Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Stanslaus Nyongo, amewataka wananchi kujitokeza kupata huduma za uchunguzi na matibabu kutoka kwa Madaktari Bingwa na wabobezi watakaotoa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tumbi kuanzia Novemba 16 hadi 20 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Novemba 11,2026 Nyongo amefafanua kuwa, kambi hiyo ya siku tano inalenga kuwafikishia wananchi huduma za kibingwa ambazo wakati mwingine hulazimika kuzifuata katika hospitali za umbali mrefu.

Aliwahimiza wananchi kujenga utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara badala ya kusubiri hadi wanapougua au hali zao kuwa mbaya.

Nyongo alielezea, katika kambi hiyo zitatolewa huduma za uchunguzi, ushauri, matibabu na upasuaji katika kada mbalimbali za afya, huku baadhi ya huduma zikitolewa bila malipo, zikiwemo upimaji wa sukari, uchunguzi wa homa ya ini na upasuaji wa mtoto wa jicho.

Alieleza kuwa wananchi watakaohitaji huduma zaidi watachangia gharama kwa viwango nafuu vilivyowekwa na Serikali, ikiwemo dawa, vipimo vya maabara, uchunguzi wa picha na upasuaji, huku akibainisha kuwa bima zote za afya zitakubaliwa katika kambi hiyo.

Nyongo alitaja huduma zitakazopatikana kuwa ni pamoja na uchunguzi wa magonjwa ya moyo, saratani ya shingo ya kizazi, mfumo wa mkojo, ubongo, ngozi, macho, kinywa, magonjwa ya watoto, uzazi, afya ya akili pamoja na matatizo ya mifupa na mgongo.

Alisema pia kutakuwa na huduma za uchunguzi wa mionzi, picha za kitabibu, CT Scan na Ultrasound.

Kwa upande wake, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Tumbi Silas Msangi alisema kambi hiyo itawakutanisha Madaktari Bingwa na wabobezi kutoka mikoa ya Singida, Morogoro, Pwani, Iringa na Dodoma pamoja na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

8888888888888888888888