Juma lililopita niligusia kuasisiwa kwa demokrasia na kutangazwa rasmi tangazo la haki za binadamu. Leo naangalia baadhi ya changamoto zinazotokana na misamiati hii ya siasa, utawala na haki kwa wananchi wa Afrika.

Nathubutu kusema tawala karibu zote duniani zinakiri kuheshimu na kufuata misingi ya demokrasia na kanuni za haki za binadamu. Lakini kuna dosari za makusudi za hapa na pale katika uelewa, usimamizi na utekelezaji wa misamiati hii mbele ya wananchi na viongozi wa mataifa mbalimbali.

Dosari ambazo zinatokana ama na purukushani au kuzuia utawala wa watu, kwa ajili ya watu na kwa manufaa ya watu na badala yake kujali utawala wa mtu binafsi, kwa faida yake na kwa manufaa ya watu wachache. Huu ni uzuzu wa aina yake kwa watu watendao. Hasara tupu.

Katika tabia kama hizi, baadhi ya tawala za mataifa yaliyoendelea yanawatendea mabaya (maovu) mataifa yanayoendelea (machanga na maskini) kwa kuwashawishi na kuwachochea kuanzisha mizozo, ghasia, mapigano hata vita.

Ingawa demokrasia iliasisiwa na kutekelezwa Ulaya na Marekani katika karne nyingi zilizopita, hapa Afrika ilianza kuzungumzwa mwishoni mwa karne ya 19 na mwanzoni mwa karne ya 20. Utekelezaji ulianza hasa miaka ya 1950 na kushamiri miaka ya 1960, nchi nyingi za Afrika zilipopata uhuru wa bendera.

Kadhalika sauti ya zumari ya tangazo la haki za binadamu, mnamo mwaka 1948, ilisikika Afrika. Sauti iliyotazamiwa kujenga na kuimarisha uelewano na maafikiano mema kati ya watawala na wanasiasa wa nchi husika.

Mayowe na sauti ya zumari yalivuma na kuziyumbisha nchi za Afrika, kuanzia miaka ya 1970 – 80 na kuendelea hadi sasa. Baadhi ya vijana walinzi wa Afrika wakaghafilika na kuanza kupokea ushauri na kuamini Wazungu ni bora kuliko wazazi wao na wao wenyewe. Ama! Usilolijua ni usiku wa giza.

Mambo ya kusikitisha na kushangaza makundi ya watawala, wanasiasa, watetezi wa haki za binadamu, wanafiki na vijana ambao ni ngao na walinzi wa taifa wakajikuta wameingizwa katika tasiliti, na wakajitengenezea sokomoko ndani ya nchi zao.

Wakashiriki katika umoja wa Wazungu na kukubali kuwa vibaraka, wahaini, wasaliti na wahujumu uchumi kwa kupora na kukomba mali za nchi zao na kupeleka Ulaya na Marekani. Wakasahau kulinda uhuru wao, ubinadamu wao, haki zao, utamaduni wao na kujenga uchumi wao kuondoa umaskini.

Wakaamua kuacha mikakati ya kuleta mapinduzi ya kiuchumi na kitamaduni kujenga nchi zao na kuipa sifa njema Afrika. Wakakubali kufanya maasi kinyume cha mapinduzi kwa lengo la kuwafurahisha Wazungu walio watawala zamani. Ama kweli, penye miti hakuna wajenzi. Maasi yaliyowatumbukiza wananchi wao katika vita ya wenyewe kwa wenyewe. Wananchi wengi wameuawa, wengine kubaki na vilema na maliasili zao kupelekwa Uzunguni na wao kuendelea kunyanyaswa na kuonekana mazumbukuku. Je, ni kweli wajinga ndio waliwao?

Kwa mtaji huu, hadi sasa nchi za Afrika zinabanwa kweli kweli na hoja za demokrasia, utawala wa sheria na haki za binadamu. Wanaobana ni Wazungu wa Ulaya na washirika wao, wakihubiri na kushadidia hoja hizo. Lakini kauli na matendo yao hayaoani!

Mama Afrika anataka demokrasia ya kweli, si demokrasia. Demokrasia ya kweli itakayowatoa Waafrika kwenye unyonge na umaskini na kuwafikisha kwenye uhuru kamili na utajiri, si ya kuwazidishia unyonge na kuwapa ufukara.

Waafrika tuamke na kuitafuta demokrasia ya kweli popote ilipofichwa, na tuikamate na kuitumia kwa masilahi yetu. Si kushikilia demokrasia inayotoa uwezo wa kusimama juu ya milima na kupokea mapesa kutoka kwa mabeberu kwa ajili ya kuangamiza nchi zetu. Je, ni kweli Waafrika ndivyo tulivyo?

202 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!