Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) imesajili miradi 1,148 ya uwekezaji yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 15.32, inayotarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 344,031.

Akizungumza leo Novemba 2, 2026 katika kikao kazi kati ya mamlaka hiyo, wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri amesema kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Septemba 2026, mamlaka hiyo imeendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi, kuboresha huduma kwa wawekezaji na kuendeleza Maeneo Maalum ya Kiuchumi (SEZs).

TISEZA ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Na. 6 ya mwaka 2025, kwa kuunganisha iliyokuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Kukuza Maeneo ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).

Amesema kuwa mamlaka hiyo ina jukumu la kuratibu, kukuza na kuwezesha uwekezaji, kusimamia uendelezaji wa Maeneo Maalum ya Kiuchumi pamoja na kuishauri Serikali kuhusu masuala ya uwekezaji na kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Amesema kuwa kati ya mtaji wa uwekezaji uliosajiliwa, uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje ya nchi (FDI) ulifikia dola za Marekani bilioni 9.60, huku uwekezaji wa ndani ukifikia dola bilioni 5.72.

“Katika kuendeleza Maeneo Maalum ya Kiuchumi, TISEZA imeelekeza nguvu zake katika maeneo ya Bagamoyo, Kwala na Nala kwa lengo la kuvutia wawekezaji katika sekta za viwanda, uzalishaji, uchakataji wa mazao, biashara na usafirishaji.

“Kupitia juhudi hizo, mamlaka ilipokea maombi zaidi ya 80 ya matumizi ya ardhi katika maeneo hayo, ambapo maombi 43 yalifikia hatua ya kusainiwa kwa mikataba ya upangishaji au haki za upangaji wa ardhi. Uwekezaji unaotarajiwa katika maeneo hayo unakadiriwa kufikia zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.5 na kuzalisha ajira zaidi ya 15,844” amesema. Teri

Aidha amesema kuwa TISEZA imeendelea kuratibu ujenzi wa miundombinu katika eneo la Bagamoyo SEZ, ikiwemo barabara yenye urefu wa takribani kilomita 3.116, pamoja na kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha upatikanaji wa umeme katika eneo la hekta 151.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa katika eneo la Tanga SEZ, maandalizi ya Mpango Kabambe wa matumizi ya eneo hilo yamefikia asilimia 12.

Huduma kwa wawekezaji

Teri amesema kuwa katika kuboresha huduma kwa wawekezaji, TISEZA imeendelea kutumia Kituo cha Huduma za Pamoja kwa Wawekezaji (OSFC) na Kituo cha Huduma kwa Wawekezaji wa Kimkakati (PISC).

“Kupitia vituo hivyo, wawekezaji 524 walihudumiwa katika Premium Lounge. Kati yao, wawekezaji 34 walifanikiwa kusajili kampuni, huku miradi 83 ikisajiliwa kupitia mifumo ya Certificate of Incentives na Export Processing Zones (EPZ).

“Vilevile, wawekezaji 142 walipata ushauri kuhusu masuala ya ardhi, kodi, fursa za uwekezaji na huduma za kifedha” amesema Teri.

Amesema kuwa zaidi ya wajumbe 107 kutoka nchi na maeneo mbalimbali, yakiwemo Afrika, China, Japan, Ulaya, Urusi na Bulgaria, walipatiwa ushauri kuhusu fursa za uwekezaji nchini.

Pia, mamlaka imeandaa na kuzindua Sera ya Watoa Huduma kwa Wawekezaji ya mwaka 2025 (Investor Service Providers Policy, 2025), pamoja na jukwaa la watoa huduma hao kwa lengo la kuweka utaratibu wa usajili, ada na utoaji wa huduma kwa wawekezaji kwa uwazi na ufanisi.

Ufuatiliaji wa miradi ya uwekezaji

Katika kuhakikisha miradi iliyosajiliwa inatekelezwa, TISEZA ilitoa huduma za baada ya usajili wa miradi (investment aftercare) kwa miradi 789, sawa na asilimia 112.8 ya lengo lililowekwa.

Huduma hizo zilihusisha ziara katika maeneo ya miradi, mazungumzo na wawekezaji, ufuatiliaji wa utekelezaji pamoja na uratibu wa utatuzi wa changamoto zilizojitokeza.

Katika kipindi cha Aprili hadi Juni 2026, mamlaka ilifuatilia miradi 111 kati ya 141 iliyolengwa. Zoezi hilo lililenga kutathmini utekelezaji wa miradi, ajira zilizozalishwa, uzingatiaji wa sheria, mauzo ya nje, mapato ya fedha za kigeni na ongezeko la thamani ya malighafi zinazozalishwa nchini.

Kuhamasisha uwekezaji wa ndani

Amesema kuwa katika kuongeza ushiriki wa Watanzania kwenye shughuli za uwekezaji, TISEZA ilitekeleza Kampeni ya Kitaifa ya Kuhamasisha Uwekezaji wa Ndani ya mwaka 2026 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Mara, Kagera, Katavi, Rukwa, Mbeya na Songwe, pamoja na maeneo ya Kusini mwa Tanzania.

“Kampeni hiyo iliwafikia washiriki 1,402 na kutembelea na kuhakiki miradi 24 ya uwekezaji wa ndani katika sekta za utalii na ukarimu, uchakataji wa mazao, uongezaji thamani wa madini, viwanda na biashara.

Kupitia kampeni hiyo, wananchi walipata elimu kuhusu fursa za uwekezaji, huduma zinazotolewa na TISEZA, vivutio vya kodi na visivyo vya kodi pamoja na umuhimu wa kushiriki katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi” amesema.

Aidha, mamlaka ilizindua Kituo cha Utafutaji wa Masoko na Mauzo ya Nje (Sourcing and Export Centre) katika eneo la Benjamin William Mkapa SEZ, Mabibo, Dar es Salaam.

Kituo hicho kinalenga kuwasaidia wazalishaji, wafanyabiashara na wawekezaji, hususan vijana, kupata taarifa za masoko, teknolojia, vifaa vya uzalishaji, huduma za usafirishaji, ushauri na fursa za kuuza bidhaa nje ya nchi.

Mifumo ya kidijitali na mafunzo

Mkurugenzi ameongeza kuwa katika kuboresha ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za uwekezaji, TISEZA imeendelea kutumia mifumo ya kidijitali ya Open Data Kit (ODK) na KoboToolbox katika zoezi la ufuatiliaji wa miradi.

Mifumo hiyo inatumika kukusanya taarifa kuhusu hatua za utekelezaji wa miradi, ajira, kiwango cha uwekezaji, uzingatiaji wa sheria, viwianishi vya kijiografia na picha za miradi.

“Matumizi ya teknolojia hiyo yanalenga kupunguza matumizi ya nyaraka za karatasi, makosa ya uingizaji wa taarifa na kuboresha ubora wa takwimu zinazotumika katika kufanya maamuzi.

“Katika upande wa kujenga uwezo wa watumishi na wadau, TISEZA ilianzisha mafunzo kupitia TISEZA Training and Capacity Building Academy.

Mafunzo ya kwanza yalifanyika Juni 2 na 3, 2026, jijini Dodoma, yakilenga maandalizi ya miradi ya mpito wa nishati na uwekezaji ili iweze kukidhi vigezo vya kupata ufadhili” amesema.

Amesema kuwa washiriki walitoka katika taasisi mbalimbali za Serikali na fedha, zikiwemo Wizara ya Fedha, Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPPC), TANESCO, TGDC, TPDC, NDC, TIB Development Bank, Azania Bank na TISEZA.

Mafunzo hayo yalilenga kuongeza uelewa kuhusu namna ya kuandaa miradi inayoweza kupata ufadhili na kuimarisha mawasiliano kati ya waandaaji wa miradi na taasisi za fedha.

Mafunzo mengine yalifanyika Septemba 2 na 3, 2026, jijini Dodoma, kupitia programu ya majaribio ya pili (Pilot II), iliyokuwa na mada ya Effective Investment Facilitation for Investment Retention, Expansion and Economic Transformation. Programu ya tatu (Pilot III) imepangwa kufanyika Desemba 2026.

Tuzo na kutambuliwa

Katika kipindi hicho, TISEZA ilipata tuzo ya Leadership Excellence Award 2025 kutokana na mchango wake katika kuboresha na kubuni huduma kwa wawekezaji na wananchi.

Pia, Ofisi ya Kanda ya Ziwa ilitambuliwa kuwa miongoni mwa washiriki bora katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane ya mwaka 2025.

Kwa ujumla, mafanikio hayo yanaonesha hatua zilizopigwa na TISEZA katika kutekeleza majukumu yake baada ya kuunganishwa kwa TIC na EPZA, hususan katika usajili wa miradi, kuvutia mitaji, kuendeleza maeneo ya viwanda na kuboresha huduma kwa wawekezaji.

Amesema kuwa hata hivyo, mamlaka inakabiliwa na umuhimu wa kuharakisha ujenzi wa miundombinu katika Maeneo Maalum ya Kiuchumi, kuboresha upatikanaji wa huduma za msingi na kuimarisha uratibu na taasisi nyingine za Serikali.

Pia, kuna umuhimu wa kuondoa vikwazo vya kiudhibiti na kuimarisha matumizi ya mifumo jumuishi ya kidijitali pamoja na ufuatiliaji wa miradi ili kubaini tofauti kati ya uwekezaji uliosajiliwa na ule ulioanza kutekelezwa.

Hatua hizo zinatarajiwa kusaidia TISEZA kuongeza mchango wake katika kuvutia mitaji, kukuza viwanda, kuongeza mauzo ya nje na kuimarisha ushiriki wa wazalishaji wa ndani, sambamba na kuunga mkono malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.