N

awaza sana na huwa naona ni kama hadithi au ndoto iliyoisha muda wake, naona kama kumekucha ni asubuhi na mapema najinyoosha kitandani, ni ndoto mfu, ndoto ya mchana nikiwa macho natembea, ndoto ya kweli lakini alinacha, kuna uhalisia zaidi japokuwa kuigiza kumetamalaki,  sasa nahisi ni mchezo wa kuigiza ambao sisi ni wacheza sinema na waangalia sinema pia.

Nawaza jinsi miaka michache tulivyokuwa na idadi ndogo ya magereza kwa ajili ya wahalifu, wahalifu walikuwa wakitafutwa kwa shida sana, walikuwa kama maadui wa maendeleo, ni miaka michache ambapo ukimuona  mwizi ni kama umemuona jini, tuliwachukia wahalifu sana, tuliwachukia sana wavivu katika jamii, tuliwachukia  wasio wazalendo, wasiopenda taifa lao, ni juzi tu kama naota.

Nawaza miaka michache jinsi ambavyo tarafa nyingi hapa nchini zilivyokuwa zikimiliki mabasi ya usafiri kutoka tarafani, maroli ya kubebea bidhaa  na matrekta ya vijiji,  mabohari na dispensari katika tarafa nyingi, nawaza mpango mzuri wa sogeza huduma  muhimu za jamii miaka ya sabini na kilimo cha kufa na kupona ili kuondokana na umaskini.

Ni ndoto ya mchana kweupe kuona utu umepotea, uzalendo haupo tena, rushwa imetamalaki na kuwa uti wa mgongo, na kilimo siyo uti wa mgongo tena ila biashara na fedha ni kila kitu katika uchumi wa taifa letu, ni kama ndoto kuona suala la ufugaji halipo tena midomoni mwa viongozi wa maeneo yetu, ndoto tu kuwasahau mabwana shamba na mabibi mifugo.

Nawaza hii ndoto ya mabasi ya viwanda na makampuni kwa ajili ya wafanyakazi hapa nchini, nawaza viwanda hivyo na ule usafiri ambao ulikuwa umeficha dhana ya foleni katika miji mikubwa, naoana ni maendeleo ya kijinga kwa upande wangu, yako wapi mabasi yetu, wapi utumishi uliotukuka, wapi uzalendo, hii ni ndoto ya alinacha na mchana kweupe.

Nawaza simu za kukoroga na mipango iliyothabiti wakati huo, nawaza miadi na kwenda na wakati, naona ni ndoto ya ajabu, naona kila mtu na simu mkononi na mipango isiyothabiti, uongo mwingi na kutozingatia miadi, naona ndoto ya maisha ya kweli enzi hizo na kuiona hii ni sinema ni juzi tu kwa mabadiliko makubwa ya ajabu.

Ni ndoto kuamini kuwa sasa hivi kila kitu ni fedha, haki inapatikana kwa fedha, huduma zote muhimu kwa jamii ni fedha kwanza, elimu ndio bidhaa aghali zaidi katika miaka ya hivi karibuni, ni kama ndoto kuona Mtanzania anakufa kwa ugonjwa kwa kukosa fedha, anakufa mbele ya daktari wa kitanzania, ni ndoto kuamini kuwa ule utu na uzalendo tuliokuwa nao  jana ya usiku wa ndoto  leo umepotea, maisha ni safari fupi sana.

Naota ndoto ya ajabu ya mchana kweupe kuona tanzania ninayoijua mimi haina bidhaa yoyote iliyozalisha yenyewe na kujidai nayo katika soko la kimataifa kama zamani, leo tanzania ile ninayoijua mimi inajivunia udalali wa kujaza mali za nje ya nchi na kurithi utamaduni wa nje ndani ya ardhi ambayo juzi tu tulikuwa tukikataa kutawaliwa kifikra na utamaduni.

Kimejaa chakula cha ulaya, hatulimi tena mazao yetu, kweli ni ndoto, siamini ninavyoona baadhi yetu wakitumia nyanya za ulaya, tukitumia unga wa ulaya, mboga za ulaya, maji ya ulaya, nguo za ulaya, dawa za ulaya, pombe za ulaya, umeme wa ulaya na kila kitu cha ulaya, tanzania yetu niliyolala nayo jana leo ni koloni la kila kitu cha ulaya. Hii ni ndoto mbaya sana lakini sina budi kuikubali ni yetu na ndimo tunamoishi.

Hivi ile Tanzania yangu ya maadili iko wapi, Tanzania ya shikamoo mzee, mzee nikupokee mzigo, ulinzi wa pamoja kiuzalendo, Tanzania ya utu, Tanzania ya kilimo uti wa mgongo, Tanzania ya ufugaji na uvuvi, tanzania ya fedha siyo msingi wa maendeleo, kweli naota ndoto ya mchana lakini ni kweli kwamba Tanzania ile imekwisha kuna Tanzania mpya.

Nitaendelea kuota ndoto japo nipo macho nadhani nahitaji kuamushwa na kiongozi wa hapa kazi tu ili ile jana ya kweli irudi na iwe ya Watanzania.

 

Wasaalam

Mzee Zuzu

Kipatimo.

By Jamhuri