Na Mwandishi Wetu — Jamhuri Media
Dar es Salaam

Chama cha ACT Wazalendo kimeiomba Serikali kusitisha operesheni za kuwaondoa wafanyabiashara wadogo katika maeneo wanayofanyia biashara, kikisisitiza kuwa changamoto zinazohusishwa na shughuli zao zinapaswa kushughulikiwa kwa mipango shirikishi badala ya kuwaondoa katika maeneo yenye wateja.

Waziri Kivuli wa TAMISEMI na Maendeleo Vijijini wa ACT Wazalendo, Kulthumu Jumanne Mchuchuli, ametoa kauli hiyo Septemba 25, 2026, akisema changamoto zinazohusu msongamano, usafi, usalama na matumizi ya maeneo ya umma zinapaswa kutafutiwa ufumbuzi kwa kuwashirikisha wafanyabiashara hao.

Kwa mujibu wa ACT Wazalendo, tangu Rais Samia Suluhu Hassan kutoa maagizo Septemba 2, 2026 kwa wakuu wa mikoa kusimamia na kupanga shughuli za wafanyabiashara wadogo, kumekuwa na operesheni katika maeneo mbalimbali nchini.

Chama hicho kimesema baadhi ya operesheni hizo zimehusisha kuvunjwa kwa vibanda na meza, kuharibiwa kwa bidhaa pamoja na kukamatwa kwa wafanyabiashara.

ACT Wazalendo imetaja Dar es Salaam kuwa miongoni mwa maeneo ambako operesheni hizo zimefanyika, ikitaja Tandika, Buguruni, Gongo la Mboto, Ilala Boma, Kigamboni, Tegeta, Msasani na Mbagala.

Aidha, chama hicho kimesema Halmashauri ya Ubungo imetangaza operesheni ya kuwaondoa machinga kuanzia Septemba 29, 2026, huku Mwanza, Tanga, Mbeya na Kilimanjaro zikitajwa kuwa miongoni mwa mikoa ambako hatua kama hizo zimechukuliwa.

Kuhusu matukio ya moto katika masoko, ACT Wazalendo imetaja moto ulioteketeza zaidi ya vibanda 50 katika Machinga Complex Dodoma, Septemba 20, 2026, pamoja na matukio mengine yaliyotokea katika masoko ya Marangu mkoani Kilimanjaro na Mbao Saba Saba mkoani Mwanza.

Kuhusu suala la kodi, chama hicho kimesema madai kwamba baadhi ya machinga hawalipi kodi yanapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia mazingira halisi ya biashara ndogo, kikitaka Serikali kuweka mfumo rahisi wa kuwatambua na kuwasajili wafanyabiashara hao ili waweze kutekeleza wajibu wao wa kisheria.

ACT Wazalendo pia kimesisitiza kuwa mipango ya miji haipaswi kutumika kuwaondoa wafanyabiashara wadogo bila kuwapatia maeneo mbadala yenye wateja na mazingira yanayowezesha biashara zao kuendelea.

Chama hicho kimesema ongezeko la idadi ya wamachinga linahusishwa na changamoto za ajira na mazingira ya uchumi, hivyo Serikali inapaswa kushughulikia sababu hizo kwa kuongeza fursa za ajira na kuweka mazingira bora ya uzalishaji na biashara ndogo.

Kutokana na hali hiyo, ACT Wazalendo imeitaka Serikali kukaa na wafanyabiashara hao, kuwasikiliza na kupanga maeneo yanayoweza kuwawezesha kuendelea na shughuli zao badala ya kutumia operesheni za kuwaondoa.

Pia, chama hicho kimeitaka Serikali kuzuia matumizi ya askari na migambo katika kuvunja au kuchukua mitaji ya wafanyabiashara hao, kikieleza kuwa masuala hayo yanapaswa kushughulikiwa kwa njia za kiraia kupitia maafisa maendeleo na biashara.

Katika hatua nyingine, ACT Wazalendo imependekeza Bunge, kupitia Kamati ya Kudumu ya Serikali za Mitaa, kuchunguza matukio ya kuungua kwa masoko nchini na kuchukua hatua stahiki.

Mapendekezo mengine ya chama hicho ni Serikali kuanzisha masoko ya jioni katika miji na majiji nchini, pamoja na kuweka sheria na taratibu rasmi zitakazowapa wafanyabiashara wadogo hadhi na ulinzi wa kisheria katika shughuli zao.