Na Prosper Makene

GENEVA, Uswisi, Novemba 3, 2026– Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Balozi Dkt. Hoyce Temu, amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bi. Shahad Matar.

Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) hapa Geneva, katika kuendelea kukuza uhusiano mzuri l kati ya Tanzania na UAE.

Mabalozi hao wawili wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana na kusaidiana ndani ya mashirika mbalimbali ya kimataifa yaliyoko Geneva.

Ajenda nyingine muhimu ilikuwa ni maandalizi ya Mapitio ya Hali ya Haki za Binadamu (Universal Periodic Review – UPR). Balozi Dkt. Temu alimjulisha mwenyeji wake kuhusu maandalizi ya Tanzania na juhudi za kitaifa zinazoendelea katika kukuza na kulinda haki za binadamu. UPR ni utaratibu wa kipekee wa Baraza la Haki za Binadamu ambapo rekodi ya haki za binadamu ya kila Nchi Mwanachama wa Umoja wa Mataifa hupitiwa kila baada ya miaka minne na nusu.

Bi. Matar amethibitisha dhamira ya UAE ya kuendelea kushirikiana kwa njia ya kujenga na kueleza uungaji mkono wa nchi yake kwa Tanzania wakati wa mapitio hayo yajayo.

Wanadiplomasia hao pia walijadili ushirikiano katika eneo la maji na maendeleo endelevu. Walibadilishana mawazo kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Maji wa mwaka 2026, unaoandaliwa na Umoja wa Falme za Kiarabu na unatarajiwa kufanyika jijini Abu Dhabi mapema Desemba 2026.

Balozi Temu ameipongeza UAE kwa uongozi wake katika kuandaa mkutano huo muhimu wa kimataifa na kuthibitisha kuwa Tanzania itashiriki Mkutano huo.

Alibainisha kuwa masuala ya maji safi na usafi wa mazingira yanaendelea kuwa kipaumbele kikuu kwa Tanzania wakati nchi inapoongeza kasi ya utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo ya taifa.

Mkutano wa 2026 ni muendelezo wa Mikutano wa kihistoria wa Maji
unalenga kuharakisha utekelezaji wa Lengo Nambari 6 la Maendeleo Endelevu (SDG 6) kuhusu maji safi na usafi wa mazingira kwa wote, pamoja na malengo mengine yanayohusiana na maji. Tanzania, ikiwa na rasilimali kubwa za maji baridi Katika nchi za Maziwa Makuu Afrika, ina maslahi makubwa katika usimamizi endelevu wa rasilimali za maji duniani.

Kwa ujumla, mkutano huo umethibitisha tena dhamira ya pamoja ya Tanzania na UAE katika kudumisha mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, mshikamano wa kimataifa na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu.