Na Deodatus Balile, JamhuriMedia, Dodoma
UZINDUZI wa majengo ya wizara na taasisi za Serikali pamoja na barabara za lami katika Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma, umeongeza ukurasa mwingine katika historia ya utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati nchini Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Sitanii, tukio hilo la Oktoba 30, 2026, halikuwa uzinduzi wa kawaida wa majengo na barabara, bali lilikuwa ishara ya mwendelezo wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuhakikisha miradi mikubwa iliyoanzishwa katika awamu zilizotangulia inakamilishwa na kuanza kutoa manufaa yaliyokusudiwa kwa wananchi.
Katika hafla hiyo, Rais Samia aliambatana na Rais wa Angola, João Manuel Gonçalves Lourenço, ambapo viongozi hao walikata utepe kuashiria ufunguzi wa majengo ya ofisi za wizara na taasisi za Serikali pamoja na mtandao wa barabara za Mji wa Serikali Mtumba.
Kwa kuangalia mwenendo wa miradi mikubwa nchini, uzinduzi wa Mtumba unatoa picha ya mtindo wa uongozi unaosisitiza mwendelezo wa mipango ya maendeleo, badala ya kuiacha miradi iliyobuniwa au kuanzishwa na watangulizi na kuanzisha mipya. Hapa falsafa ya Kazi Iendelee inathibitika.
Rais Samia amesimamia kukamilika kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere unaozalisha megawati 2,115 na kuifanya Tanzania kuwa na umeme mwingi kuliko nchi yoyote ya Afrika Mashariki na Kati, Daraja la Kigongo–Busisi lililopewa jina la Hayati Rais John Pombe Magufuli, ambalo nalo ni refu kuliko yote Afrika Mashariki.
Sitanii, amekamilisha kipande cha reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma. Reli hii inatumia umeme, na ni ya kwanza pia katika Afrika Mashariki kwani jirani pekee aliyejaribu kujenga SGR ni Kenya ambayo yao inatumia dizeli badala ya umeme. Sasa Mji wa Serikali Mtumba umeingia katika orodha hiyo ya mafanikio ya miundombinu.
Miradi hii ina tofauti za matumizi na ukubwa wa uwekezaji, lakini inaunganika katika jambo moja muhimu: kujenga misingi ya uchumi wa kisasa kupitia upatikanaji wa nishati, usafiri, mawasiliano na mazingira bora ya utendaji wa Serikali.

Mtumba yatimiza maono ya muda mrefu
Historia ya kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya Tanzania inaanzia katika maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ambaye alitaka shughuli za Serikali zihamishiwe katikati ya nchi ili kusogeza utawala uwe karibu zaidi na wananchi.
Uamuzi wa kuhamia Dodoma ulipitishwa mwaka 1973 kupitia Azimio la Halmashauri ya Taifa ya TANU. Sababu kuu ilielezwa kuwa ni kuweka makao makuu katikati ya nchi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wa mikoa mbalimbali.
Sitanii, wazo hili lilianza pia kujadiliwa rasmi bungeni kupitia hoja binafsi iliyowasilishwa na mbunge wa taifa Joseph Nyerere mwaka 1966. Joseph Kizurira Nyerere alikuwa mdogo wake wa kuzaliwa Mwalimu Julius Nyerere. Alizaliwa mwaka 1934 na alifariki mwaka 1994 akiwa na umri wa miaka 60.
Kwa miaka mingi, azma hiyo ilitekelezwa kwa mwendo mdogo, huku sehemu kubwa ya shughuli za Serikali ikiendelea kufanyika Dar es Salaam.
Mwaka 2016, Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ilichukua hatua ya kuharakisha uhamaji wa shughuli za Serikali kwenda Dodoma. Ujenzi wa awamu ya kwanza ya majengo ya Mji wa Serikali Mtumba ulianza mwaka 2018 na kukamilika mwaka 2019. Baadhi ya wizara zilihamia kwenye ofisi zilizojengwa kwa mabati.
Serikali ya Awamu ya Sita ilipoingia madarakani mwaka 2021, iliendeleza mradi huo kwa kuanza ujenzi wa majengo ya kudumu, barabara na miundombinu mingine muhimu.
Sitanii, kwa mujibu wa taarifa za Serikali, uwekezaji katika Mji wa Serikali Mtumba umefikia takribani Sh bilioni 700, fedha zilizotokana na makusanyo ya ndani. Si mkopo.
Kukamilika kwa sehemu kuu za mradi huu kunamaanisha kwamba maono yaliyoanzishwa miongo kadhaa iliyopita sasa yamepiga hatua kubwa na kuwa uhalisia. Serikali imeonesha kuwa mabadiliko ya uongozi hayapaswi kuwa sababu ya kusimamisha mipango yenye manufaa ya muda mrefu kwa taifa.
Barabara za Mtumba zafungua ukurasa mpya
Moja ya mafanikio yanayoonekana wazi katika Mji wa Serikali Mtumba ni ujenzi wa mtandao wa barabara za lami wenye urefu wa kilomita 59.1, uliotekelezwa kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Akitoa taarifa ya mradi wakati wa uzinduzi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Profesa Riziki Shemdoe, alisema miundombinu hiyo inajumuisha vituo 52 vya mabasi, taa 1,635 za barabarani, njia za watembea kwa miguu na waendesha baiskeli, pamoja na mabwawa matatu ya kudhibiti mafuriko.
Sitanii, ujenzi huo unaonesha mwelekeo wa kujenga miji inayozingatia mahitaji ya watumiaji mbalimbali wa barabara badala ya magari pekee. Kwa mtazamo wa kiuchumi, barabara hizi zinatarajiwa kuongeza thamani ya maeneo yanayozunguka Mtumba, kuvutia uwekezaji katika makazi, hoteli, biashara na huduma nyingine zinazohitajika na watumishi pamoja na wananchi wanaofika katika ofisi za Serikali.
Hata hivyo, manufaa hayo yatategemea pia ubora wa mipango miji, usimamizi wa matumizi ya ardhi na upatikanaji wa huduma za msingi. Jambo moja linaloonekana kuwa tishio ni kwamba maeneo yanayozunguka Mji wa Serikali yameanza kujengwa kiholela kwa kiwango kinachotishia mpangilio wa mji wa Dodoma, nje ya Mji wa Serikali Mtumba.

Samia ataka mabadiliko ya utendaji
Katika hotuba yake, Rais Samia alionesha kwamba thamani ya majengo ya kisasa haipimwi kwa uzuri wake pekee, bali kwa uwezo wake wa kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Sitanii, Rais amesisitiza matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), akitaka mifumo ya taasisi za Serikali iweze kuwasiliana ili wananchi wasilazimike kupeleka taarifa zilezile katika ofisi tofauti.
“Mwananchi hatakiwi kupeleka taarifa ileile aliyopeleka katika moja ya ofisi za Serikali,” alisema Rais Samia, akisisitiza umuhimu wa mifumo ya Serikali kusomana.
Kauli hiyo ina maana kwamba mafanikio ya Mtumba hayataishia kwenye kukamilika kwa majengo, bali yatapaswa kupimwa kwa kupungua kwa urasimu, gharama na muda unaotumiwa na wananchi kupata huduma.
Rais Samia pia aliagiza kutunzwa kwa miundombinu na maeneo ya kijani, kuheshimiwa kwa Mpango Mkuu wa Dodoma wa mwaka 2019–2039 na kuimarishwa kwa huduma za maji, umeme na barabara. Pia, alitaka ushirikiano na sekta binafsi uongezwe ili kuchochea uwekezaji na maendeleo ya jiji hilo.
Bwawa la Nyerere, ushahidi wa mwendelezo
Sitanii, mradi mwingine unaoonesha mwendelezo huo ni Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere katika Mto Rufiji, lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.
Mradi huu ulioanza chini ya Serikali ya Awamu ya Tano uliendelezwa na Serikali ya Rais Samia, ambapo mitambo yake iliingizwa katika mfumo wa gridi ya taifa kwa hatua hadi kukamilika kwa mradi na kuzinduliwa rasmi Agosti 2026.
Umuhimu wake hauishii kwenye kuongeza uwezo wa uzalishaji wa umeme. Unahusisha pia kujenga msingi wa upatikanaji wa nishati kwa viwanda, biashara, huduma na uwekezaji.
Kwa uchumi unaolenga kuongeza uzalishaji wa bidhaa na ajira, umeme wa uhakika ni hitaji la msingi. Hivyo, kukamilika kwa mradi huu kunaonesha namna uwekezaji wa muda mrefu unavyoweza kuendelezwa licha ya mabadiliko ya uongozi.
Daraja la Magufuli launganisha uchumi
Mfano mwingine ni Daraja la Kigongo–Busisi katika Ziwa Victoria, linalojulikana kama Daraja la J.P. Magufuli. Wakati Rais Samia anaingia madarakani mwaka 2021, ujenzi wa daraja hilo ulikuwa umefikia takribani asilimia 25. Serikali yake iliendelea kugharamia utekelezaji wake hadi kukamilika mwaka 2025.
Sitanii, kwa mujibu wa TANROADS, Serikali ya Awamu ya Sita ililipa takribani Sh bilioni 539.28 kwa ajili ya ukamilishaji wa mradi huo. Daraja hilo limeondoa utegemezi wa vivuko katika eneo hilo na kuboresha muunganiko wa barabara kati ya maeneo ya Kigongo, Busisi na mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Katika uchambuzi wa maendeleo, daraja hilo lina umuhimu mkubwa kwa kuwa linapunguza vikwazo vya usafirishaji na kuwezesha shughuli za biashara kufanyika kwa urahisi zaidi na kwa saa 24. Uamuzi wa kuendeleza mradi uliobuniwa na mtangulizi wake pia unaonesha umuhimu wa kutenganisha miradi ya kitaifa na ushindani wa kisiasa.

SGR Dar–Dodoma nayo yakamilika
Reli ya kisasa ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ni mfano mwingine wa mwendelezo wa miradi ya kimkakati aliyoijenga Rais Samia. Agosti Mosi, 2024, Rais Samia alizindua rasmi huduma za treni za abiria na miundombinu ya reli hiyo hadi Dodoma, hatua iliyowezesha wananchi kutumia usafiri wa kisasa unaopunguza muda wa safari.
Katika hotuba yake ya uzinduzi, Rais Samia alikumbusha kwamba maendeleo ni mchakato wa hatua kwa hatua, akieleza mchango wa awamu mbalimbali za uongozi katika kufanikisha mradi huo.
Alitaja hatua za awali zilizochukuliwa wakati wa Rais Benjamin Mkapa, upembuzi yakinifu chini ya Rais Jakaya Kikwete na kuanza kwa ujenzi wakati wa Rais Magufuli, kabla ya Serikali ya Awamu ya Sita kuendeleza na kukamilisha sehemu ya Dar es Salaam–Dodoma.
Sitanii, uchambuzi wa miradi hii minne unaonesha kuwa maendeleo ya taifa yanahitaji zaidi ya maamuzi ya kuanzisha miradi. Yanahitaji pia nidhamu ya utekelezaji, fedha, usimamizi na dhamira ya kuikamilisha. Miradi hii imethibitisha kuwa Tanzania inaweza na Rais Samia amethibitisha nidhamu kubwa ya matumizi ya fedha za walipakodi.

Mtumba iwe kipimo cha tija
Pamoja na mafanikio ya miundombinu, changamoto inayofuata ni kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha thamani inayolingana na fedha zilizotumika. Majengo ya Mtumba yanapaswa kupunguza gharama za uendeshaji wa Serikali, kuimarisha uratibu kati ya wizara na kuongeza kasi ya utoaji wa huduma.
0784 404827

