• Watuhumiwa wa makosa ya uhamiaji wakamatwa ndani ya miezi 15
• JAMHURI lashuhudia weledi wa watumishi, usafi wa hali ya juu ofisi za Uhamiaji Kurasini
Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Idara ya Uhamiaji nchini imewakamata na kuwachukulia hatua mbalimbali watuhumiwa 103,544 wa makosa yanayohusiana na uhamiaji katika kipindi cha miezi 15, kuanzia Julai 2025 hadi Septemba 2026; JAMHURI linaripoti.
Takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa kazi inayofanywa na taasisi katika kusimamia utekelezaji wa sheria za uhamiaji, kudhibiti mienendo ya watu wanaoingia na kutoka nchini na kuhakikisha taratibu za ukaazi zinafuatwa.
JAMHURI limeelezwa wiki iliyopita kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja, kuanzia Julai 2025 hadi Juni 2026, jumla ya watuhumiwa 87,366 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali kwa makosa yanayohusiana na uhamiaji.
“Katika kipindi cha miezi mitatu iliyofuata, kuanzia Julai hadi Septemba 2026, watuhumiwa wengine 16,178 walikamatwa na kuchukuliwa hatua mbalimbali,” inasema taarifa iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji kwa JAMHURI.
Takwimu hizo zinamaanisha kuwa kwa wastani, katika kipindi cha miezi 12, watuhumiwa wapatao 239 walikuwa wakikamatwa kwa siku, huku katika miezi mitatu iliyofuata wastani ukiwa takribani watuhumiwa 176 kwa siku.
Uhamiaji imekuwa ikifanya operesheni za mara kwa mara kwa mujibu wa sheria kudhibiti matatizo kama wahamiaji haramu, usafirishaji haramu wa binadamu kwa lengo la kuwanyonya (human trafficking) na magendo ya binadamu (human smuggling).
Wakati tatizo la uhamiaji haramu likiendelea hasa katika mikoa ya mipakani, katika miaka ya karibuni tatizo la magendo ya binadamu limepungua baada ya kwanza Idara ya UHAMIAJI kurekebisha sheria ya ‘visa’ kwa raia wa mataifa yaliyokuwa yakikimbiwa na watu wake; na pili kutokana na kuibuka kwa machafuko dhidi ya wageni huko Afrika Kusini.
Majukumu ya Idara ya Uhamiaji ni kusimamia utekelezaji wa sheria zinazohusu uingiaji na utokaji wa watu nchini, vibali vya ukaazi na masuala mengine yanayohusiana na uhamiaji.
Utekelezaji wa majukumu hayo ni muhimu katika kulinda mipaka ya nchi, kusimamia taratibu za kisheria na kuhakikisha watu wanaoingia na kuishi Tanzania wanafuata masharti yaliyowekwa.

JAMHURI lashuhudia weledi, usafi Kurasini
Kwa upande mwingine, likiwa Ofisi za Uhamiaji Kurasini jijini Dar es Salaam, JAMHURI limeshuhudia mazingira ya usafi wa hali ya juu, huku huduma kwa wananchi zikiendelea kutolewa kwa utaratibu na weledi.
Weledi wa watumishi wa Uhamiaji unaanza kuonekana kuanzia mapokezi hadi ndani kwa maofisa wa ngazi na vyeo mbalimbali katika kuwahudumia wageni kutoka ndani na nje ya nchi kwa nidhamu, ustaarabu, ukarimu na kasi ya kushughulikia mahitaji ya wananchi.
“Hatupendi kuona watu wakishinda hapa siku nzima. Kila mtu apate huduma anayostahili mapema na kwenda kuendelea na shughuli zake,” JAMHURI limemsikia ofisa mmoja wa Uhamiaji akitoa maelekezo kwa ofisa wa ngazi ya chini Ijumaa wiki iliyopita.
Ofisa husika alitoa maelekezo baada ya kumwona mzee mwenye takribani miaka 70 aliyeambatana na mwanamke mtu mzima wakiwa kwenye viti vya wateja wakisubiri huduma.
Jina la ofisa huyo halikupatikana mara moja kwa kuwa hakuwa amevaa sare, lakini aliyepewa maelekezo, sare yake ilikuwa na jina la ‘Mallya’.
Upande wa huduma za kijamii, JAMHURI limeshuhudia maliwato za Kurasini zikiwa katika hali ya usafi wa hali ya juu tayari kutumiwa na wateja bila kusababisha adha ya aina yoyote, iwe harufu kali au ukosefu wa maji.
Mazingira ya ndani na nje ya maliwato, pamoja na maeneo mengine yaliyotembelewa yalikuwa nadhifu na yenye kuvutia, hali inayoendana na weledi na utaratibu mzuri wa utoaji huduma ulioshuhudiwa katika ofisi hizo.

