Na Mwandshi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umeokoa Sh bilioni 47.26 kupitia operesheni za kudhibiti udanganyifu katika kipindi cha miaka 7 kuanzia Julai 2018 hadi Juni 2025.

Katika kipindi hicho, Mfuko ulifanya uchunguzi 747, kusimamisha matumizi ya kadi 13,053 za wanachama, kusitisha mikataba ya vituo vya kutolea huduma za afya 52 na kuwaripoti wataalamu 234 wa afya katika bodi zao za kitaaluma.

Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk. Irene Isaka, ameyasema hayo katika wasilisho lake kwenye kikao kazi kati ya Mfuko na wahariri wa vyombo vya habari kilichofanyika Dar es Salaam, mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa Dk. Isaka, katika mwaka wa fedha wa 2024/2025 pekee, NHIF ilifanya uchunguzi 76 na kutembelea vituo 527 vya huduma za afya. Operesheni hizo ziliokoa Sh bilioni 6.07, kusitisha matumizi ya kadi 1,090 na kuvunja mikataba ya vituo vinne. Aidha, wataalamu 13 wa afya waliripotiwa kwenye bodi zao za taaluma.

Mafanikio hayo yanakwenda sambamba na jitihada za kuimarisha hali ya kifedha ya Mfuko, ambao umefikisha akiba ya Sh trilioni 1.31 hadi mwisho wa mwaka wa fedha 2025/26.

Dk. Isaka amesema rasilimali hizo zinaiwezesha NHIF kuhimili mahitaji yake kwa zaidi ya miaka miwili, huku ikiendelea kulipa madai ya watoa huduma na kuhudumia wanachama.

Katika hatua nyingine ya kuimarisha mapato, NHIF imekusanya Sh bilioni 96.56 kati ya Sh bilioni 104.1 zilizokuwa zinadaiwa kutoka kwa waajiri hadi Septemba, mwaka huu.

Hata hivyo, ukaguzi ulibaini kuwa Sh bilioni 5.59 hazikuwa deni halisi, bali zilitokana na makosa ya ankara na uhamishaji wa taarifa wakati wa mabadiliko ya mifumo. Kiasi kilichobaki kinachopaswa kukusanywa ni Sh bilioni 1.95.

KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA JAMHURI LA NOVEMBA 10- 16, 2026