Tunaposikia kauli za viongozi kuwa uongozi wa nchi ni changamoto kubwa sana, siyo rahisi kwa wengi wetu kuelewa. Haihitaji kufanya utafiti wa kina kukubali ukweli huo.

Uongozi ni mzigo mkubwa, alisema Mwalimu Julius Nyerere. Akifafanua, alisema rais anapokuwa pale Ikulu husumbuliwa sana na jinsi ya kukabili mzigo wa matatizo yanayoikabili nchi kila wakati.

Na matatizo hayapo kidogo, na hayapunguwi. Kwanza kabisa, kuna tatizo la kukosa pesa za kutosha za kukabiliana na matatizo yaliyopo. Mapato siku zote hayafikii mahitaji. Tumewahi kusikia umahiri wa serikali kupata misaada ya kuziba pengo hili la mapato na matumizi. Lakini tumewahi kusikia wakati mwingine baadhi ya viongozi wetu kujisifia ni jinsi gani wamejenga uhusiano mzuri na wahisani kiasi cha kutuhakikishia kuendelea kupata misaada ya kufidia pengo kati ya mapato na mahitaji yetu kama nchi.

Hili si jambo la kulionea fahari hata kidogo. Ni aibu kwa mtu binafsi au serikali kujisifia kwa uwezo wake wa kuwa ombaomba. Kiongozi ambaye anaona kuwa hii ni sifa hapaswi kuwa kiongozi. Kiongozi anayeonea aibu suala hii ataelekeza uwezo wake na wa viongozi wenzake kutafuta suluhisho la namna ya kupunguza utegemezi. Kiongozi wa aina hii analala na mzigo wa mawazo kila siku.

Kujitegemea hakufikiwi kwa haraka kwa hiyo yapo matatizo mengi ya mpito ambayo yanamuumiza kichwa kiongozi mahiri. Pesa hizo hizo chache ambazo zinapatikana, kujumlisha na zile za kuomba huwa zinasubiriwa kwa hamu na baadhi ya watu ambao huamini kuwa wao Mwenyezi Mungu kawaleta ulimwenguni kupanga mikakati ya kutumia mali ya umma kwa manufaa yao.

Kwa hiyo kiongozi huyo huyo ambaye anakosa usingizi kutafuta pesa za kuendesha nchi, anakabiliwa pia na umati wa watu ambao unataka pesa hizo hizo kwa manufaa yao. Miundombinu ambayo inajengwa kwa viwango hafifu, upungufu wa huduma mbalimbali kwenye sekta ya afya, ujangili na uharibifu wa mazingira, na kukithiri kwa rushwa kwenye kila nyanja ya maisha ya raia ni baadhi ya maeneo ambayo baadhi ya watu wanayatumia kujinufaisha wao badala ya taifa. Yote haya ni nyongeza ya masuala ya kumkosesha usingizi kiongozi mahiri.

Elimu ni upanga wenye ncha mbili, na unaweza kumkosesha kiongozi usingizi kwa namna mbili tofauti. Elimu kubwa sana ya raia ni chanzo cha kuhoji uongozi na uamuzi wa uongozi katika kila hatua. Kuwa kiongozi mahiri haina maana kuwa pia na uwezo wa kufanya uamuzi sahihi kila wakati. Uwepo wa raia waliobobea kwa elimu na wenye kutambua wajibu wao wa kuhoji uamuzi wa viongozi na sera ni chanzo cha kukosesha usingizi viongozi, bila kujali kama ni mahiri au la.

Lakini tunaamini elimu inapokuwa chanzo cha raia kuhoji, kwa hoja, uamuzi wa viongozi na sera zao; basi kiongozi mahiri anayekabiliwa na changamoto kama hiyo naye atapima zile hoja na kuzifanyia kazi kwa manufaa ya wote. Uamuzi wowote unaochukuliwa kwa manufaa ya wote, unapaswa kumpunguzia kiongozi mzigo wa uongozi.

Lakini tunatambua kuwa elimu si kitu ambacho kila mtu anacho. Wapo wengi ambao hawana elimu ya kutosha au wamepata elimu hafifu. Elimu ndogo au hafifu ni changamoto nyingine kubwa ambayo inapaswa kukosesha usingizi viongozi wetu kwa muda mrefu sana.

Juma moja lililopita nikiwa nyumbani nilitembelewa na jirani yangu ambaye aliona jarida la kitabu cha Mwalimu Nyerere, Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania na akasema: “Kingekuwa kitabu cha Kiswahili ningempelekea mwanangu akasome. Lakini ni cha Kiingereza.”

Mwanzo nilicheka kwa kuwa ni mtu ambaye nataniana naye, lakini baadaye nilitambua kuwa nachekea suala ambalo halipaswi kumchekesha mtu. Kwanza, aliyetamka hayo amesoma hadi darasa la saba. Pili, baya zaidi, kile kitabu kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili, lakini yeye hakutambua hilo. Tatu, na la msingi zaidi, alishika kitabu ambacho kiliandikwa na Mwalimu Nyerere, kiongozi ambaye aliongoza Tanzania akisisitiza juu ya umuhimu wa elimu kwa Taifa, na kama nyenzo ya kumkomboa raia kutokana na changamoto zinazomkabili. Ni kiongozi aliyechangia mawazo jadidifu juu ya aina ya elimu ambayo Watanzania wanapaswa kuipata.

Aliyeandika kitabu angesikia maneno ya jirani yangu angepata majonzi makubwa, na kukoswa usingizi kwa muda mrefu. Lakini hata kiongozi yeyote leo anapaswa kuona hali hiyo kama ni mzigo mwingine mkubwa kati ya mizigo mingi inayoikabili nchi yetu.

Kiongozi asiye mahiri hapaswi kusumbuliwa sana na raia ambao hawana elimu ya kutosha, kwa sababu katika maisha ya siku hadi siku raia wenye elimu hafifu si watu ambao watamkosesha usingizi kama wale ambao wana elimu ya kutosha. Ni watu ambao hawana makuu, ambao wanaendelea na maisha yao bila kuhoji hili wala lile.

Lakini tukubaliane kuwa raia aliyeelimika vya kutosha atamtua mzigo mzito kiongozi wa nchi kwa sababu tu atakuwa amejiongezea uwezo wa kukabiliana na changamoto nyingi ambazo zinatafutiwa suluhisho Ikulu au kwenye wizara mbalimbali.

Ongezeko la elimu bora kwa raia linaweza hata kumfanya kiongozi akorome siku hadi siku, ingawa hatutarajii yatokee hayo. Anayepata usingizi wa pono Ikulu anahitaji kutumbuliwa.

Lakini ni dhahiri kuwa kupunguzwa kwa changamoto nyingi za Taifa kunategemea sana kuongezeka kwa elimu bora kwa raia.

By Jamhuri