Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia, Arusha

Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR) imeadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake huku ikiwa na changamoto ya kutotekelezwa kwa sehemu kubwa ya maamuzi yake na nchi husika, hali inayozua wasiwasi kuhusu upatikanaji wa haki na ufanisi wa utekelezaji wa hukumu zinazotolewa na taasisi hiyo.

Licha ya kupokea zaidi ya kesi 350 na kutoa maamuzi katika takribani kesi 200, mahakama hiyo bado inakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha nchi zinazohusika zinatekeleza hukumu hizo na kuwapatia haki wananchi waliowasilisha mashauri yao.

Rais Mstaafu wa Mahakama hiyo, Jaji Imani Aboud, amesema katika kipindi cha miaka 20 taasisi hiyo imepiga hatua kubwa katika kutekeleza jukumu lake la kulinda na kusimamia haki za binadamu barani Afrika, licha ya changamoto zinazohitaji ushirikiano wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).

Akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya mahakama hiyo yaliyofanyika jijini Arusha, amesema mahakama hiyo ilianzishwa ikiwa na nchi 12 zilizokubali kutambua mamlaka yake kupitia matamko maalumu yaliyokuwa yanaruhusu wananchi na taasisi husika kuwasilisha mashauri moja kwa moja mahakamani hapo.

Amesema mafanikio ya mahakama hiyo yanaonekana kupitia ongezeko la kesi zinazowasilishwa, ambapo kati ya zaidi ya kesi 350 zilizopokelewa, takribani 200 tayari zimeamuliwa huku nyingine zikiendelea kushughulikiwa.

Hata hivyo amesema baadhi ya nchi zimeondoa matamko yaliyokuwa yanaruhusu wananchi na mashirika yasiyo ya kiserikali kufikisha mashauri moja kwa moja mahakamani hapo, hatua inayopunguza fursa ya wananchi kutumia chombo hicho kutafuta haki.

Jaji Aboud amesema mahakama imeongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma kuhusu uwepo wake, majukumu na namna ya kuwasilisha malalamiko kupitia kampeni zilizofanyika katika nchi mbalimbali za Afrika hususan katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Ameeleza kuwa Tanzania ambayo ni mwenyeji wa mahakama hiyo, imeonesha dhamira ya kuiunga mkono kwa kuwekeza katika ujenzi wa jengo maalumu litakalotumika kwa shughuli zake, akisema kukamilika kwake kutaboresha mazingira ya kazi na kuimarisha miundombinu ya taasisi hiyo.

Akizungumzia utekelezaji wa hukumu, Jaji Aboud amesema baadhi ya nchi zimeanza kuonesha utayari wa kutekeleza maamuzi ya mahakama kutokana na juhudi za uhamasishaji, lakini bado kuna changamoto kubwa inayohitaji kushughulikiwa.

“Kutoa hukumu pekee hakutoshi iwapo nchi husika hazitachukua hatua za kuhakikisha maamuzi hayo yanatekelezwa na wananchi wanapata haki zao” alisema.

Ameongeza kuwa maamuzi ya mahakama hiyo yana umuhimu mpana zaidi ya kutatua migogoro ya watu binafsi, kwani yanaweka viwango vinavyopaswa kuzingatiwa na nchi za Afrika katika masuala ya uchaguzi, haki za wanawake na maeneo mengine yanayohusu haki za msingi kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu pamoja na mikataba mingine ya kimataifa.

Kwa upande wake Wakili Bahame Nyanduga kutoka Tanzania ambaye ni mdau mkubwa wa mahakama hiyo, amesema mahakama hiyo inakabiliwa na changamoto kuu mbili ambazo ni upungufu wa rasilimali watu na fedha, pamoja na nchi wanachama kutoridhia kikamilifu masharti yanayowezesha wananchi kufikisha mashauri yao moja kwa moja katika taasisi hiyo.

Amesema licha ya mahakama hiyo kuwa na majaji 11 kwa mujibu wa mkataba ulioianzisha, bado inahitaji watumishi wa kutosha katika vitengo mbalimbali ili kuimarisha utendaji wake hasa ikizingatiwa kuwa majukumu yake yanaweza kupanuka kupitia Mkataba wa Malabo unaolenga kuongeza mamlaka ya mahakama katika masuala ya utawala bora na demokrasia.

Nyanduga amesema changamoto ya upatikanaji wa haki inajitokeza pia katika masharti ya kuruhusu wananchi na mashirika yasiyo ya kiserikali kuwasilisha kesi moja kwa moja, akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano hadi kumi ya mwanzo, kati ya nchi 34 zilizokuwa zimeridhia mkataba wa mahakama hiyo ni nchi 10 pekee zilizokuwa zimekubali utaratibu huo.

“Hali hii imeendelea kuwa kikwazo baada ya baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania, kujiondoa katika matamko hayo na kwa sasa ni nchi saba pekee kati ya nchi 55 za Afrika ambazo wananchi wake wanaweza kufikisha mashauri moja kwa moja katika mahakama hii”.

Ameonya kuwa changamoto hizo zisiposhughulikiwa, mahakama inaweza kuendelea kuhudumia idadi ndogo ya nchi badala ya kutekeleza dhamira yake ya kuwa chombo cha bara zima katika kulinda haki za binadamu, akizitaka nchi wanachama kuhakikisha inapata rasilimali za kutosha na wananchi wanapewa fursa ya kuifikia.

Awali akifungua kongamano la maadhimisho hayo, Rais wa Mahakama hiyo Jaji Blaise Tchikaya, amesema miaka 20 ya mahakama hiyo ni kipindi muhimu cha kutafakari mafanikio, changamoto na mustakabali wa taasisi za haki barani Afrika.

Amesema haki inahitaji tafakari, majadiliano na kubadilishana maoni huku akisisitiza umuhimu wa Waafrika kuwa na imani na taasisi zao katika kuhakikisha demokrasia, utawala bora na haki za binadamu vinaimarishwa barani humo.