Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MFUKO wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umefanikiwa kujenga minara 2,199 kati ya minara 2,324 iliyopangwa kujengwa katika awamu mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini na mijini yenye changamoto ya mawasiliano.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwenye kikao kazi kilichoratibiwa na ofisi ya Msajili wa Hazina leo Novemba 3, 2026, Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa UCSAF, Albert Richard, wakati akielezea utekelezaji wa miradi ya UCSAF kuwa miradi hiyo imehusisha mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku kata 2,053 kati ya 2,306 zilizolengwa zikiwa tayari zimefikiwa na huduma za mawasiliano.

Amesema katika mradi wa ujenzi wa minara 758, UCSAF imeeleza kuwa minara yote imekamilika na kuwashwa, ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa Sh bilioni 126 uliolenga kuboresha huduma za mawasiliano kwa wananchi wapatao milioni 8.5 katika kata 713 na vijiji 1,401.

Mkurugenzi huyo amesema mradi huo umetekelezwa kwa kushirikiana na kampuni za simu zikiwemo Airtel, Viettel, Yas, TTCL na Vodacom.

Richard amesema Serikali kupitia UCSAF inaendelea kutekeleza mradi wa awamu ya 10 unaohusisha ujenzi wa minara 287 katika kata 287, ambapo hadi wakati wa kutolewa kwa taarifa hiyo minara 65 ilikuwa imewashwa, sawa na asilimia 23 ya utekelezaji.

“Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 29 ulizinduliwa Desemba 5, 2025 na unatarajiwa kutekelezwa ndani ya miezi 15.

Katika sekta ya utangazaji, UCSAF pia imefadhili ujenzi wa vituo 11 vya kurushia matangazo ya Redio ya Taifa (TBC), ambavyo vimekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 2.5, huku vituo vingine 26 vikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji” amesema.

Ameongeza kuwa kwa upande wa TEHAMA, shule za umma 1,167 zimenufaika na mradi wa kupeleka vifaa vya TEHAMA na ujenzi wa maabara, ambapo Serikali imewekeza Sh bilioni 17.7 hadi Oktoba 2026.

Vilevile, mfuko huo umefanikisha kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule 22 zinazotoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, hatua inayolenga kuongeza usawa na ujumuishi katika upatikanaji wa elimu ya kidijitali.

UCSAF imeeleza kuwa itaendelea kutekeleza miradi ya mawasiliano kwa kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wananchi wa maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara wanapata huduma za mawasiliano na kuchochea uchumi wa kidijitali.

Aidha, UCSAF imeendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za posta nchini kupitia Shirika la Posta Tanzania kwa kutoa vifaa vya kisasa vinavyorahisisha utoaji wa huduma. Vifaa vilivyotolewa katika mwaka wa fedha 2024/25 ni pamoja na vifaa 50 vya Personal Assistance Devices (PDA), kompyuta 30, kompyuta mpakato saba, vifaa vya umeme vya UPS 30 na mashine tano kubwa za kunakili nyaraka.

Amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, mfuko huo ulipanga kuendelea kuimarisha huduma hizo kwa kutoa vifaa vingine, vikiwemo PDA 50, printa tano za matumizi ya viwandani, kompyuta za mezani saba, kompyuta mpakato saba, UPS tano na mashine nne za kunakili nyaraka.

“Kwa upande wa huduma za intaneti, UCSAF imeanzisha vituo vya intaneti vya bure katika maeneo mbalimbali yenye mikusanyiko ya wananchi, yakiwemo Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Nyerere Square jijini Dodoma, Soko la Nyamagana mkoani Mwanza na Soko la Tabora. Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wananchi kupata huduma za kidijitali kwa urahisi zaidi” amesema Richard.

Vilevile, UCSAF inaendelea na mpango wa kuunganisha ofisi za halmashauri na mkongo wa mawasiliano wa nyuzi za optiki (faiba) ili kuboresha upatikanaji wa intaneti ya uhakika katika utoaji wa huduma za umma. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, maeneo 10 yamefanyiwa utambuzi na mchakato wa manunuzi unaendelea ili kumpata mkandarasi wa kutekeleza mradi huo.

Katika kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu, mfuko huo pia umegharamia mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 5,094 wa shule za msingi na sekondari za umma Tanzania Bara na Zanzibar tangu mwaka wa fedha 2016/17. Kwa mwaka wa fedha 2026/27, walimu wengine 692 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo, wakiwemo walimu 100 wenye mahitaji maalumu.

Hatua hizo ni sehemu ya jitihada za UCSAF za kupunguza pengo la kidijitali na kupanua fursa za wananchi kutumia teknolojia katika elimu, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi. Mfuko huo unaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wa sekta ya mawasiliano kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi katika maeneo ambayo hayana mvuto mkubwa wa kibiashara.