Mkuu wa Gereza kortini kwa mauaji 

*Afikishwa pamoja na askari magereza wawili

*Akiwa mahabusu anatumia simu kutoa maelekezo ya kikazi 

Na Mwandishi Wetu

Dar es Salaam

Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Liwale, Gilbert Sindani na askari magereza wawili; Sajenti Yusuph Selemani na Koplo Fadhili Mafowadi wamefikishwa mahakamani mkoani Lindi kwa tuhuma za mauaji ya mfungwa.

Watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani hivi karibuni baada ya Gazeti la JAMHURI kuripoti wiki iliyopita kifo cha mfungwa Abdallah Ngatumbara ambaye pia ni mnyampala mwenye namba 70/2020 kilichotokea Juni 8, 2022 na mwenzake Siaba Mbonjola mwenye namba 76/2021 amejeruhiwa kwa kipigo wakilazimishwa kuwataja askari magereza walioiba mahindi ya Sindani.

Kwa sasa Sindani yumo mahabusu katika Gereza la Mkoa wa Lindi lakini pamoja na hatua hiyo taarifa za uhakika zinadai akiwa huko anatumia simu ya mkononi kuwasiliana na watu walioko nje.

“Hakuna sheria inayoruhusu mtuhumiwa aliyeko mahabusu kukaa na simu au mawasiliano ya aina yoyote, wala kufanya mawasiliano ya simu na watu walio nje ya gereza bila kibali cha bwana jela.

“Hili linafanyika kwa Sindani, ameingia na simu mahabusu, anaitumia kuwasiliana na watu. Tunajiuliza jeuri ya kumiliki simu akiwa mahabusu anaitoa wapi? Ipo shaka kwamba huenda anatumia simu hiyo kuwasiliana na vigogo wanaosadikiwa kuwa karibu yake ili wamsaidie kujinasua katika kesi hiyo,” amesema mtoa taarifa wetu hivi karibuni.

Juni 26, 2022, Mkuu wa Gereza la Mkoa wa Lindi, Fadhili Donile, amezungumza na JAMHURI na kukiri Sindani kufanya mawasiliano ya kiofisi baina yake na anayekaimu nafasi ya Mkuu wa Gereza la Liwale kwa ajili ya kumpa maelekezo.

“Sindani naye ni mfungwa kama wafungwa wengine, haijalishi ni convicted au ni un convicted. Naye tunamsikiliza kama

tunavyowasikiliza wengine.

“Siku analetwa hakujua kama hatarudi tena, tulimpatia simu awasiliane na ndugu zake, hii haki ya kuwasiliana na ndugu si kwake tu ni kwa hata wafungwa wenzake, hata wao tuliwaruhusu kuwasiliana na ndugu zao na kuwapa taarifa kuhusu walipo na namna ya kuwatunzia mali zao,” amesema.

Donile anasema suala la Sindani kufanya mawasiliano akiwa mahabusu gerezani halina tatizo, wala haliwezi kuharibu uchunguzi unaoendelea, kwa sababu tukio likiwa na jinai ndani yake huwa halina namna ya kulikwepa.

“Mambo ya kiupelelezi yana hatua zake, kuhusu kuwasiliana na watu ni lazima kwa sababu ndiye alikuwa anafahamu masuala ya fedha ya kule alikokuwa na hata utawala, sasa katika mazingira aliyochukuliwa aliyeachwa ni lazima ahitaji

maelekezo yake,” amesema.

Vilevile anasema naye analazimika kumpelekea simu mara kwa mara mahabusu kwa ajili ya kufanya mawasiliano.

Sindani na wenzake walikamatwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa mahakamani hivi karibuni mara baada ya taarifa za kifo cha mfungwa huyo na kujeruhi mwingine.

Sajenti Yusuph na Koplo Fadhili walikamatwa siku chache baada ya kutokea kifo cha mfungwa huyo na kumjeruhi  mwingine aliyenusurika kifo baada ya kuwahishwa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alikolazwa kwa wiki tatu sasa akipatiwa matibabu katika wodi ya wagonjwa walio katika uangalizi maalumu (ICU).

Mbonjola kufika Gereza la Liwale inaanzia Kisarawe ambako Desemba 10, 2015 Mahakama ya Wilaya ilimhukumu kifungo cha miaka 30.

Kwa upande wake, Mbunge wa Liwale (CCM), Zuberi Kuchauka, ameshitushwa na taarifa za kifo cha mfungwa huyo na mwingine kujeruhiwa kutokana na na kipigo jimboni kwake baada ya kuzungumza na JAMHURI hivi karibuni.

“Liwale kuna tabia ya watu kunyamanzia matukio, sijui ni kwa sababu ya nini? Kuhusu kifo cha mfungwa huyo (Ngatumbara) kwamba kimetokana na kipigo wewe ndiye mtu wa kwanza kuniambia, nilijua amefariki dunia kwa ugonjwa wa kawaida.

“Taarifa ninayoifahamu ni ya magereza kuchelewesha mwili wa marehemu kukabidhiwa kwa ndugu, wala sijui kama kuna mfungwa mwingine amelazwa MOI,” amesema.

Kuchauka amewalaumu wananchi wa jimbo lake kwa kuyakalia kimya matukio kama hayo. JAMHURI liliripoti hivi karibuni kwamba linafahamu kifo cha Ngatumbara kimetokea baada ya yeye na mpambe wake kutembezewa kipigo na

askari magereza, wakilazimishwa kuwataja watu walioiba mahindi ya Sindani.

Awali, wafungwa hao walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Liwale ambako wataalamu walithibitisha kifo cha Ngatumbara na baadaye Mbonjola akahamishiwa Hospitali ya Mkoa ya Sokoine na kisha kupelekwa MOI.

Inadaiwa kuwa wizi wa mahindi ya Sindani ulitokea wakati wafungwa wakivuna kutoka katika shamba la magereza.

“Mahindi yaliyoibwa yalikuwa yamekusanywa barabarani tayari kusombwa na magari kupelekwa ghalani na mengine kwa Afande Sindani ambaye siku hiyo alikuwa safarini Dar es Salaam.

“Akatumiwa taarifa za kuibwa mahindi yake yaliyovunwa. Aliporejea Liwale, akamuita msaidizi wake na kuhoji juu ya taarifa za wizi. Akajibiwa kuwa zipo lakini hazikuwa zimefanyiwa uchunguzi,” amesema mtoa taarifa mwingine

aliyezungumza na JAMHURI hivi karibuni.

Amesema hadi wakati huo hakukuwa na yeyote anayetuhumiwa kwa sababu hakuna aliyebainika kupelekewa au kukutwa na mzigo wa mahindi.

Taarifa hizo hazikumridhisha Sindani, ambaye kesho yake, Juni 8, 2022 akawaita nyampala (Ngatumbara) wa gereza na mpambe wake (Mbonjola) na kuwataka wampe taarifa kamili lakini wakamjibu kuwa hawajui chochote.

“Palepale akaanza kuwapiga akiwataka wamtaje aliyechukua mahindi na amechukua kiasi gani. Alipochoka, akaona haitoshi, akawaita askari wawili; Sajenti Yusuph na Koplo Fadhili wamsaidie kuwapiga hadi watakapowataja wezi,”

amesema.

Mtoa taarifa huyo amesema kuwa kipigo hicho hakikuwafurahisha askari wengine ambao waliwazuia Sajenti Yusuph na Koplo Fadhili wasiendelee kuwapiga, wakihoji iwapo kama wana uhakika kweli kuna wizi umetokea; wengi wakiamini kuwa uchache wa mavuno ya mwaka huu ndiyo sababu ya kudhani kwamba wizi umefanyika.

Pia amesema baada ya Sindani kubaini kuwa wafungwa hao wameumizwa sana, akaondoka kisha muda mfupi baadaye akarudi na kuwapakia katika gari kuwapeleka hospitalini ambako madaktari walibaini kuwa tayari Ngatumbara alikuwa ameshafariki dunia huku matumaini ya kupona kwa Mbonjola ni madogo.

Amsema madaktari wakashauri tukio liripotiwe polisi na kupewa ‘PF3’ ili taratibu za matibabu kwa Mbonjola zifanyike.

Ndugu wa Ngatumbara aliyezungumza na JAMHURI hivi karibuni, Said Mohamed, amesema awali taarifa kuwa mfungwa huyo ana hali mbaya walizipata kutoka kwa mtu wasiyemfahamu, aliyewaeleza kuwa amemuona Hospitali ya Wilaya ya Liwale.

“Muda mfupi baadaye tukapigiwa simu na Diwani (Nassoro) akatueleza kuhusu tukio hilo. Siku ile afya yangu haikuwa nzuri, hivyo nikampigia simu Kassim Arafi (ambaye ni ndugu yake) nikamwambia aende hospitalini kuhakiki taarifa,”

amesema.

Anasema alipofika hospitalini, Arafi, alizuiwa kumuona Ngatumbara kwa maelezo kuwa akatafute kibali kutoka kwa Mkuu wa Gereza.

Kutokana na kizingiti hicho, Arafi, aliamua kuulizia taarifa za ndugu yake kutoka kwa watu wengine, ndipo akaelezwa kuwa alifikishwa hospitalini akiwa na mfungwa mwingine, lakini yeye amefariki dunia.

Kutokana na utata wa taarifa na kwa kushauriana na diwani, Mohamed na ndugu zake wakaona ni vema kuwasiliana na mkuu wa wilaya aliyewataka wafike ofisini kwake siku inayofuata.

“Tukaenda kuzungumza naye. Akakiri kuwa anazo taarifa za tukio na kuwa amewasiliana na Mkuu wa Mkoa wa Lindi atume vyombo vya dola kufanya uchunguzi.

“Siku iliyofuata tukaitwa na Mkuu wa Gereza akisema tunahitajika kwenda Kipule liliko gereza tukapate maelekezo. Sisi tukamwambia hatuna usafiri. Akatutumia gari. Mimi, Arafi na Omari Mchite tukaenda gerezani ambako tuliwakuta

maofisa wa vyombo vya ulinzi na usalama,” amesema.

Miongoni mwa maofisa waliokuwapo ni Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Lindi na Sindani akawaeleza ndugu wa Ngatumbara kuwa kifo cha ndugu yao kimetokana na shinikizo la damu (pressure).

Mohamed anasema walipohoji zaidi, wakaelezwa kuwa katika gereza hilo kuna kawaida ya kutokea

wizi wa mahindi na mara nyingi wafungwa wanapoyasomba kutoka shambani hupotea.

“Sindani akadai kuwa askari wasimamizi ndio watekelezaji wa aina hiyo ya wizi. Akatuambia kuwa siku ya tukio yeye alikuwa amesafiri, akamuacha msaidizi wake afuatilie wizi wa mahindi unaofanywa na askari magereza kwa kushirikiana na wafungwa,” amesema.

Aidha, amesema Sindani mbele ya maofisa wengine kutoka mkoani, akawaambia kuwa aliporudi alipewa orodha ya askari wanaohusika, lakini hakutaja majina yao.

Amesema Sindani akaendelea kusema kuwa kesho yake aliitisha gwaride rasmi likijumuisha wafungwa wote na askari magereza, na kutamka kuwa wezi wa mahindi wamekwisha kufahamika, akiwataka kutorudia tabia hiyo.

Baada ya onyo hilo, amesema Sindani alipanda gari lake na kuelekea mjini na wakati akiwa njiani ndipo akapigiwa simu na msaidizi wake kumpa taarifa za Ngatumbara kuzidiwa, kupelekwa zahanati, na kwamba walikuwa wanaomba kibali

apelekwe Hospitali ya Wilaya.

“Akasema kuwa msaidizi wake alitoa kibali, Ngatumbara akapelekwa hospitalini. Nako hali ikazidi kuwa mbaya hadi akafariki dunia,” amesema Mohamed.