisa). Hakuna anayelilia faini. Hapa unatoka kabisa nje ya muktadha wa argument. Tunachosema ni kuwa mahakama ilijielekeza vibaya wakati inatamka adhabu. Imekwenda kinyume na Sentencing Guidelines za 2023 na imekwenda kinyume na misimamo ya kisheria (case law) kuhusiana na kutoa adhabu kwa aliyetiwa hatiani, kama kuna option ya adhabu ya fine, kifungo au vyote viwili.

Nchi hii inaongozwa kwa utawala wa sheria. Unless kama wewe sio muumini wa utawala wa sheria. Katika nchi inayoongozwa kwa utawala wa sheria, hakimu au Jaji hana uhuru wa kuchagua adhabu anayoipenda. Anapaswa kufuata mchakato uliowekwa na sheria, na kama hatofuata huo mchakato, adhabu yake ni batili hata kama kosa limethibitika.

Huyu nimemjibu kuwa hiyo inayoitwa ‘case law’ ni sehemu ya uhuru wa majaji kwenda kinyume cha sheria au miongozi iliyopo kwa kuangalia haki imesimama wapi. Ndiyo maana pengine kwa kubaini kuwa adhabu ya faini isingeleta urekebu katika fikra za mtuhumiwa, ikaamua kumpa adhabu itakayompa nafasi ya kujutia kosa alilotiwa nalo hatiani. Rejea mfano wa kreti mbili hapo juu!

Gabira Zona: *Kifungu cha 319(1):*

Iwapo mtu ameshtakiwa kwa kosa la jinai linalojumuisha vipengele kadhaa, ambapo muunganiko wa baadhi tu ya vipengele hivyo unaunda kosa jingine dogo ambalo linajitosheleza kisheria, na muunganiko huo wa vipengele umethibitishwa, lakini vipengele vilivyobaki havijathibitishwa, mtu huyo anaweza kutiwa hatiani kwa kosa hilo dogo, *licha ya kwamba hakuwa ameshtakiwa kwa kosa hilo.*

*Kifungu cha 319(2):*

Iwapo mtu ameshtakiwa kwa kosa la jinai na ushahidi ukathibitisha ukweli au mazingira ya tukio ambayo yanapunguza uzito wa kosa hilo na kulifanya kuwa kosa dogo zaidi, mtu huyo anaweza kutiwa hatiani kwa kosa hilo dogo, *licha ya kwamba hakuwa ameshtakiwa kwa kosa hilo.*

*Section 319(1):*

Where a person is charged with an offence consisting of several particulars, a combination of some only of which constitutes a complete minor offence, and such combination is proved but the remaining particulars are not proved, *he may be convicted of the minor offence although he was not charged with it.*

*Section 319(2):*

Where a person is charged with an offence and facts are proved which reduce it to a minor offence, he may be convicted of the minor *offence although he was not charged*

Amerejea vifungu hivyo kama vilivyoandikwa katika Kanuni ya Adhabu.

Msomaji mwingine: 1. Hukumu hii imedhihirisha Uhuru wa Mahakama Tanzania. Mahakama imekuwa chini ya mashinikizo ya kisiasa kutoka kwa Chadema na washirika wa Chadema dunia nzima, na pia mashinikizo ya kidiplomasia kutoka kwa Bunge la Ulaya, balozi mbalimbali na wanaharakati kuwa Lissu aachiwe huru.

Kama Mahakama isingekuwa huru, maana yake mtuhumiwa ama angefungwa kwa makosa ya uhaini aliyoshitakiwa nayo ama angeachiwa huru ili mashinikizo ya kisiasa na kidemokrasia yaonekane kushinda, lakini Mahakama imemhukumu Lissu kwa kosa lililotokana na mwenendo wa kesi ulivyokuwa. 

2. Hukumu ya uchochezi kwa Lissu haina mashaka kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani na ushahidi wa picha mjongeo (video) za mikutano aliyoifanya ambako alisema chama chake kitahakikisha kinakinukisha na uchaguzi huo hautafanyika. Kwa yaliyotokea mwaka jana – vifo na uharibifu mkubwa wa mali uliotokeza na ushahidi uliotolewa mahakamani na watu waliokiri kufanya vurugu baada ya kuchochewa na maneno ya Lissu, hukumu inaeleweka.

3. Maamuzi ya mahakama kumpa adhabu kwa kosa la uchochezi ambalo alikuwa hajashitakiwa nalo ni maamuzi halali ya kisheria. Kwenye kesi ya jinai ya Charles Ambrose dhidi ya Jamhuri na kesi ya DPP dhidi ya Lengai Ole Sabaya na wenzake Mahakama ilitoa maana ya maelezo kuwa;

*Ukishtakiwa kwa kosa fulani (kubwa* – kifungo kikubwa) ila ushahidi unathibitisha kosa dogo (kifungo kidogo), *basi Mahakama itakuhukumu kwa kosa dogo. LAKINI ili iwe hivyo, hilo kosa dogo lazima liwe damu moja/kizazi kimoja (genus/species) na lile kosa kubwa* ambalo ulishtakiwa. 

Mfano ulishtakiwa kwa (kupora) unyang’anyi wa kutumia silaha (Robbery – jela miaka 30+) lakini lengo halikutimia, unaweza hukumiwa kwa kosa dogo la kujaribu kupora (Attempted Robbery – jela miaka 7-20).

*Sio Mtu kashtakiwa kwa ubakaji* (Rape – jela miaka 30+), halafu ushahidi unaonesha kumbe hakubaka bali alikuwa anajaribu kupora (Attempted Robbery – jela miaka 7-20), *hawezi kuhukumiwa kwa kujaribu kupora kwasababu kosa la kubaka sio damu moja na kosa la kujaribu kupora, ni vitu viwili tofauti* hata kama kosa la kujaribu kupora ni dogo kwa kosa la ubakaji.

Kwa kesi ya Lissu kosa la uchochezi halina mashaka kuwa ni kosa dogo linalofanana na kosa kubwa la uhaini. Hivyo Mahakama iko sahihi kabisa kumhukumu kwa kosa dogo la uchochezi kama cognate offense ya Uhaini.

*Nchini Tanzania, Kifungu cha 319 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinahusu mazingira ambayo kosa lililothibitishwa linajumuishwa katika kosa la awali.     

*Utaratibu huu haupo nchini Tanzania pekee. Sheria za nchi za Kenya (Kifungu cha 179 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai) na Uingereza (Kifungu cha sita cha Sheria ya Makosa ya Jinai) kinatoa pia utaratibu wa mtu kuhukumiwa kwa kosa linalojumuishwa katika kosa la awali*

Mfano rahisi mwingine ni kwamba *Mtu anaweza kushitakiwa mahakamani kwa kosa la mauaji. Lakini baada ya majaji kusikiliza kesi, wanaweza kuamua kesi kuwa ya kuua bila kukusudia. Hakushitakiwa kwa kosa la kuua bila kukusudia, lakini mwenendo wa kesi umeonyesha hakukusudia kuua. 

Kwenye kesi ya Lissu, Mahakama imeona kwamba hakuna ushahidi wa kutosha kumhukumu kosa la uhaini, lakini kuna ushahidi kwamba maneno yake yalikuwa na uchochezi ambao kwa mujibu wa sheria zetu pia ni kosa*

4. Hukumu hii ni ushindi kwa pande zote; Kwa wafuasi wa Chadema, angalau kiongozi wao ameepuka hukumu ya kifo ambayo ingekuwa mbaya kwao. Upande wa mashitaka angalau umemkuta Lissu na hatia katika kosa lenye adhabu ya kifungo. Hii maana yake ni kwamba haikupoteza bure muda na rasilimali kwenye kesi hii.

Kwa Watanzania, adhabu hii ya kifungo cha miaka 4 kwa kosa la uchochezi haifungi milango ya kisheria kwa kukata rufaa, lakini pia haifungi milango ya busara za kisiasa – kama ambavyo ingekuwa kwenye kosa la uhaini. Haki imeshinda na Mahakama imeonyesha ukomavu.

Sitanii, hapa nimeweka machache kati ya mengi niliyoletewa. Swali moja kuu ni je, tunaitaka Tanzania ya ina gani? Ikiwa ajenda ya wanasiasa ni Katiba Mpya, kwani lazima tumwagiane matusi? Lakini kwa upande wa serikali, hivi mnajiona mko katika mkondo sahihi wa wapinzani kuendelea kuambiwa hawajui kusoma au kuandika? Mnajisikia vizuri kila mnapopata ushindi ukabezwa kuwa haukuwa ushidi halali?

Mdharau mwiba, mguu huota tende. Nafikiri hapa tulipofika, misingi ya taifa letu imetikiswa. Kila upande, kwa maana ya CHADEMA na upinzani kwa upande mmoja na CCM na serikali kwa upande mwingine, ebu tuionyeshe dunia kuwa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume walituwekea misingi ya utu,  kuthaminiana na kuwa tayari kuzungumza kama njia ya kumaliza matatizo yetu.

Sitanii, natamani Tanzania ambayo uchaguzi ukiitishwa iwe kama Marekani. Bila kujali nani yupo madarakani akishinda jimbo au kata anakabidhiwa kiti. Tumeshuhudia uchaguzi wa mwaka huu nchini Marekani Chama cha Republican kimepoteza Bunge na Seneti.

Kinakwenda kujipanga. Democrat mbao walikuwa wanatulazimisha ushoga, hii sera yao haikukubalika wakaondolewa madarakani, lakini nao Republican sera ya vita dhidi ya Iran imekataliwa Democrat wakarejeshwa madarakani.

Natamani nchi yetu ifike huko. Tubadilishane madaraka kwa sera, si matusi. Nia na lengo ni Watanzania wapate nafuu. Chama chochote kiseme kikiingia madarakani kitafanya nini, badala ya kumwaga matusi kwa viongozi, watoto wao na wenza wao.

Nchi haitajengwa kwa matusi. Najua kwa kuandika hivi mpo mtakaonishushia matusi kama mlivyofanya tangu juzi, karibuni. Mungu ibariki Tanzania.

0784 404827