Na Mwandishi Wetu.
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeendelea kuimarisha juhudi za kulinda afya za wananchi na kukuza biashara zenye kuzingatia viwango kwa kutoa elimu kwa wafanyabiashara wadogo wadogo kuhusu umuhimu wa usalama wa chakula, ubora wa bidhaa na uzingatiaji wa matakwa ya kisheria katika shughuli zao za kila siku.
Elimu hiyo imetolewa leo, Septemba 26, 2026, wakati TBS iliposhiriki Kongamano la Wafanyabiashara Ndogo Ndogo lililofanyika katika Viwanja vya TEFA, Temeke, jijini Dar es Salaam, lililobeba kaulimbiu isemayo “Maendeleo Yangu, Mtaa Wangu, Urasimishaji ndio Uchumi wa Sasa.”
Kupitia kongamano hilo, TBS imekutana na makundi mbalimbali ya wafanyabiashara, wakiwemo Mama Lishe, Baba Lishe na wafanyabiashara wa nguo za mitumba maarufu kama Machinga, kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango na kulinda afya za watumiaji wa bidhaa na huduma zao.
Akizungumza na wafanyabiashara katika kongamano hilo, Meneja wa Tathmini ya Vihatarishi katika Chakula wa TBS, Bi. Immaculatha Justin Tarimo, amesema shirika hilo limetumia fursa hiyo kutoa elimu kwa wafanyabiashara wa chakula, hususan Mama Lishe na Baba Lishe wanaofanya shughuli zao katika maeneo yenye mikusanyiko ya watu, ikiwemo masoko, stendi na maeneo mengine ya biashara.
Amesema elimu hiyo imelenga kuwahimiza wafanyabiashara hao kuandaa na kuhifadhi chakula katika mazingira safi na salama, ili kulinda afya za wateja wao na kuhakikisha kuwa chakula kinachouzwa kwa walaji kinakuwa salama kwa matumizi ya binadamu.
Bi. Tarimo amesisitiza kuwa kuzingatia usafi katika maandalizi na uhifadhi wa chakula ni jambo muhimu katika kuzuia vihatarishi vinavyoweza kusababisha madhara kwa afya za walaji, hivyo ni wajibu wa kila mfanyabiashara wa chakula kuhakikisha anazingatia maelekezo yanayotolewa na mamlaka husika.
Aidha, amesema wafanyabiashara hao wamekumbushwa kuhusu umuhimu wa kusajili majengo wanayotumia katika shughuli zao za biashara ya chakula, hatua inayochangia kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika katika mazingira yanayokidhi matakwa ya usalama na viwango vinavyohitajika.
Katika hatua nyingine, TBS imetoa elimu kwa wafanyabiashara wa nguo za mitumba kuhusu udhibiti wa uuzaji wa nguo za ndani zilizotumika, zikiwemo nguo za ndani za wanawake na wanaume, mataulo pamoja na nguo nyingine zinazovaliwa katika maeneo nyeti ya mwili wa binadamu.
Wafanyabiashara hao wameelezwa kuwa kwa mujibu wa matakwa ya kisheria, bidhaa hizo zilizotumika haziruhusiwi kuuzwa, kutokana na hatari zinazoweza kujitokeza kwa afya za watumiaji, ikiwemo uwezekano wa kuathiriwa na maradhi kutokana na matumizi ya nguo hizo na watu wengine.
Elimu hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa wafanyabiashara kuhusu bidhaa ambazo haziruhusiwi kuuzwa, huku ikiwahimiza kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa katika biashara ya nguo za mitumba, kwa maslahi ya afya ya jamii.
Wakizungumza katika kongamano hilo, wafanyabiashara walioshiriki wameishukuru TBS kwa kuwafikishia elimu hiyo, wakieleza kuwa imewasaidia kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango, kulinda afya za wananchi na kufanya biashara kwa kuzingatia matakwa ya kisheria.
Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wa nguo za mitumba, Bw. Salehe Omary, mfanyabiashara wa nguo za mitumba katika Soko la Tandika, amesema wameipokea elimu hiyo na kuahidi kuwafikishia wafanyabiashara wengine ili kuongeza uelewa kuhusu bidhaa zisizoruhusiwa kuuzwa na umuhimu wa kulinda afya za watanzania.
Amesema ushirikiano kati ya TBS na wafanyabiashara ni muhimu katika kuhakikisha elimu ya viwango inawafikia wadau wengi zaidi, hususan wafanyabiashara wadogo wanaohudumia wananchi katika masoko na maeneo mbalimbali ya biashara.
Kwa upande wake, Bi. Elizabeth Mfugale, ambaye ni mfanyabiashara wa chakula maarufu kama Mama Lishe, ameishukuru TBS kwa elimu waliyoipata na kuahidi kuyatekeleza maelekezo waliyopewa, hususan katika kuhakikisha chakula kinaandaliwa na kuhifadhiwa katika mazingira safi na salama.
Amesema elimu hiyo ni muhimu kwao kama watoa huduma za chakula, kwani inawasaidia kutambua wajibu wao katika kulinda afya za wateja na kuhakikisha wanapata chakula salama.
Ushiriki wa TBS katika kongamano hilo ni sehemu ya jitihada za kuendelea kuwaelimisha wafanyabiashara kuhusu viwango, usalama wa bidhaa na uzingatiaji wa sheria, huku ukichochea ujenzi wa mazingira bora ya biashara yanayolinda afya za wananchi na kuchangia maendeleo ya uchumi.
Kupitia elimu hiyo, TBS inaendelea kusisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuwa mabalozi wa usalama na ubora wa bidhaa wanazouza, ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya biashara yanaenda sambamba na ulinzi wa afya za walaji na ustawi wa jamii.














