Yasiyosemwa Ngorongoro

Ngorongoro

Na Mwandihi Wetu

Muda ni saa 4 asubuhi, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala, wakiwa na viongozi mbalimbali wa vyombo vya ulinzi na usalama wanaelekea katika Kijiji cha Kimba kilichoko ndani ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA).

Kwa kuwa ni mara ya kwanza kufika eneo hili, tukiwa njiani naingiwa woga na hofu kudhuliwa. Taarifa zinazosambaa kwenye vyombo vya habari, hasa mitandao ya kijamii zinanifanya nikose amani. Picha niliyonayo kichwani mwangu ni ya mapambano, majeruhi, na pengine hata umwagaji damu.

Lakini najiuliza, endapo kuna vurugu zinazodaiwa kuanzishwa na vyombo vya dola vinavyowahamisha kwa nguvu wenyeji wa Ngorongoro, mbona sioni tukiwa na askari wenye mitutu ya bunduki ya kuashiria shari? Najipa moyo. Tunafika katika lango kuu la kuingia Ngorongoro – hapa ni Loduale. Nastaajabu kuona makumi ya magari ya watalii yenye mamia ya watalii wanaoingia Ngorongoro na wengine wakiendelea hadi Serengeti. Wingi huu wa wageni wasioonyesha hofu yoyote nao unanipa matumaini ya kwamba tuendako hali si mbaya kama ulimwengu unavyohadaiwa.

Tunaendelea na safari na hatimaye tunafika juu kabisa mahali ambako ukisimama unaiona kreta, na hapo kwetu wengine tunaopenda masuala ya asili kama haya huwa hatukosi kuusifu uumbaji uliofanywa na Mwenyezi Mungu.

Kutoka hapa msafara wetu unakwenda moja kwa moja na kupita mahali ambako awali kulikuwa makao makuu ya NCAA, lakini baada ya kuwapo mpango wa kupunguza shughuli za kibinadamu hifadhini, uongozi wa mamlaka ukawa wa kwanza kuhamisha ofisi zake kwenda Karatu.

Tunafika mbele kidogo. Kulia kuna uwanja wa ndege, na kushoto kuna vilima vifupi ambavyo nakumbuka tukipita hapa kwenda likizo mkoani Mara, tulifaidi mandhari nzuri iliyopambwa kwa pundamilia, nyati na nyumbu. Hali ni tofauti kabisa leo. Ninachoona ni punda vihongwe, ng’ombe waliodhoofu, makundi makubwa ya mbuzi na kondoo. 

Hakuna pundamilia wala nyumbu ambao zama zile ndege ikitaka kutua ilianza kuwatisha kwanza kwa kupita karibu na ardhi ili wasambae, hivyo rubani aweze kushusha ndege. Ngorongoro imebadilika.

Kutoka hapa tunaacha kushoto njia inayoelekea Endulen hadi Meatu; tunapinda kulia na mita chache tunaingia kushoto katika Kijiji cha Kimba. Hapa ni miongoni mwa maeneo ya awali kabisa yaliyotumiwa na baadhi ya wananchi walioishi Ngorongoro.

Msafara wa mkuu wa mkoa unalakiwa na wakazi kadhaa wa eneo hili waliomwita kiongozi huyo kumuonyesha kwa vitendo dhamira yao ya kuihama Ngorongoro. Wakati mkuu wa mkoa akiendelea na itifaki yake, mimi nikawa nauliza wananchi ni kwa namna gani wamepokea mwito wa kuhama kwa hiari ndani ya hifadhi. Mama mmoja niliyeanza kumuuliza ananieleza kitu ambacho sikukitarajia, anasema: “Nashangaa mnakuja kutuuliza wakati sisi wengine tunataka hata kuondoka kwa miguu kwenda Msomera.” 

Namuuliza, kwa nini amefikia uamuzi huo. Anajibu: “Jana tumetoka Msomera kupaona, ni pazuri mno. Walituahidi pia fidia, tukadhani ni ya kawaida, lakini Mama (Rais Samia) ameamua kutuwekea na cha juu, hatukuamini ndiyo maana sisi hata mkitaka sasa hivi tunaondoka.”

Basi, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Mangwala, anaanza kuzungumza na wananchi. Anawahakikishia kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha na timu yake yote wamefika kuitikia wito wa wananchi wa kaya 21 waliokubali kuhama Ngorongoro kwa hiari yao kwenda kuanza maisha mapya Msomera, Handeni.

“Watu wanatangaza uongo kwamba Ngorongoro kuna watu wanahamishwa kwa nguvu, mmeona nguvu zozote hapa? Nani anayehamishwa kwa shuruti? Nawahimiza wananchi walio tayari kuhama wafanye hivyo wenyewe kwa hiari yao,” anasema.

Anamkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mongella, naye anaanza kulaani kauli za uchochezi zinazoenezwa na watu anaowaita kuwa ni maadui wa taifa.

“Wanasema wananchi wanaondolewa kwa nguvu, huu ni uzushi. Sisi tunaomsaidia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, mara zote ametuhimiza tufanye kazi zetu kwa utu. Hakuna mwananchi anaondolewa Ngorongoro kwa nguvu. Au yupo hapa aliyeshurutishwa kuondoka? (hakuna).”

Mongela anaendelea kusema: “Watu wanasema Loliondo kuna vurugu, waziri mkuu alishatoa kauli ya serikali na ukweli unabaki huo huo kwamba Loliondo hakuna vurugu, bali kilitokea kikundi cha watu waliochochewa kikafanya vurugu na kumuua askari polisi wetu mmoja.

“Kuna uongo mwingi unasambazwa kwamba Loliondo kuna watu wanaondolewa, eti Ngorongoro nako watu wanaondolewa kwa nguvu. Naomba Watanzania wapuuze uzushi huu.

“Wengine wanachanganya haya maeneo mawili – Ngorongoro na Loliondo. Haya ni maeneo mawili tofauti na mazoezi yake ni tofauti. Kutoka hapa Ngorongoro hadi Loliondo ni kilometa zaidi ya 200.

“Ngorongoro kinachoendelea ni serikali kusimamia shughuli ya kuondoa watu waliojitokeza wenyewe kwa hiari ili kupunguza idadi ya watu na mifugo maana tafiti zote zimeonyesha umuhimu wa kufanya hivyo.

“Rais Samia amesema hawaondoki hivi hivi, bali wanapewa fidia, wanapewa nyumba zenye hati, ekari 3 za eneo la nyumba na ekari 5 za shamba. Wanasafirishiwa mifugo na vifaa vyao vya ndani. Kule wanakokwenda kuna shule, zahanati, maji, umeme na huduma za majosho na malisho. Tayari kaya 21 zenye watu takriban 300 zimeshajitokeza kwa hiari na wengine jana wametoka Msomera kuona hali ilivyo.

“Loliondo hakuna mwananchi anayeondolewa, bali serikali imeamua kupunguza kilometa za mraba kutoka 4,000 za Pori Tengefu hadi kilometa za mraba 1,500. Hizo 2,500 wanapewa wanavijiji wazitumie kadiri wanavyotaka. Sasa kuna uzushi kwamba watu wanaondolewa, si kweli. Kinachofanyika ni kuweka ‘beacons’ (vigingi) ili eneo hilo litambulike kwa sababu ni muhimu sana kwa ikolojia – Ndilo linalolinda Ngorongoro, Serengeti hadi Maasai Mara.”

Baada ya maneno haya ya Mongela, baadhi ya wananchi waliojitokeza kwa hiari kuhamia Msomera wanaanza kubomoa nyumba zao kwa hiari, na pale walioshindwa wakaomba Mongela awasaidie njia ya kuzibomoa ili zisije zikakaliwa na watu wengine.

“Sisi wananchi wa Ngorongoro tuliojiandikisha kwa hiari kuhamia Msomera ni sawa na kufika kwenye nchi ya maziwa na asali, tunakwenda kumiliki nyumba na eneo lenye ukubwa wa ekari tatu – achilia mbali hilo, tumepewa fidia nono na kwa mara ya kwanza tangu kuzaliwa nina uwezo wa kukopa benki yoyote kwa sababu nina hati miliki ya ardhi,” anasema Lemula Ngalioi.

Kuona hivyo, Anna Didia naye akasogea mbele ya mkuu wa mkoa na kusema: “Tunaishukuru sana serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa sababu tumepekekwa Msomera tumeona nyumba, mashamba pamoja na miundombinu yote ya kijamii ikiwa imekamilika, tumeridhika sana, hivyo tupo tayari kuhamia Msomera ambako sisi wafugaji ni mahali pazuri kwa ajili ya kulishia mifugo yetu.”

Mkazi mwingine Masiaya Parakoi, akasema: “Mimi kwangu kuhamia Msomera ni fursa kubwa, nawasihi na wenzangu twende kule tukatafute maisha. Tukiendelea kung’ang’ania kubaki hapa kwa kujidanganya kuwa ardhi ni yetu huko mbele watoto wetu watapata shida, hivyo ni lazima tukubali hii ni ardhi kwa ajili ya shughuli za uhifadhi.”

Samwel Huho ambaye ni Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Kimba, akiwa ameshika nyundo mkononi tayari kuanza kubomoa nyumba yake ili asubuhi aanze safari, anasema: “Nimeamua mimi mwenyewe kwa hiari yangu kujiandikisha tayari kwenda Msomera kuanza maisha mapya na hapa nilipo nabomoa jengo langu nakwenda kuanza maisha mapya huko Handeni ambako vizazi vyangu vitakuwa na haki ya kumiliki ardhi kama ilivyo kwa Watanzania wengine.

“Tayari nimetoa vitu vyangu vyote sasa naiomba serikali isaidie kubomoa maeneo niliyoshindwa kubomoa kwa sababu nataka nipaache hapa peupe, watu wasivamie na kufanya makazi tena.”

Hamasa ni kubwa, kitendo hiki cha wananchi kuonyesha furaha ya kwenda Msomera kinawafanya baadhi waanze kumzonga mkuu wa mkoa na wasaidizi wake wakitaka nao waandikishwe tayari kwenda Msomera.

Mongella anawageukia na kusema: “Jamani, leo tunashughulika na zile kaya 21 zilizokwisha kujiandikisha, kama wewe unataka kawaone viongozi akiwamo katibu tarafa ili muandaliwe kwa awamu zinazokuja.”

Kutoka hapa Kimba tunakwenda Kijiji cha Mokilal, na kumkuta Richard Sane, mkewe na watoto wake wawili. Tayari nyumba moja wameshaanza kuibomoa mwenyewe, ikiwa ni maandalizi ya kwenda Handeni kuanza maisha mazuri yenye amani na furaha.

“Maisha ya hapa hayana uhakika na ukitaka kujenga mpaka kibali tena kwa masharti, sasa hayo ni maisha gani? Ninatoka eneo duni kwenda eneo bora zaidi. Kule nina nyumba nzuri niliyojengewa na serikali, shamba la kulima na kuna huduma zote za kijamii, nawashukuru viongozi wa serikali kuanzia Mheshimiwa Rais Samia, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu na watendaji wote kwa kututhamini sisi tulioamua kuondoka kwa hiari. Kuondoka kwetu ni faida kwa taifa, maana mazingira ya hifadhi yatalindwa na kuleta manufaa kwa taifa.”

Muda ni jioni, mkuu wa mkoa anaambiwa kiza kinaingia kwa hiyo ni vema akarejea kwenye makazi yake, lakini yeye anagoma na kutaka awafikie wananchi wengi zaidi wanaotaka kuondoka kwa hiari.

Kwa maana hiyo anaelekeza msafara uende Kijiji cha Endulen. Hapa anamkuta Gagi Didia akiwa ameanza kubomoa nyumba yake mwenyewe.

Anasema awali alikuwa anahofu kuhama, lakini baada ya kijana wake kumshauri alikubali kwenda Msomera kuliona eneo.

“Kijana wangu aliyemaliza chuo kikuu ndiye aliniambaia nisichezee bahati kwani kule tutakuwa na makazi ya kudumu maana hapa ni eneo la hifadhi na hatuna mamlaka nalo na hata ukitaka kujenga unaomba vibali, sasa ya nini kuishi kwa wasiwasi wakati kumbe kuna maisha mazuri huko Handeni,” anasema Gagi.

Hatimaye muda wa kurejea kwenye makazi umewadia, lakini kabla ya hapo mkuu wa mkoa anatoa maelekezo kwamba wananchi hao zaidi ya 100 waandaliwe sehemu nzuri za kulala mjini Karatu ili asubuhi zifanyike taratibu za kuwakabidhi baadhi ya nyaraka muhimu za malipo yao ya fidia na mambo mengine muhimu ya kuwahusu.

Naam, muda ni asubuhi. Watu ni wengi katika eneo hili la Makao Makuu ya NCCA nje kidogo ya Mji wa Karatu. Magari ya abiria aina Double Coaster sita hivi – yenye viyoyozi na vitambaa vyeupe ndani yapo hapa tayari kuwapeleka wananchi hawa Msomera. Baada ya kifungua kinywa na makabidhiano ya nyaraka, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mongella; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro na viongozi wengine, wanatoka nje ya lango kuu na kuashiria kuanza rasmi kwa safari ya kundi la kwanza la wananchi wa Ngorongoro wanaohamia kwa hiari Msomera, Handeni mkoani Tanga.

Mongella anawaaga wananchi hawa kwa hisia kali: “Siku hii itakuwa ni leo tu nyingine zitakuwa tofauti. Pili, nimshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa imani yake na sisi kwa umoja wetu kutuamini viongozi wa mkoa, wilaya, wizara, Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro… viongozi wa kimila na jamii nzima na nisiwasahau kabisa wanahabari tusiposema kwamba kwa baraka za Rais leo tunaweka historia hii tutakuwa hatundeki haki lazima tumshukuru sana kwa hilo.

“Niwashukuru sana wananchi kwa ujumla wao wote, hawa ndugu zetu leo wanaondoka na wale ambao bado, lakini wamejiandikisha na ambao hawajajiandikisha wote wana mchango wao kwenye kufanikisha hili.

“Niseme tu Mwenyezi Mungu katubariki hili limefanikiwa na mnajua wengine hatujakaa muda mrefu ni kama mwaka mmoja na ushei, lakini jambo hili lina miaka mingi na mjadala wake ni wa miaka mingi, kuna mafaili na mafaili yamejaa, kila aina ya ushauri wa kitaalamu na wa kawaida umetolewa mpaka leo tumefika hapa.

“Niseme zoezi hili la wananchi wa Ngorongoro kwa fursa hii iliyotolewa na serikali ambayo wana hiari na kwa dhamira zao za dhati binafsi na kwa familia zao. Je, kuna mtu kasukumwa au kalazimishwa? Kama kuna mtu kalazimishwa au kashurutishwa, basi aseme (hakuna).

“Kwa sababu Rais Samia Hassan katika muongozo wake kila siku kwa viongozi na watendaji wa serikali lisifanyike jambo lolote la shuruti, kusukuma, la lazima na wananchi lazima waelewe chema ambacho serikali inawatakia, kwa hiyo naomba ieleweke kwa sababu kuna upotoshaji mkubwa unatokea.

“Kuna neno linatumika la Kiingereza na wakati mwingine linatumika ili kuficha maana ya lile neno. Kuna neno linatumika linaitwa ‘EVICTION’ ambayo maana yake ni kuondolewa. Tafsiri yake si sahihi kutumika katika hili. Nadhani tutumie tafsiri ya Kiswahili, haya maneno mengine yatatupotosha, hakuna kuondolewa hapa.

“Kila mtu anatoka kwa hiari na kwa ridhaa na ambao wamejiandikisha wapo takriban kaya 290 na wameanza na kaya 20. Wiki ijayo kuna wengine wataondoka, serikali imeelekeza lazima uondokaji wao uwe wa staha, kibinadamu na heshima inayostahili kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.

“Na ndiyo maana hata mchakato wenyewe wa kuondoka inabidi tuupeleke kwa utaratibu na kufuata sheria zote za nchi na mimi nataka kusema kama kuna mtu amenyanyasika aseme. Na sisi tunaahidi tutafuata sheria, taratibu na haki zote ambazo mwananchi anastahili na yeyote yule ambaye ataonekana kutaka kwenda kinyume tutamshughulikia kwa mujibu wa sheria na taratibu hizo hizo za nchi yetu.”

Wananchi hawa wanapewa muda wa kuzungumza, lakini mmoja aitwaye Paulina Bajuta, anatia fora, akisema: “Namshukuru sana Rais Samia, sina cha kumpa, sina cha kumwambia, lakini naomba niseme kwa upendo huu wa Rais Samia mtoto wangu nimeamua kukata jina lake na sasa anaitwa Samia.”

Mbele ya mabasi haya kuna gari maalumu la kuongoza msafara, na nyuma lipo gari la kuhakikisha usalama wao ikiwa ni pamoja na gari la dharura ya matibabu.

Dakika kadhaa baada ya mabasi haya kuondoka, sasa ni zamu ya malori zaidi ya 10 yaliyobeba vifaa vya ndani, mbuzi, ng’ombe, kuku, punda na kadhalika. Wananchi waliojitokeza hapa wanawapungia mikono kwa shangwe.

Msafara wawasili Msomera

Muda ni alasiri, msafara wa kwanza wa wananchi hawa wakazi, unawasili Msomera. Hapa unalakiwa na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Tanga, Wilaya ya Handeni, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Pindi Chana, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ridhiwan Kikwete, na wengine wengi. Shangwe zimetawala kila mahali.

Baada ya makaribisho haya makubwa, sasa ni zamu ya viongozi kuzungumza. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Chana anawapongeza waratibu wote na wananchi wa Ngorogoro walioamua kwa hiari yao wenyewe kuhamia Msomera.

“Tunamshuku Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wetu wa Rais, Mheshimiwa Dk. Philip Mpango, pamona na Waziri Mkuu wetu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa kwa kutuongoza vema kwenye jambo hili, limekwenda vizuri na linakwenda vizuri kwa wana Ngorongoro wenyewe kuhama kwa hiari.

“Sisi kama wizara tutaendelea kutekeleza maagizo ya viongozi wetu wa juu ili kuhakikisha ndugu zetu wanaishi kwenye mazingira bora kama mlivyoyaona hapa,” anasema Dk. Chana. 

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima, anasema wanachi hao wapo salama na wataendelea kuwa salama wao na mifugo yao, hivyo serikali ya mkoa imejipanga vema kuwahudumia vizuri, kwa kuwa wameshakuwa wakazi wa Tanga.

Naye, Waziri wa Maji, Juma Aweso, anasema miradi ya maji imeshafanyika na wanaendelea kuhakikisha hakutakuwapo changamoto yoyote ya maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo.

Laigwanani atoa ya moyoni

Mkuu wa Kimila wa kabila la Wamasai waliokuwa wakiishi katika Hifadhi ya Ngorogoro, Laigwanani Matigoi Tauwo, anamshukuru Mungu kwa kumuongoza Rais Samia kwa maono yake ya kuwapatia makazi bora.

Kwa niaba ya wananchi wenzake, Laigwanani Tauwo, anasema sasa maisha yao yatakuwa ya amani zaidi na yenye maendeleo kuliko huko nyuma kwa kuwa serikali imewapatia nyumba, ardhi kwa ajili ya kilimo na ufugaji; huduma bora za kijamii (elimu, maji na afya).

“Namshukuru sana Mungu kwa kutupa Rais Mama Samia, leo sisi tunamiliki nyumba jamani, kweli Mungu mkubwa sana, tunaahidi tutaishi vizuri sana na ndugu zetu wa hapa Msomera,” anasema Laigwanani Tauwo.

Pembeni naitwa na kiongozi mmoja wa serikali wilayani Ngorongoro. Ananiuma sikio: “Nakuambia idadi ya watu wanaotaka kuja Msomera imeongezeka. Tayari tunao wengine 300 hivi. Wengine wameanza kuvunja nyumba zao wenyewe. Wananchi wamehamasika sana.”

Hii ndiyo hali halisi ya wananchi wanaohama kwa hiari kutoka Ngorongoro. Hakuna matumizi ya nguvu wala shuruti. Hali ni tofauti kabisa na taarifa za kwenye mitandao kwamba wananchi wanahamishwa kwa nguvu.

Kwanini Ngorongoro?

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwenye ripoti zake tano kuanzia mwaka 2007 na ya karibuni kabisa ikiwa ni ya mwaka mwaka jana, zinaeleza hatari inayoikabili Ngorongoro kutokana na wingi wa binadamu na mifugo.

Shirika hilo baada ya kuona hali mbaya ya Ngorongoro, limesema: “UNESCO kwa ujumla wake imeshauri yafanyike mapitio ya mfumo wa matumizi mseto ya ardhi ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro ambao kwa sasa umebainika kushindwa kufanya kazi ipasavyo; na kuhamasisha uhamaji wa wenyeji kutoka eneo la Hifadhi kwa kutoa motisha kwa wenyeji ili waweze kuhama. Aidha, inashauri kuhamisha wafanyakazi wa taasisi ya NCAA na wafanyakazi wa mahoteli ili waishi nje ya eneo la hifadhi.”

Mwaka 1979, Ngorongoro ilitangazwa kuwa Eneo la Urithi wa Dunia. Eneo la Urithi wa Dunia ni eneo lenye ulinzi wa kisheria na mkataba wa kimataifa unaosimamiwa na UNESCO. Maeneo ya Urithi wa Dunia yameteuliwa na UNESCO kwa kuwa na umuhimu wa kitamaduni, kihistoria ama kisayansi.

Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro lilianzishwa mwaka 1959 kama eneo la majaribio ya matumizi mchanganyiko ya ardhi, huku wanyamapori wakiishi pamoja na wafugaji (Wahadzabe, Wadatoga, Waamasai). Mwaka 2010 UNESCO iliiorodhesha NCA kama eneo mseto kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia.

Hifadhi ya Ngorongoro

Hifadhi ya Ngorongoro imekumbana na changamoto ya uharibifu wa mazingira tangu kuanzishwa kwake mwaka 1959 kunakosababishwa na ongezeko la watu.

Taarifa ya sensa ya watu na wanyama wafugwao ya mwaka 2017 iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ilionyesha kuwa idadi ya watu wakati huo katika eneo la Hifadhi ya Ngorongoro ilikuwa zaidi ya 90,000 ikilinganishwa na idadi ya wenyeji 8,000 wakati wa kuanzishwa kwa hifadhi hiyo mwaka 1959.

Taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali inasema idadi ya wanyama wafugwao inakadiriwa kuwa ni 799,462 ikilinganishwa na idadi ya wanyama wafugwao 261,723 waliokuwapo wakati wa kuanzisha hifadhi. Katika eneo la hifadhi, wanyama wafugwao wanashindana na kugombania malisho na wanyamapori.

Vilevile ongezeko la wenyeji pamoja na wanyama wafugwao linaongeza shughuli za kibinadamu zinazochangia uharibifu wa mazingira.