MOSHI

NA CHARLES NDAGULLA

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kilimanjaro
imewafikisha mahakamani mtumishi wa
halmashauri na mfanyabiashara
wakituhumiwa kufuja fedha za Uchaguzi
Mkuu mwaka 2015.
Safari hii waliofikishwa mahakamani ni
Mkuu wa Kitengo cha Uchaguzi katika
Halmashauri ya Wilaya ya Hai, Edward
Ntakiliho, akikabiliwa na mashtaka manne.
Kati ya mashtaka hayo, matatu ni ya
kughushi na kuiba fedha za umma
zilizokuwa chini ya uangalizi wake.
Ntakiliho na mfanyabiashara, Oscar

Kigumu, ambaye ni mmiliki wa Mgahawa wa
Oscar Food and Beverage Catering
Service, wamefikishwa mbele ya Hakimu
Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Hai,
Devota Msofe na kusomewa mashtaka na
Mwendesha Mashtaka wa Takukuru,
Rehema Mteta.
Ntakiliho anatuhumiwa kuandaa nyaraka za
uongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri
wake na kufanikiwa kufuja Sh milioni 27.16.
Fedha hizo zilitolewa na NEC katika Jimbo
la Hai zikilenga uendeshaji wa mafunzo ya
wasimamizi wa vituo vya uchaguzi.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka,
mshtakiwa huyo anadaiwa kutumia nyaraka
za kughushi kuonyesha kwamba Sh milioni
3.15 zilitumika kulipia usafiri wa
wawezeshaji wa mafunzo huku akifahamu
kuwa nyaraka hizo zilikuwa ni za kughushi.
Pia anadaiwa kuandaa nyaraka za uongo
kuonyesha Sh milioni 3.702 zilitumika
kulipia ukodishaji wa ukumbi wa mafunzo
na vipaza sauti; na Sh milioni 20.308
zikidaiwa kulipia chakula na viburudisho.
Kwa upande wake, Kigumu, anashtakiwa

kwa makosa mawili – moja likiwa ni
kughushi nyaraka kuonyesha kuwa
Kampuni yake ya Oscar Food and
Beverage Catering Service ilipokea Sh
milioni 20.308 kutoka kwa Edward Ntakiliho.
Katika shtaka la pili, mfanyabiashara huyo
anadaiwa kumsaidia Ntakiliho kufanya
ubadhirifu wa Sh 1,495,500.
Washtakiwa wote walikana mashtaka yao
na wako nje kwa dhamana hadi Septemba
5, mwaka huu.
Hivi karibuni Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro
iliwafikisha mahakamani aliyekuwa
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Jimbo la
Mwanga mkoani humo, Hassan Mkwizu,
kwa makosa ya kughushi nyaraka na kufuja
fedha za umma.
Mkwizu na Mhasibu Msaidizi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga,
Mustafa Haji na Mtunza Kumbukumbu,
Monica Mkasa, walifikishwa katika
Mahakama ya Wilaya ya Mwanga.
Mwendesha Mashtaka kutoka Takukuru,
Suzan Kimaro, alisoma mashtaka hayo
mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa
mahakama hiyo, Mariam Lusewa.

Kwenye hati ya mashtaka, kosa la kwanza
linamkabili mshtakiwa wa pili, Mkwizu,
anayedaiwa kuwa Oktoba 22, 2015 akiwa
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi katika
halmashauri hiyo alighushi nyaraka zenye
majina ya watu 220 akidai kuwa walikuwa ni
walinzi.
Pia anadaiwa kuandaa nyaraka za uongo
kwa lengo la kumdanganya mwajiri na
kuonyesha kuwa walinzi hao walilipwa
posho ya Sh milioni 11 ili kusimamia
Uchaguzi Mkuu wakati akijua si kweli.
Katika kosa la tatu, mshtakiwa huyo
anadaiwa kufuja Sh milioni 11 ambazo ni
fedha za Halmashauri ya Wilaya ya
Mwanga. Mtuhumiwa alikana mashtaka
yote.
Shtaka la nne linawakabili washtakiwa Haji
na Mkasa wanaodaiwa kumsaidia Mkwizu
kutenda kosa kinyume cha Kifungu cha 30
cha Sheria ya Kupambana na Rushwa
Namba 11 ya mwaka 2007.
Washtakiwa wote walikana mashtaka hayo
na wako nje kwa dhamana. Kesi hiyo
ilitajwa Julai 19, mwaka huu.
Takukuru pia ilimfikisha mahakamani
mfanyabiashara, Abdallah Majungu,
akishtakiwa kwa kosa la kumsaidia

Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi, Mkwizu
kutenda kosa lililomwezesha kujipatia Sh
milioni 12.4.
Ilidaiwa kuwa fedha hizo zilitolewa na Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa ajli ya
kukodi magari 20 na vipaza sauti 20
ambavyo vingegawanywa katika kata 20 za
Jimbo la Mwanga.
Kandarasi hiyo ya kusambaza vipaza sauti
ilitolewa kwa mfanyabiashara huyo na
kuonyesha kazi hiyo ilifanyika, lakini
Takukuru wanadai kuwa kazi hiyo
haikufanyika.
Takukuru wanadai kuwa matangazo ya
kuhamasisha wapiga kura katika kata zote
yalisambazwa kwa kutumia gari la serikali
lililoazimwa Idara ya Maji Wilaya ya
Mwanga.
Mfanyabiashara huyo alifikishwa mbele ya
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya
Mwanga, Jacqueline Osujaki na kusomewa
mashtaka na Mwendesha Mashtaka wa
Takukuru, Suzan Kimaro.
Wilayani Hai, Takukuru ilimfikisha
mahakamani Mhasibu wa Halmashauri ya
wilaya hiyo, Eline Lema, akikabiliwa na
tuhuma za ubadhirifu wa Sh milioni 5 za
makusanyo ya ushuru wa Soko la Kwa

Sadala.
Inadaiwa kuwa Aprili 27, 2015 alipokea
fedha kutoka kwa mmoja wa mawakala
waliopewa zabuni katika soko hilo na
akampa stakabadhi ya malipo yenye namba
00089902.
Alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa
Mahakama ya Wilaya ya Hai, Regina Moshi,
na kusomewa mashtaka na Mwendesha
Mashtaka wa Takukuru, Rehema Mgeta.
Inadaiwa kuwa kitabu cha stakabadhi ya
malipo kilichotumika hakikuwa kwenye
kumbukumbu za vitabu alivyopewa na
mwajiri wake.
Mshtakiwa huyo hakutakiwa kujibu
chochote kutokana na kosa lake kuangukia
kwenye makosa ya uhujumu uchumi na
mahakama hiyo kutokuwa na nguvu
kisheria kusikiliza shauri hilo.

MWISHO

By Jamhuri