📌Akagua Mradi wa njia ya kusafirisha umeme Msongo wa Kv 220 Songea – Tunduru – Masasi

📌Aagiza Meneja wa Mradi upande wa Mkandarasi kuondolewa ili kuongeza kasi ya utekelezaji.

📌Atoa rai kwa TANESCO kupeleka wataalamu kuongeza nguvu ya utekelezaji wa mradi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Deogratius Ndejembi, ameitaka Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha inambana na kumsimamia Mkandarasi anayetekeleza mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovolti 220 ya Songea–Tunduru–Masasi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati.

Amesema Kampuni ya Kalpataru inayotekeleza mradi huo imekuwa ikifanya kazi kwa kasi isiyoridhisha, hali inayokwenda kinyume na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wa Mikoa ya Kusini, ikiwemo Ruvuma, Lindi na Mtwara, kupata huduma ya umeme wa uhakika kupitia Gridi ya Taifa.

Akizungumza leo Novemba 11, 2026 Makamu huyo wa Rais amesema utekelezaji wa miradi ya umeme katika Mikoa ya Kusini inatarajiwa kuimarisha uwezo wa usafirishaji umeme na kuongeza thamani ya maisha ya wananchi kwa kufungua fursa za kiuchumi katika sekta za uchimbaji madini, kilimo na uzalishaji viwandani.

Amesema wananchi wa Mikoa ya Kusini, hususani Wilaya ya Tunduru, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika kutokana na umeme wanaoupata kusafirishwa kutoka umbali mrefu.

“Mradi huu ni muhimu kwa kuwa utachangia Mikoa ya Kusini kuunganishwa na Gridi ya Taifa. Mahitaji ya juu ya wananchi wa Tunduru ni Megawati 4, ambazo zinasafiri umbali mrefu, hivyo kusababisha changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika. Natoa rai kwa TANESCO kupeleka wataalamu wake kuongeza nguvu katika utekelezaji wa mradi huu ili ukamilike kwa wakati,” amefafanua Mheshimiwa Ndejembi.

Aidha, amesema Serikali hivi karibuni imetoa zaidi ya Shilingi bilioni 42 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, kama ilivyoombwa na Mkandarasi, lakini kasi ya utekelezaji haiendani na ahadi na makubaliano yaliyofikiwa.

Naye Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba, amesema awali utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Tunduru hadi Masasi ulikuwa asilimia sita, lakini baada ya Serikali kumpatia fedha Mkandarasi utekelezaji umeongezeka na kufikia asilimia 35 huku mradi wa njia ya kusafirisha umeme Songea – Tunduru ukiwa umefikia asilimia 58.

“Wizara itahakikisha inamsimamia Mkandarasi ili ifikapo Septemba 30, 2027, mradi uwe umekamilika. Tunafahamu umuhimu wa mradi huu kwa wananchi wa Mikoa ya Kusini na tunahakikisha kazi hii inafanyika kwa haraka na kwa ufanisi,” amesema Mhe. Salome.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, amesema sehemu ya kwanza ya mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru, yenye urefu wa kilomita 214.5, inatekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 151, huku sehemu ya pili kutoka Tunduru hadi Masasi, yenye urefu wa kilomita 177, ikitekelezwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 158.

“Mradi huu ni sehemu ya miradi 27 ya Gridi Imara inayotekelezwa na Serikali kupitia TANESCO kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme. Kwa ujumla mradi umefikia asilimia 58. Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Tunduru kitafungwa transfoma mbili zenye uwezo wa MVA 60 kila moja na kitakuwa na matoleo 10 ya msongo wa Kilovoti 33 yatakayohudumia maeneo mbalimbali ya wananchi,” amesema Bw. Twange.

Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Kalpataru kutoka India unatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 30, 2027, ambao utakuwa chachu ya kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuchochea shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi katika Mikoa ya Kusini.