Na Waandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Hukumu ya kifungo cha miaka minne jela bila faini dhidi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, imeibua mjadala mzito nchini; JAMHURI linaripoti.
Mjadala huo unahusu hasa njia za kisheria na kisiasa zinazoweza kutumika kumwezesha mwanasheria na mwanasiasa huyo maarufu kurejea uraiani; wengi wakihoji sababu ya kutotozwa faini.
Wasomi, wachambuzi wa siasa, viongozi wa vyama na wanaharakati waliozungumza na JAMHURI wameibua hoja za rufaa, dhamana, mamlaka ya Rais kutoa msamaha na umuhimu wa mazungumzo katika kutafuta maridhiano ya kitaifa.
Mjadala huo umeibuka baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, Novemba 6, 2026, kumwachia Lissu katika shtaka la uhaini ambalo ndilo lililoaminika kuwa pekee linalomkabili, lakini ikamtia hatiani kwa kosa la uchochezi.
Jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru, limeeleza kuwa upande wa mashtaka haukuthibitisha vipengele vyote vya kosa la uhaini, lakini ushahidi ulitosha kuthibitisha kosa la uchochezi.
Uamuzi huo umehitimisha kesi iliyomweka Lissu rumande kwa siku 577, huku ukiibua maswali kuhusu matumizi ya sheria, adhabu iliyotolewa na hatima ya maridhiano ya kisiasa nchini.
Njia za kisheria
Kwa mujibu wa Kifungu cha 319 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, mahakama inaweza kumtia hatiani mshtakiwa kwa kosa dogo linalotokana na baadhi ya vipengele vya kosa kubwa aliloshtakiwa nalo, iwapo masharti ya kifungu hicho yametimia.
Mahakama imetumia mamlaka hayo kumtia Lissu hatiani kwa uchochezi chini ya Kifungu cha 390 cha Kanuni ya Adhabu. Hata hivyo, mjadala umeibuka iwapo uchochezi unaweza kuhesabiwa kuwa kosa dogo linalotokana na vipengele vya uhaini, na kama Lissu alipata nafasi ya kutosha kujitetea dhidi ya kosa hilo.
Maswali hayo yanaweza kuwa sehemu ya hoja za rufaa, lakini uamuzi wa kama mahakama ilikosea kisheria unabaki kuwa wa mahakama yenye mamlaka ya kusikiliza rufaa.
Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha CHADEMA, Dk. Rugemeleza Nshala, ametangaza kwamba upande wa Lissu unakusudia kukata rufaa na kuomba dhamana wakati ukisubiri kusikilizwa kwake. Hata hivyo, dhamana baada ya mshtakiwa kuhukumiwa si haki ya moja kwa moja, kwani mahakama huenda ikalazimika kuzingatia uwepo wa mazingira ya kipekee (ya Lissu kupewa dhamana); hoja nzito za kisheria katika rufaa; hali ya afya inayothibitishwa kitabibu na uwezekano wa mhusika kutumikia sehemu kubwa ya kifungo kabla ya rufaa kusikilizwa.
KWA HABARI ZA KINA ZAIDI SOMA GAZETI LA JAMHURI LA NOVEMBA 10 – 16, 2026



