Na Mwandishi Wetu, JammhuriMedia,
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limekamata silaha 105, watuhumiwa 385 wa ujangili na kutibua mitego 1,971 iliyokuwa ikitumika katika vitendo vya ujangili ndani ya hifadhi za taifa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Katika kipindi hicho, shirika hilo pia limekamata mifugo 65,600 iliyokuwa ikiingia ndani ya hifadhi kinyume cha sheria, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori na mazingira.
Mafanikio hayo yanaenda sambamba na matumizi ya teknolojia za kisasa, ikiwemo ndege zisizo na rubani (drones), mifumo ya GPS na vituo vya mawasiliano kwa ajili ya kufuatilia mienendo ya wanyamapori, kuimarisha doria na kupunguza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.
Kamishna Mkuu wa Uhifadhi wa TANAPA, Massana Gibril Mwishawa, ameyasema hayo Novemba 10, 2026, wakati akizungumza katika kikao kazi na wahariri kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR), katika ukumbi wa JNICC, Dar es Salaam.
Amesema mafanikio hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan za kuimarisha uhifadhi, kulinda rasilimali za wanyamapori na kukuza mchango wa sekta ya utalii katika maendeleo ya taifa.
Akifafanua hatua zilizochukuliwa katika kupambana na ujangili, Mwishawa amesema TANAPA imefanya doria 31,314 katika kipindi hicho, idadi inayozidi mara mbili doria 14,940 zilizokuwa zimepangwa.
“Tumekamata watuhumiwa wa ujangili 385 katika matukio mbalimbali na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria kwa hatua zaidi. Lengo ni kuhakikisha uhalifu huo unadhibitiwa na rasilimali zetu zinaendelea kulindwa,” amesema.
Amesema matumizi ya teknolojia yameongeza ufanisi katika shughuli za ulinzi, ambapo shirika hilo limepata ndege zisizo na rubani 40 zinazotumika kufanya doria za angani, kufuatilia mienendo ya wanyamapori na kubaini maeneo yenye viashiria vya uhalifu.
Ameongeza kuwa TANAPA imeweka mifumo ya GPS kwa baadhi ya wanyamapori ili kufuatilia mienendo yao na kutoa taarifa mapema wanapokaribia maeneo yanayokaliwa na wananchi, hatua inayolenga kupunguza madhara yanayotokana na migogoro baina ya binadamu na wanyamapori.
Katika kuimarisha mawasiliano na usalama wa hifadhi, Mwishawa amesema shirika hilo limejenga vituo vitatu vya kisasa vya mawasiliano katika Hifadhi za Taifa za Serengeti na Nyerere.
Aidha, linaendelea kuboresha mifumo ya mawasiliano ya redio katika hifadhi za Serengeti, Ziwa Manyara, Tarangire, Mkomazi na Nyerere ili kurahisisha mawasiliano kati ya askari wa wanyamapori na vyombo vingine vya usalama.
Katika eneo la urejeshaji wa mazingira, amesema TANAPA imeendelea kukabiliana na uharibifu wa mifumo ikolojia kwa kudhibiti mimea vamizi katika hekta 984.2 kwenye hifadhi 15 na kusafisha hekta 1,546 zilizokuwa zimeathiriwa na vichaka katika Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
Amesema juhudi hizo zinalenga kurejesha maeneo ya malisho ya wanyamapori na kuboresha mazingira yao, ili kupunguza changamoto ya wanyama kutoka ndani ya hifadhi na kuingia katika maeneo ya wananchi kutafuta chakula.
Mwishawa amesema shirika hilo pia limefanikiwa kurejesha ukanda wa ikolojia unaounganisha Hifadhi za Taifa za Katavi na Milima Mahale kwa kushirikiana na wananchi, hatua inayosaidia kuhifadhi misitu ya asili na kuwezesha wanyamapori kuhama kati ya hifadhi hizo.
Ameeleza kuwa wananchi wanaozunguka eneo hilo wananufaika kiuchumi kupitia shughuli mbalimbali, ikiwemo biashara ya hewa ukaa na mikataba inayowezesha upatikanaji wa mapato kwa ajili ya kuendeleza shughuli za uhifadhi.
Kuhusu mchango wa uhifadhi katika maendeleo ya jamii, amesema TANAPA imeendelea kutekeleza miradi ya kijamii katika maeneo yanayozunguka hifadhi, ikiwemo ujenzi wa zahanati, madarasa, nyumba za walimu, miundombinu ya maji na barabara.
Amesema shirika hilo pia linaendelea kutoa ajira kwa Watanzania, hususan vijana wanaotoka katika jamii zinazozunguka hifadhi, pamoja na kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa sekta ya utalii ili kuongeza fursa za ajira katika hoteli, usafirishaji na huduma nyingine zinazohusiana na utalii.
Amesisitiza kuwa TANAPA itaendelea kushirikiana na wananchi, taasisi za Serikali na wadau wengine kuhakikisha uhifadhi wa rasilimali za taifa unakuwa endelevu na kuleta manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.










