Na Mwandishi Maalumu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

TAASISI ya Saratani Ocean Road (ORCI) imesogeza huduma za uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti kwa washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake wa Jukwaa la Mabunge la Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) huku ikitumia fursa hiyo kutoa elimu na kutangaza huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi hiyo.

Mkutano huo wa siku nne umefunguliwa leo katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ambapo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkutano huo muhimu pamoja na ajenda nyingine ni kielelezo cha jitihada zinazofanywa katika kuwawezesha wanawake na kutambua nafasi yao muhimu katika kuimarisha uongozi, kudumisha amani na kuchochea maendeleo endelevu pamoja na kuendeleza misingi ya mshikamano, usawa na ushirikiano wa Kiafrika ambayo imekuwa sehemu muhimu ya historia ya Bara la Afrika.

Akizungumza kuhusu huduma za uchunguzi zinazotolewa katika mkutano huo Daktari Bingwa Mbobezi wa Radiolojia Anganile Kalinga, alisema saratani ya mlango wa kizazi na saratani ya matiti zimekuwa zikiathiri wanawake wengi hivyo basi Taasisi imeona umuhimu wa kutumia fursa ya mkutano huo unaowakutanisha wabunge wanawake kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa awali kwa washiriki.

“Katika mkutano huu tumejipanga kutoa elimu na kufanya upimaji wa awali wa saratani. Washiriki ambao tutawabaini kuwa na changamoto za kiafya tutawapa rufaa ya kwenda Ocean Road kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi,” alisema Dkt. Anganile.

Alisema saratani ya mlango wa kizazi ni miongoni mwa saratani zinazowasumbua wanawake wengi ikifuatiwa na saratani ya matiti hivyo aliwahimiza wanawake kutenga muda wa kuchunguza afya zao ili kubaini changamoto za kiafya mapema na kupata matibabu stahiki, huku akisisitiza kuwa saratani inatibika inapobainika na kutibiwa kwa wakati.

Dkt. Anganile aliongeza kuwa ushiriki wa wabunge kutoka nchi mbalimbali katika mkutano huo ni fursa muhimu kwa ORCI kutangaza huduma zake huku akieleza kuwa wabunge hao wanaweza kusaidia kufikisha taarifa za huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo kwa wananchi katika nchi zao.

“Wabunge ni watunga sera. Kufahamu huduma zinazotolewa na ORCI kutasaidia kuongeza uelewa kuhusu huduma hizo na kufungua fursa kwa ORCI kuwafikia wagonjwa wanaohitaji matibabu ya saratani katika nchi zao, kwani Serikali imewekeza vya kutosha katika sekta ya afya ikiwemo kusomesha wataalamu na kununua vifaa tiba vya kisasa,” alisema Dkt. Anganile.

Kwa upande wao washiriki wa mkutano huo waliofika katika banda la Taasisi hiyo walipongeza huduma zinazotolewa na ORCI huku wakieleza kufurahishwa na fursa ya kupata elimu na huduma za uchunguzi katika mkutano huo.

Miongoni mwa washiriki hao ni Maria John ambaye alipongeza huduma zinazotolewa na ORCI katika mkutano huo na kusema kuwa naye atatumia fursa hiyo kwenda kufanya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi na matiti ili kufahamu hali ya afya yake.

Mshiriki mwingine ni Dkt. Julius Masishanga kutoka Hospitali ya Lugalo ambaye ni mtaalamu mbobezi wa magonjwa ya ini alieleza kufurahishwa na huduma zinazotolewa na ORCI na kusema kuwa anatamani kushirikiana na Taasisi hiyo katika juhudi za kupambana na maambukizi ya homa ya ini.

Ushiriki wa ORCI katika mkutano huo ni sehemu ya juhudi za Taasisi hiyo za kuendelea kutoa elimu kuhusu saratani, kuhamasisha jamii kufanya uchunguzi wa afya mapema na kutangaza huduma zake kwa wadau wa ndani na nje ya nchi.

 nchi.

1000514429
1000514432