Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kwa kushirikiana na wakufunzi kutoka taasisi ya Uongozi,  Mafunzo ya Uongozi, kwa viongozi wa vyama vya wanafunzi wa vyuo kadhaa hapa nchini wanaosomea fani ya ununuzi na ugavi.

Mafunzo hayo ya siku moja yamefanyika Dar es Salaam katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kwa kuwakutanisha viongozi wataalamu 35, wenye taaluma ya ununuzi na ugavi na wanafunzi kutoka vyuo vinane hapa nchini vinavyofundisha kozi ya ununuzi na ugavi.

Akizungumza katika hitimisho la mafunzo hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Godfrey Mbanyi, amesema mafunzo ya uongozi kwa vijana viongozi kwenye vyama ama klabu za fani ya ununuzi na ugavi ni muhimu na yamekuja kwa wakati mwafaka.

“Kiongozi lazima ajihakikishie utimilifu katika akili yake, mwili wake na roho pia iwe tayari kufanya mambo anayotakiwa kuyatekeleza. Tunawafundisha kuwa kiongozi mzuri ni yule mwenye uwezo wa kuhimili vishindo, kiongozi anatakiwa kuleta suluhu ya matatizo yanayokabili taasisi anayoiongoza,” amesema Mbanyi.

Amesema mafunzo ya uongozi na maadili wamekuwa wakiyatoa kwa wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani ya kitaalamu kwa kufuata mtaala wa Bodi, huku mafunzo hayo yakiendelea kutolewa kwa wanataaluma ambao tayari wapo kazini.

“Ni muhimu sana kwa kiongozi yeyote kuzingatia maadili katika utendaji wake. Iwapo kiongozi husika hatakuwa na maadili wala misingi ya utawala bora anaweza kutumia madaraka yake isivyo na hivyo kusababisha matatizo katika taasisi anayoiongoza,” amesema Mbanyi.

Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo wa Bodi hiyo, Amani Ngonyani, amesema bodi ya wataalamu wa ununuzi na ugavi imeona kuna umuhimu mkubwa wa kuendesha mafunzo ya uongozi kwa viongozi hao.

Amesema viongozi hao baada ya kupata mafunzo  wanatarajiwa kuifikisha kikamilifu elimu hiyo kwa wanafunzi wenzao wanaowaongoza huko vyuoni.

“Mafunzo haya ni ya kuwajengea uwezo, kuwafanya kuwa na maono na tabia za kiuongozi. Tunawajengea stadi za uongozi ikiwa ni pamoja na kutengeneza timu nzuri ya watu unaofanya nao kazi. 

“Watakapotakiwa kutoa michango katika vikao vya maamuzi (uamuzi) wawe weledi. Mafunzo haya ni endelevu yakilenga kuandaa viongozi mahiri katika fani hii. Tunahitaji viongozi wenye uwezo wa kujenga hoja zenye kuleta mafanikio ya kiutendaji,” amesema Ngonyani.

Amesema marekebisho ya sheria ya manunuzi ya mwaka 2011 yaliyofanyika mwaka 2016 yametoa fursa ya kwa wataalamu wa fani ya ununuzi na ugavi kuteuliwa kushika nafasi nyeti za juu katika mashirika kama ukurugenzi, umeneja na ukuu wa vitengo vya ununuzi na ugavi.  

“Hapo awali hatukuwa na wakurugenzi wala mameneja ambao wangeweza kutoa mawazo yao katika masuala ya manunuzi. Shughuli zilikuwa zikisimamiwa na watu wa kada tofauti mathalani wahasibu na kadhalika. Sasa hivi nafasi hizi zinakwenda kwa wataalamu wenyewe ambapo wanakuwa ni sehemu ya wafanya maamuzi (uamuzi) yanayofikiwa katika masuala ya ununuzi,” amesema Ngonyani.

Mtaalamu wa mafunzo ya uongozi kutoka katika taasisi ya Kazi Services Limited, Zuhura Muro, amewaeleza viongozi hao wa wanafunzi kuwa sifa ya uongozi ni pamoja na kuwa na uwezo mzuri wa kufurahia mafanikio ya unaowangoza kiutendaji.

“Kiongozi mzuri ni yule anayependa kutendea walioko chini yake yale anayopenda wao wamtendee. Mpe mfanyakazi wako sifa anayostahili kupewa kulingana na alichokitenda. Hii humpa ari zaidi ya kujituma na kuwa mwaminifu.

“Akitambua kuwa mchango wake na uwepo wake katika taasisi husika ni muhimu…hizi ni mbinu muhimu sana kwa kiongozi kujenga mtandao mzuri wa kiutendaji,” amesema Muro.

Amesema kujenga mtandao wa kitendaji wala hauhitaji kuwekeza fedha nyingi. Ni suala la namna unavyoishi na unaowaongoza na ukaribu unaoujenga baina yako na taasisi nyingine.

 “Katika uongozi usimuonee mtu ili wewe ufanikishe malengo yako. Kumkanyaga mtu ili ufike unapopataka huharibu mtandao mzima wa utendaji wako. Kiongozi ni mtu mwenye ushawishi katika jamii na miongoni mwa watu anaowaongoza,” amesema Muro.

Amesema uzembe wa kitendaji hautakiwi katika uongozi, watu wanahitaji kujifunza kutoka kwa kiongozi wao, kiongozi ni lazima ajue kuongoza watu kulingana na nyakati.

Amewaeleza viongozi hao wa wanafunzi kuwa kiongozi hatakiwi kuwa na majivuno na kiburi cha kuona kwamba mawazo yake ni sahihi muda wote kuliko ya wengine. Amesema kiongozi mzuri ni yule anayeshirikisha mawazo ya watu wengine na kisha kuyachuja kwa kutumia hekima za kiuongozi.

Katibu Mkuu wa chama ya wanafunzi wa fani ya ununuzi na ugavi kutoka CBE,  John Lelo, amesema mafunzo hayo yamekuwa ni chachu kwake na washiriki wenzake kwani yamewaleta katika mtazamo mpya wa kwamba kiongozi ni mtumishi wa anaowaongoza.

“Mafunzo haya yamenijenga kujua niweje nitakapobahatika kuendelea kuwa kiongozi hata baada ya hapa. Nafikiri hata wenzangu pia wamejifunza mengi. Nimejifunza kiongozi anatakiwa awe na mwonekano gani, aseme nini kwa wakati gani na mahala gani, awe mtu mwenye uthubutu, mzalendo na msikivu kwa watu wa kada zote,” amesema Lelo.

Bodi ya wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) ni taasisi ya Serikali iliyoundwa kwa Sheria ya Bunge Na. 23 ya mwaka 2007. Bodi hii ina wajibu wa kulea fani ya Ununuzi na Ugavi nchini pasipokuwa na mipaka. 

Bodi hiyo ina mamlaka ya kutoa mitihani na vyeti kwa watu wanaosomea fani ya Ununuzi na Ugavi na kisha kuwasajili ili wafanye kazi za ununuzi na ugavi nchini.

2288 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!