Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Arusha
Benki ya CRDB imetoa mikopo yenye thamani ya Sh trilioni 4.3 katika sekta ya kilimo hadi sasa, kiasi kinachowakilisha asilimia 45 ya mikopo yote inayotolewa na taasisi za fedha nchini katika sekta hiyo. Hatua hiyo ni sehemu ya dhamira ya Benki ya kuchochea uwekezaji, kuongeza uzalishaji na kuimarisha mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, ikiwemo mazao ya bustani (horticulture).
Akizungumza na waandishi wa habari pembezoni mwa Maonesho ya Horti Logistica yanayoendelea jijini Arusha, ambako Benki ya CRDB ni mdhamini mkuu, Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa Benki hiyo, Maregesi Shabaan, alisema CRDB imeendelea kuwa mdau muhimu katika maendeleo ya sekta ya kilimo kwa kutoa mikopo na huduma za kifedha zinazolenga kuwawezesha wakulima, wafanyabiashara na wawekezaji katika hatua mbalimbali za mnyororo wa thamani.
Alibainisha kuwa mchango huo unaifanya CRDB kuwa miongoni mwa taasisi zinazoongoza katika kufadhili sekta ya kilimo nchini, huku Benki ikiendelea kujipanga kuongeza uwekezaji wake ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa.
Akizungumzia ushiriki wa Benki katika maonesho hayo, Maregesi alisema udhamini huo ni sehemu ya juhudi za CRDB kuunganisha wakulima, wawekezaji, wanunuzi na wadau wengine wa mnyororo wa thamani wa mazao ya bustani kutoka ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kukuza fursa za uwekezaji, biashara na masoko.
Kupitia banda lake katika maonesho hayo, Benki inatoa huduma mbalimbali za kibenki, ikiwemo kupokea amana, kufanya malipo na kutoa elimu kuhusu fursa za mikopo na uwezeshaji wa kifedha. Huduma hizo zinalenga kuwasaidia washiriki kutambua fursa zilizopo na kupata suluhisho za kifedha zitakazowawezesha kupanua na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.
Maregesi alieleza kuridhishwa na mwitikio wa Serikali na sekta binafsi katika maonesho hayo, akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za fedha na wadau wa sekta binafsi ni muhimu katika kuvutia uwekezaji, kuongeza uzalishaji na kuimarisha ushindani wa mazao ya Tanzania katika masoko ya ndani na kimataifa.
Alisema maendeleo katika sekta ya kilimo yanaonekana kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa, ongezeko la uzalishaji na kuimarika kwa shughuli za uchakataji na uongezaji thamani wa mazao. Wazalishaji wengi sasa wanatumia teknolojia za kisasa kuongeza uzalishaji, kuchakata mazao badala ya kuyauza yakiwa ghafi na kuyafungasha kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa katika masoko ya kimataifa, hatua inayofungua fursa zaidi za biashara na kuongeza thamani ya mazao ya ndani.
Alisisitiza kuwa Benki ya CRDB iko tayari kuwa mshirika wa kifedha wa wawekezaji katika hatua zote za mnyororo wa thamani wa kilimo, kuanzia uzalishaji mashambani, ufugaji, usindikaji na uchakataji, hadi biashara na usafirishaji wa mazao. Aliwakaribisha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia huduma za Benki hiyo kutekeleza na kukuza miradi yao.
Katika kuimarisha nafasi yake kama mshirika wa biashara na uwekezaji wa kimataifa, Maregesi alisema CRDB imepanua wigo wa shughuli zake nje ya Tanzania kwa kuwa na shughuli za kibenki nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na uwepo wa ofisi Dubai, hatua inayoiwezesha kuunganisha wateja na wawekezaji na fursa za biashara katika masoko mbalimbali.
Aidha, alisema Benki ya CRDB ni benki ya kwanza nchini kupata ithibati ya Mfuko wa Tabianchi wa Umoja wa Mataifa (Green Climate Fund – GCF), hatua iliyowezesha kutengwa kwa jumla ya Dola za Marekani milioni 200 kwa ajili ya kutekeleza Programu ya Kilimo Himilivu dhidi ya Mabadiliko ya Tabianchi. Kiasi hicho kinajumuisha Dola milioni 100 kutoka GCF na Dola milioni 100 kutoka Benki ya CRDB, kupitia ushirikiano unaolenga kuwawezesha wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha uzalishaji wa chakula na kujenga mifumo ya kilimo endelevu na himilivu.
Alieleza kuwa mafanikio hayo yamewezekana kupitia ushirikiano na Ofisi ya Makamu wa Rais inayosimamia masuala ya mazingira, huku akiishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi yanayoruhusu taasisi za kifedha kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Aliwahimiza wawekezaji kutoka Tanzania, Afrika na maeneo mengine duniani kuitumia Benki ya CRDB kama mshirika wao wa kifedha katika kutekeleza miradi mbalimbali, akisisitiza kuwa Benki iko tayari kutoa huduma za kisasa na suluhisho za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wawekezaji katika sekta mbalimbali.
Alisema kaulimbiu ya Benki ya CRDB, “Ulipo, Tupo,” inaakisi dhamira ya Benki ya kuendelea kuwafikia wakulima, wafanyabiashara na wawekezaji katika maeneo mbalimbali, kuwawezesha kupata huduma na mitaji inayohitajika na kuwa mshirika wao katika kukuza shughuli za kiuchumi.
Akizungumza katika maonesho hayo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, ambaye alikuwa Mgeni Rasmi, aliipongeza Benki ya CRDB kwa mchango wake katika kuwawezesha wakulima kupitia mikopo na huduma mbalimbali za kifedha. Aliihimiza Benki hiyo kuendelea kuongeza mikopo na kuimarisha mifumo ya udhamini wa shughuli za kiuchumi ili kuwafikia wakulima wengi zaidi, kuchochea uwekezaji na kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo.



