Kwa hizi kazi za taaluma (professionals) kama ualimu, udaktari, ufundi, sheria, kilimo na kadhalika zina kima chake cha kuhitimu.

Mimi sijawahi kusikia hata mara moja duniani wamepatikana wahitimu wa udaktari wa binadamu au wanyama waliopewa mafunzo ya dharura ya muda mfupi wa miezi sita au hata mwaka mmoja!


Sasa, vipi hii taaluma ya ualimu kuchakachuliwa hadi anapatikana mwalimu mhitimu wa mwezi mmoja tu? Mwalimu wa namna hii ndiye tumemwandaa kutoa elimu kwa watoto wetu. Kweli atatoa elimu bora?


Isitoshe walimu hawa kwa kozi ya mwezi mmoja walikuwa ni wa muda, na hivi sasa wengi wao wamekwenda kujipatia elimu ya juu kwenye vyuo mbalimbali.

Hali namna hii imewakosesha watoto wa shule za kata kuwa na walimu wa kutosha katika shule karibu zote katika nchi. Hapo hakuna “elimu bora” inayoweza kutolewa katika shule hizi.


Walimu katika nchi hii wana matatizo mengi mno. Lipo hili la taaluma ya ualimu kuchakachuliwa. Limewakatisha tamaa walimu wengi wenye hati za ualimu baada ya kuhitimu kozi za miaka miwili katika vyuo pale wanapochanganyishwa (equated) na walimu wa kidato cha VI wenye mafunzo ya mwezi mmoja tu.


Baadhi wameacha ualimu na kwenda kupata kazi nyingine nje ya kufundisha darasani. Walimu wana mishahara midogo mno wakilinganishwa na wenzao katika taaluma nyingine. Walimu hawana nyumba za kuishi katika maeneo ya shule wanakofundisha.


Walimu hawapati likizo kwa wakati na hasa hawalipwi stahili zao za nauli. Sisi zamani miaka ile ya 1950 -1970 tulienda likizo kwa gharama za serikali kwa kutumia karatasi au vocha zilizoitwa “motor – warrants”. Ilikuwapo kanuni ya upendeleo maalumu kwa watu wa mikoa ya Kusini – Lindi/Mtwara na Ruvuma kupewa hati ya kwenda kwa ndege kutoka Dar es Salaam hadi Lindi/Mtwara/Songea.


Upendeleo huo ulikuwapo katika “General Orders” za utumishi serikalini kifungu cha 8 (Special privilege for civil servants from Southern Province during the rainy season) na ulitumika wakati wa masika tu (Desemba – Mei).


Mwalimu wa leo anafanya kazi katika mazingira magumu mno. Hana utulivu kiakili na kiafya na upo usemi wa kale wa Kirumi usemao “MENS SANA IN CORPORE SANO.” Maana yake “akili timamu hutokana na afya timamu ya mwili wa mtu.” Mwalimu wa leo hatulii kiakili, hivyo basi hawezi kuandaa masomo yake sawasawa, na ni mnyonge kiafya.

 

Kwa hiyo tukitaka kweli kupata elimu bora kwa watoto wetu, Dira ya Wizara ya Elimu, Sera ya Elimu na mazingira yote yaandaliwe kulenga kwenye ubora wa elimu. Mitaala, mafunzo ya ualimu, shule za msingi, za sekondari hadi vyuo ipangwe kutoa elimu bora kwa watoto wa Tanzania.


Mwalimu Nyerere aliwahi kutamka, “INAWEZEKANA KUFANYIKA, FANYA SEHEMU YAKO (Nyerere: Mei 12, 1964 bungeni).  Tujiulize wananchi, wazazi, na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kweli kila mmoja wetu ametekeleza wajibu wake?


Brigedia Jenerali mstaafu Francis Mbenna anapatikana katika simu 0715 806758. Alikuwa mwalimu wa sekondari na Afisa wa JWTZ. Ni mwanahistoria na ameandika kitabu cha HISTORIA YA ELIMU TANZANIA toka 1892 hadi sasa (Dar es Salaam University Bookshop).


By Jamhuri