Mashindano ya soka ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), yamehitimishwa Jumapili iliyopita huku Tanzania ikiwa mtazamaji na msikilizaji tu.

Mashindano hayo yamefanyika Afrika Kusini yakizihusisha nchi 16: Nigeria, Burkina Faso, Ghana, Mali, Afrika Kusini, Cape Verde, Angola, Morocco, Congo, Ethiopia, Niger, Ivory Coast, Togo, Tunisia, Algeria na Zambia iliyoshindwa kutetea kombe hilo.


Tumeshuhudia nchi zinazozidiwa na Tanzania kisoka zikifanya vizuri katika mashindano hayo ingawa hazikutwaa ubingwa.


Wiki iliyopita, Timu ya Taifa (Taifa Stars) ilionesha kiwango kikubwa cha soka kwa kuifunga timu ya Cameroon 1-0. Cameroon ni ya pili kwa kutwaa ubingwa wa AFCON mara nyingi zaidi baada ya Misri.

Mchuano huo ni kipimo kwamba Taifa Stars ina uwezo wa kuhimili AFCON na mashindano mengineyo, ikaibuka na matokeo mazuri.


Matumaini ya Watanzania ni kwamba ahadi ya Serikali ya kushirikiana na Kocha Kim Poulsen wa Taifa Stars kuhakikisha Tanzania inafuzu kucheza AFCON mwaka 2015 itatekelezwa kwa vitendo kufanikisha shabaha hiyo.


Watanzania wangependa kuona Serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaitazama dosari ya kutoshiriki AFCON mwaka huu kama changamoto ya kuimarisha Taifa Stars iweze kushiriki mwaka 2015.


Taifa Stars ikiwezeshwa ipasavyo inaweza kutwaa ubingwa wa AFCON kama ilivyo mazoea kwa nchi za Misri, Cameroon, Gahana na Nigeria. Inawezekana.


By Jamhuri