Na Bituro Kazeri, JamhuriMedia, Mwanza

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limetoa wito rasmi kupitia barua ya Oktoba 23, 2026; Waraka huo namba TEC/Pr.No. 114/2026 ulisainiwa na Rais wa TEC ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Lindi, Mhashamu Wolfgang Pisa, ikielekeza kuadhimishwa kwa Misa Takatifu maalumu Oktoba 29, 2026 katika parokia zote, vituo vya sala na taasisi za Kanisa Katoliki nchini kote.

Maombi yanalenga kuliombea taifa amani, haki, ukweli, uponyaji wa kisaikolojia na kiroho na mshikamano huku ikikumbukwa kumekuwa na miaka tangu matukio hayo yenye maumivu makali kwa Watanzania.

Katika Kanisa Katoliki upo utaratibu wa kuwaombea marehemu ukijikita katika imani ya “Ushirika wa Watakatifu” (kuunganishwa kwa Kanisa la hapa duniani, Kanisa la toharani na Kanisa la mbinguni). Kanisa linafundisha kuwa sala na sadaka za Ekaristi huwasaidia marehemu walioko toharani kusafishwa dhambi zao nyepesi au madeni yao mbele ya Mungu (Rejea ya kibiblia: 2 Wamakabayo 12:38-45 na Katekisimu ya Kanisa Katoliki, namba 1032).

Kwa utaratibu huo kila ifikapo Novemba kila mwaka, Kanisa huweka msisitizo mkubwa wa pekee kuwaombea marehemu wote, huku Novemba 2 ikiwa Siku ya Kumbukumbu ya marehemu wote (All Souls’ Day).

Aidha, katika kila Misa Takatifu, wakati wa sala ya Ekaristi, Padri husali na kuwakumbuka maalumu wazima na wafu.

TEC imetaja mahsusi kabisa kuwa wito wake wa misa una nia na makusudio, kwanza, kuwakumbuka waliofarikidunia: Kuwaombea roho za Watanzania waliopoteza maisha katika vurugu hizo. Pili, uponyaji na faraja kwa kuwaombea uponyaji wale wote walioumizwa, kujeruhiwa na kupata athari za kisaikolojia au kiuchumi. Kusudio la tatu ni haki na ukweli kwa kuombea haki, uwazi, na ukweli kwa ajili ya wale waliopotea na familia zinazoomboleza na nne, amani ya taifa: Kuliombea Taifa la Tanzania, viongozi wake na wananchi wote ili kuimarisha umoja, upendo na mshikamano.

Tanzania tunayo matukio makubwa yaliyosababisha vifo vya Watanzania wenzetu. Kwa mfano tunalo tukio la vifo baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000 kule Zanzibar, vurugu hizo zilisababisha vifo vya watu takriban 23 (huku ripoti nyingine zikitaja idadi kubwa zaidi), majeruhi wengi, watu kukimbilia ukimbizini nchini Kenya na hofu kubwa katika historia ya kisiasa ya Tanzania lakini hatukuona TEC wakitualika kuadhimisha misa.

KWA HABARI ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA NOVEMBA 3-9, 2026