Na Mwamvua Mwinyi, JmahuriMedia, Bagamoyo
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga, kuhakikisha zinaundwa kamati za usuluhishi na utatuzi wa migogoro baina ya wakulima na wafugaji ili kuimarisha mahusiano na kudumisha amani.
Nyongo alitoa agizo hilo Novemba 2, 2026, katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Fukayosi, ulioitishwa kufuatia migogoro baina ya wakulima na wafugaji wa jamii ya Wamang’ati.
Amesema kamati hizo zitakuwa na jukumu la kusikiliza pande zote, kusuluhisha migogoro na kutafuta ufumbuzi wa kudumu, huku akiwataka wafugaji kuacha kuingiza mifugo kwenye mashamba ya wakulima na kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa shughuli zao.
Aidha, amewataka wakulima kuacha kujichukulia sheria mkononi kwa kuwadhuru wafugaji au mifugo yao, akisisitiza kuwa hakuna mtu au kundi linaloweza kuinunua Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan wala kuwa juu ya sheria.
“Naomba niwashukuru kwa taarifa mlizonipatia, Nitazifuatilia moja baada ya nyingine, na nikibaini kuna kiongozi yeyote anayehusika na vitendo hivyo, nitamshughulikia ipasavyo, Ninachotaka ni wananchi waishi kwa amani,” alisema Nyongo.
Katika hatua nyingine, amemtaka Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani kuwachukulia hatua askari wanaokiuka maadili, huku akielekeza kuimarishwa kwa Kituo cha Polisi Kiwangwa kwa kuongeza askari wa doria.
Pia, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi na kufuatilia kesi mahakamani kwa kutoa ushahidi wanapohitajika ili haki itendeke.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, alisema ushirikiano wa wananchi ni muhimu katika uchunguzi na uendeshaji wa kesi, akibainisha kuwa baadhi yao wamekuwa wakisita kutoa ushahidi wanapohitajika.






