Na Dennis Luambano, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Safari ya kujenga jamii yenye maendeleo endelevu haipaswi kuliacha kundi fulani nyuma hata kama la wanawake wenye ulemavu licha ya kwamba wanakabiliwa na vikwazo vinavyowazuia kutumia uwezo wao katika shughuli za kiuchumi na uongozi.

Pamoja na kujaaliwa vipaji, maarifa na uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa, wanawake wenye ulemavu wengi wao wanakumbana na ubaguzi, unyanyapaa, ukosefu wa fursa na mazingira yasiyowezesha ushiriki wao.

Hali hiyo inaibua mjadala muhimu kuhusu nafasi yao katika maendeleo na wajibu wa serikali, sekta binafsi na jamii kuhakikisha wanapata fursa sawa, kufanya uamuzi na kunufaika na matunda ya maendeleo.

Kukabiliana na vikwazo hivyo huku tukiangazia Mkutano wa Wabunge Wanawake wa Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu unaoanza Novemba 2 hadi 5, 2026 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Bajeti Kuu ya Mwaka wa Fedha wa 2026/2027, imeziagiza mamlaka za Serikali za Mitaa kutenga asilimia 15 ya mapato ya ndani badala ya asilimia 10 ya awali kwa ajili ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Kupitia mikopo hiyo, inaonyesha dhahiri kwamba kuna umuhimu wa wanawake wenye ulemavu ndani ya jamii na wataendelea kushirikishwa katika shughuli za maendeleo.

Kuthibitisha hilo, Machi 2, 2026, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, anasema serikali itaendelea kuimarisha mifumo ya kisheria, kisera na kijamii ili kuhakikisha kuna usawa wa kijinsia, ulinzi wa watoto na ujumuishwaji wa watu wenye ulemavu katika maendeleo ya taifa.

Anasema Tanzania haiwezi kufikia maendeleo endelevu endapo makundi maalumu yataendelea kutengwa.

Kutokana na hali hiyo, anasema serikali inatekeleza mipango mbalimbali ya kitaifa ukiwamo Mpango wa Pili wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na upanuzi wa vituo vya huduma jumuishi kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.

Waeleza hali halisi

Novemba Mosi, 2026 kwa nyakati tofauti, wadau wengine wameeleza hali halisi ya wanawake wenye ulemavu na umuhimu wa ushirikishwaji katika maendeleo baada ya kuulizwa katika mahojiano maalumu na mwandishi wa makala hii.

Wakili wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), William Maduhu, anaishauri serikali kuhakikisha wanawake wenye ulemavu wanashiriki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo.

Kwa sasa anasema juhudi zilizofanywa na serikali ni mabadiliko ya fedha kwenye mamlaka ya serikali za mitaa kwa kuweka mikopo ya asilimia 10 katika halmashauri.


“Yaani 4:4:2 kwa maana asilimia nne kwa vijana, asilimia nne kwa wanawake na asilimia mbili kwa walemavu. Wanawake tena wenye ulemavu ni changamoto. Wanawake walemavu wana faida mbili, wanaweza kuchukua mkopo wa ile asilimia nne kwa upande wa wanawake pia anaweza kuchukua asilimia mbili ya walemavu ili washiriki katika shughuli za maendeleo,” anasema.

Licha ya kuwapo mikopo hiyo, anasema bado kuna vikwazo vinavyowakwamisha wanawake wenye ulemavu kuifikia.

Anakitaja kikwazo kimojawapo ni mazingira akitolea mfano kwa mwanamke mwenye ulemavu wa miguu anashindwa kufikia fursa kwa wakati kwa sababu ya ukosefu wa vifaa.

“Pili ni changamoto ya kijamii kwa maana ubaguzi. Unakuta familia haitaki kumtambulisha mwanamke mlemavu katika fursa zinazopatikana nje katika jamii na muda wote wanamfungia ndani kwa sababu wanaamini huyo ni mtu wa kusaidiwa tu kwa sababu ya changamoto zake.

“Nyingine ya kielimu kwa sababu serikali lazima iwekeze katika elimu kwa makundi haya ili wenyewe wajue kwamba wana mchango wa kuchangia shughuli za ukuzaji uchumi na maendeleo ya nchi,” anasema.

Pia anasema wanawake wenye ulemavu ni kundi lenye haki ya kuchangia ujenzi wa taifa lao na serikali iwekeze zaidi katika mifumo ya ujumuishwaji ndani ya jamii ili kila mmoja afaidike na fursa zinazopatikana.

Meneja wa Kituo cha Huduma kwa Watu Wenye Ulemavu (CDS) cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Joyce Mkongo, anasema ushirikishwaji wa wanawake wenye ulemavu katika shughuli za maendeleo upo japo kwa kiwango kidogo.


“Kitu cha muhimu ni kuwabaini wanawake wenye ulemavu na kuwapa hizo fursa za kushiriki katika shughuli za maendeleo.
“Endapo kunatokea nafasi ya kushindanishwa na vigezo wanavyo basi wanawake wenye ulemavu wazingatiwe kwa kupewa kipaumbele cha kwanza,” anasema.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Mkoa wa Dodoma, Omary Lubuva, anasema kwa sasa wameanza kuona suala la wanawake wenye ulemavu kushirikishwa katika shughuli za maendeleo likifanyiwa kazi.

“Tunapozungumzia wanawake maana yake wote na tusiwaache nyuma wenye ulemavu. Kama tunazungumzia ushirikishwaji wa wanawake katika sekta mbalimbali basi tuzungumzie wote wakiwamo wenye ulemavu.

“Kwa sababu kama fursa nyingine zitafunguka na masuala yao yatasikika kwa wao kupata elimu na kujengewa uwezo katika nyanja mbalimbali ikiwamo za uongozi, naamini watakuwa sawa na uwezo wa wanawake wengine licha ya ulemavu wao kwa sababu kama tunavyosema siku zote kwamba ulemavu si kushindwa,” anasema.

Kitu kingine anachokishauri ni wanawake wenye ulemavu kujengewa uwezo wao kutokana na mazingira ya jamii zetu.

“Ndani ya jamii zetu bado wanawake wenye ulemavu hali zao si nzuri hasa kwa upande wa elimu na wao wenyewe wanatakiwa kujitokeza maeneo mbalimbali ikiwamo kugombea uongozi na kuchangamkia fursa za maendeleo.

“Jamii itakapotambua na kuwajengea uwezo, kuwapa nafasi na kuwapa fursa wataweza sawa na wanawake wengine,” anasema.

Anatoa wito wake kwa wenye nafasi kwamba kundi la wanawake wenye ulemavu haliachwi nyuma kwa sababu wana nafasi kubwa ya kuchangia maendeleo pale fursa zitakapopatikana, mazingira yatakapokuwa jumuishi na kujengewa uwezo.

Mkurugenzi wa Shirika la Kuhudumia Watu Wenye Ulemavu Tanzania (FDH), Michael Salali, anasema wanapambana kuhakikisha wanawake wenye ulemavu wanapata ushiriki sawa wa shughuli za maendeleo.

“Tukumbuke wanawake wenye ulemavu wanapata changamoto mara mbili zaidi kuliko wale wasio na ulemavu. Miongoni mwa changamoto hizo ni ubaguzi katika jamii na kukosa fursa sawa na wengine.

“Kwa hiyo uwiano wa ushiriki katika shughuli za maendeleo hauendi pamoja. Ni uwiano uliochanganyika na wenye vikwazo vingi vya kiuchumi. Wanawake wenye walemavu wanapitia changamoto zinazoanzia katika ngazi ya familia na kwenda katika jamii na mifumo ya uamuzi,” anasema.

Kama taasisi, anasema wanapambana kuhakikisha ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika nyanja mbalimbali na kazi hiyo wanaifanya kwa kushauri kuwe na sera jumuishi kwa makundi yote.

“Tunatengeneza ushiriki sawa katika jamii pia tujiulize sera za taasisi zetu zinashirikishaje wanawake wenye ulemavu? Tutahakikisha tunavunja vikwazo vya unyanyapaa ili wanawake wenye ulemavu washiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi,” anasema.

Mtaalamu wa Teknolojia Saidizi kwa Watu Wenye Ulemavu wa CDS, Mashukura Kabwogi, anasema suala la kushiriki katika maendeleo inategemea mwanamke mwenye ulemavu yuko katika jamii ipi inayomzunguka na jinsi inavyomchukulia?

“Kuna jamii inakuona haufai ila nyingine inakuona una umuhimu. Kwa ujumla angalau sasa hivi jamii kubwa inaelewa na kwa kiasi inawashirikisha na unakuta kuna baadhi ya wanawake wasioona wapo vikundi vya vikoba.

“Ajira serikalini hawaangalia ulemavu wa mtu bali uwezo wake binafsi na unaajiriwa ndiyo maana kuna wanawake wengi wenye ulemavu wameajiriwa sehemu mbalimbali na katika kada tofauti hata bungeni tuna wanawake wenye ulemavu,” anasema.

Nini kifanyike? Kwanza, anasema wao wenyewe wanawake wenye ulemavu wana kazi kubwa kuhakikisha jamii inaelewa kwamba wanaweza kushiriki kama wengine.

“Tuwe na uthubutu wa kujaribu kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo. Mwanzoni itakuwa ngumu na jamii itaona huyu naye vipi lakini ikishaona mchango wako inaelewa na inakupokea moja kwa moja,” anasema na kuongeza:

“Jamii yetu wakati mwingine inapaswa kuelimishwa kwa kuona kwamba kumbe huyu anaweza? Pia wapo wachache wanaamini moja kwa moja kwamba wanawake wenye ulemavu wanaweza na hao wana kazi kubwa ya kuielimisha jamii kwamba tunaweza.

“Ikitokea basi moja kwa moja kusema inawezekana kwamba mbona tumewahi kufanya hiki na mwanamke mwenye ulemavu na kupitia wao itasaidia jamii kuelewa haraka kwamba inawezekana.”