Kiama kipya

*Sheria kuwabana wahama vyama yaiva,

wengi kulia

*Wanaohamia CCM waambiwa wanaingia

kwenye safina

*Watabanwa wasihamie upinzani uchaguzi

mwaka 2020

NA MWANDISHI WETU

Wanasiasa wanaohama vyama
wanakabiliwa na mtego mwingine mpya,
JAMHURI limethibitishiwa.
Mpango huo uko kwenye hatua za awali
ambapo tayari serikali imeanza mchakato
wa kukusanya maoni ya wadau ili kufanya
mabadiliko kwenye Sheria ya Vyama vya
Siasa.
Kwenye mabadiliko hayo kunakusudiwa
kutungwa sheria itakayofuta utaratibu wa
sasa wa mwanachama kuhama chama na
kwenda kuwania udiwani au ubunge katika

chama kingine kama ilivyo sasa.
Kwa mabadiliko hayo, kunakusudiwa
kutungwa sheria ya kuwapo muda maalumu
ambao mwanasiasa anayehama chama
kimoja kwenda kingine atatakiwa asubiri
upite ndipo apate haki kisheria kuwania
udiwani au ubunge.
Inapendekezwa walau mwanasiasa
anayehama chama azuiwe kwa mwaka
mmoja au miwili kuwania udiwani au
ubunge kupitia chama kipya alichojiunga.
Inapendekezwa pia sheria hiyo iwaguse pia
wagombea urais.
Pamoja na mambo mengine, sheria hiyo
inatajwa kuwa inalenga kunufaisha Chama
Cha Mapinduzi (CCM) ambacho wakati wa
uchaguzi kimekuwa kikiumia kwa kukimbiwa
na baadhi ya wanachama wanaokosa
uteuzi.
Mara kadhaa imekuwa wale wanaoachwa
CCM na kwenda kugombea kupitia vyama
vingine vya siasa, wameshinda.
Mfano wa hali hiyo ni kwa aliyekuwa
Mbunge wa Karatu, Dk. Wilbrod Slaa,
ambaye baada ya kuachwa CCM, alijiunga
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) na kushinda ubunge.

Hali kama hiyo imeshatokea pia kwa Steven
Wasira mwaka 1995, ambapo baada ya

kuachwa CCM, aligombea kupitia NCCR-
Mageuzi na kushinda kiti cha ubunge Jimbo

la Bunda mkoani Mara.
“Sheria itawabana wanasiasa wanaohama
chama kimoja kwenda kingine wasiweze
kugombea kwa muda fulani…wadau
wametakiwa watoe maoni yao,

” kimesema

chanzo chetu.
Kwa mantiki hiyo, chanzo hicho kinasema,
wale wanaohamia CCM sasa wanajiweka
kwenye nafasi finyu ya kukihama chama
hicho na kugombea kwingine hata kama
hawataridhishwa na uamuzi wa vikao vya
mchujo.
“Hii ni kama safina. Hawa wanaoingia sasa
ni kama wanaingia kwenye safina. Safina
ikishafungwa hakuna wa kutoka wala
kuingia, aliye nje atabaki nje, aliye ndani
atabaki ndani, hata akiamua kuondoka,
hatagombea,

” kimesema chanzo chetu
kikirejea maandiko yaliyomo kwenye vitabu
vitakatifu.
Mpango huo unaelezwa kuwa unasukwa
kwa ustadi mkubwa, lengo likiwa
kuhakikisha kuwa CCM haiathiriwi na
uhamaji wa wanachama wake mwaka 2020.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James
Mbatia, anasema kinachopendekezwa
kufanywa ni sheria mbaya anayodai
kwamba inalenga jambo fulani
(halitaji) baada ya kuuwezesha mfumo wa
utawala kufanya kazi kwa ufanisi.
“Katiba inaruhusu mtu yeyote kugombea.
Haya mambo ya mtu kuwekewa muda wa
kugombea au kutogombea yawe ya ndani
ya vyama na siyo kisheria. Hizi ni sheria
zinazotungwa kuangalia masilahi ya muda
fulani. Ukikandamiza watu wasiwe na
uhuru, unaweza kuwafanya wafanye
mambo mabaya. Haya mambo yaachwe
kwenye vyama na mtu binafsi mwenyewe.
“Achia mtu uhuru, ukiweka sheria, kanuni
hapo hekima inakuwa haitumiki – busara
inakataa. Sheria zipo, lakini hazifikii hata
robo ya hekima. Hata bungeni tunatumia
hekima na busara – hatutumii Katiba na
sheria tu,

” anasema Mbatia.

Mmoja wa viongozi wa CCM aliyezungumza
kwa masharti ya kutotajwa jina amesema
masuala ya kisheria yana mahali
yanakoanzia.
“Mchakato wa sheria siyo speculation,
unaanza kwa muswada wa serikali,
ukishawekwa hadharani ndipo tunaanza

kuujadili.
“Chama chetu hakijapata hilo jambo, na
kama hatujapata maana yake hilo jambo
halipo. Hiki ndicho chama kinachoongoza
serikali, kwa hiyo hata lingekuwa ni suala la
kuwa na mbunge binafsi, ina maana
tungekuwa na taarifa,

” amesema.

Msajili wa Vyama vya Siasa Tanzania, Jaji
Francis Mutungi, amezunguma na
JAMHURI na kuthibitisha kuwapo kwa
mpango wa kufanya mabadiliko hayo.
Anasema watu wengi wamepata uzoefu wa
yanayoendelea sasa (wanasiasa kuhama
vyama), na kuonekana kuwapo umuhimu
wa kuwa na sheria.
Anasema sheria iliyopo sasa haikidhi
harakati za kisiasa, ndiyo maana
kukaonekana kuwapo sababu ya kutunga
sheria badala ya kuifanyia mabadiliko.
“Mwanzoni ilionekana kufanywe
marekebisho, lakini baadaye ikaonekana
heri itungwe sheria, maana kama ni
marekebisho yamekwisha kufanywa mengi
sana. Maoni yalikwisha kufanywa, lakini
hadi sasa wadau bado wana nafasi ya
kuleta maoni yao, maana tupo kwenye
hatua, milango haijafungwa. Inasubiriwa
‘draft’ ya kwanza, kwa maana hiyo bado

mawazo ya kuboresha sheria yanapokewa
mpaka itakapofika hatua ya kupeleka
bungeni.
“Huu ndio wakati muafaka wa kuleta maoni
ya wadau, maana mlango bado uko wazi,

anasema.
Kwa miezi kadhaa sasa kumekuwapo wimbi
kubwa la wanasiasa kuhama chama kimoja
na kujiunga chama kingine. Kwenye
hamahama hiyo, CCM ndiyo inayoonekana
kunufaika zaidi, kwani imekuwa ikipokea
madiwani na wabunge kutoka vyama
vingine kama Chadema, Chama cha
Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi.
Mwishoni mwa mwaka jana CCM ilimpoteza
mbunge mmoja, Lazaro Nyalandu,
aliyejiunga Chadema.
Hadi wiki iliyopita wabunge wa upinzani
waliojiunga CCM ni Mwita Waitara (Ukonga
– Chadema), Dk. Godwin Mollel (Siha –
Chadema), Maulid Mtulia (CUF –
Kinondoni), Julius Kalanga (Monduli –
Chadema) na Zubeir Kuchauka (CUF –
Liwale).
Kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika mwezi
huu, nafasi 77 za madiwani zilikuwa wazi.
Nafasi 37 kati ya hizo zilikuwa za madiwani
waliofariki dunia, na nafasi 40 ilikuwa kujaza

nafasi za madiwani waliohama vyama vyao
na kujiunga CCM.
Inakisiwa kuwa uchaguzi mdogo wa
mbunge hugharimu wastani wa Sh bilioni
1.5; na ule wa diwani ni Sh milioni 200 hadi
300 kwa kila kata.
Wakati serikali ikijiandaa kufanya
mabadiliko ya kubana wanasiasa
wanaohama vyama, wiki iliyopita JAMHURI
liliandika kuwapo mpango wa kufanya
mabadiliko mengine makubwa ya sheria,
yakilenga kupunguza idadi ya majimbo,
wabunge wa kuchaguliwa na wabunge wa
viti malumu.
Tayari wataalamu wa sheria wamekwisha
kupewa kazi ya kuainisha vipengele kwenye
sheria husika, ikiwamo inayoipa nguvu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kugawa
majimbo ya uchaguzi.
Shughuli hiyo imeanza kufanywa kwa
umakini na usiri mkubwa, lengo likiwa
kuandaa mapendekezo ambayo baadaye
yatafikishwa kwa wadau.
Miongoni mwa mabadiliko ambayo huenda
yakaanza kuonekana kwenye Uchaguzi
Mkuu wa mwaka 2020 endapo mpango huo
utafanikiwa ni kubadili mfumo wa sasa wa
majimbo yaliyopo na badala yake

halmashauri zikawa ndiyo ‘majimbo’ mapya.
Kwa hatua hiyo, baadhi ya manispaa au
halmashauri ambazo zina majimbo ya
uchaguzi mengi huenda zikabaki jimbo
moja. Lakini kuna mapendekezo mengi ya
wilaya zifanywe ndiyo majimbo.
Kwa sasa idadi ya wabunge inayounda
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ni 393. Mchanganuo wake na
idadi ikiwa kwenye mabano ni kama
ifuatavyo: Wabunge wa majimbo (264),
wabunge wa Viti Maalumu (113), wabunge
wa Kuteuliwa na Rais (10) wabunge kutoka
Baraza la Wawakilishi (5) na nafasi moja ya
Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Habari zilizopatikana kutoka serikalini
zinasema kwenye mabadiliko
yanayokusudiwa kufanywa endapo yatapita,
idadi ya majimbo itakuwa ni ile idadi ya
halmashauri zilizopo nchini, hasa kwa
upande wa Tanzania Bara. Tanzania Bara
ina halmashauri 186 ambazo ziko katika
wilaya 141 za mikoa yote 26. Kati ya hizo
halmashauri 6 ni za majiji.
Idadi ya wabunge wa kuchaguliwa kwenye
majimbo ambayo sasa ni 264, huenda
ikashuka hadi wabunge 180.

Wabunge wazungumza

Kuhusu mabadiliko ya majimbo, baadhi ya
wabunge waliozungumza na JAMHURI
wamekuwa na maoni tofauti.
Mbunge wa Viti Maalumu, Jacqueline
Ngonyani (CCM), anasema atakuwa
kwenye nafasi nzuri ya kulizungumzia
endapo litafikishwa bungeni.
“Kama litafika kwetu wabunge nitamwaga
vitu vya uhakika wakati wa kuchangia,

amesema.
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea
(Chadema), anaunga mkono utaratibu mpya
wa halmashauri kuwa majimbo, akisema
utasaidia kubana matumizi ya fedha za
umma.
Anasema uamuzi huo utakuwa na tija kama
jambo hilo litaingizwa katika Katiba ya nchi.
“Hoja siyo idadi kubwa ya wabunge, bali
wabunge bora. Itaondoa wabunge mizigo
ambao kazi yao ni kupiga makofi na
kushangilia tu bungeni. Gharama za
kuendesha Bunge hapa nchini ni kubwa
sana, mbunge mmoja analipwa karibu Sh
bilioni 1 kwa miaka mitano,

” amesema.

Anasema kufutwa kwa majimbo ni
mapendekezo ya wananchi katika rasimu ya
Katiba yaliyomo kwenye Tume ya
Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji
Joseph Warioba.
Anasema NEC isifanye suala hilo kwa
utashi wake, bali liwe kwenye Katiba ili
kuepusha kuongeza wilaya ndani ya
halmashauri moja.
Anatoa mfano kuwa kwa mfumo wa sasa
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ina
majimbo matatu (Ilala, Segerea na Ukonga)
na iwapo utaratibu huo hautawekwa katika
utaratibu unaoeleweka (Katiba) inaweza
kuanzishwa wilaya nyingine na kuirudisha
nchi kwenye utaratibu ule ule.
Kubenea anashauri ubanaji wa matumizi ya
Bunge uende sawa na kuboresha utendaji
kazi wa wabunge, likiwamo suala la kupewa
magari kwa shughuli za kibunge.
Anashauri nafasi 10 za wabunge wa
kuteuliwa alizopewa rais kikatiba nazo
zifutwe, na badala yake yake apewe
mamlaka ya kumteua Mtanzania yeyote
mwenye sifa zinazotakiwa kuwa waziri bila
kuwa mbunge.
Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia
(CCM), anasema atakuwa kwenye nafasi

nzuri kulijadili suala hilo endapo litafikishwa
bungeni.
Mbunge wa Siha, Godwin Mollel (CCM),
anasema ufutaji wa majimbo hauna budi
ufanywe kwa hadhari.
“Jambo lolote ili liwe zuri halitakiwi
kufanywa kwa haraka, mimi naona mpango
huu utakuwa mzuri endapo utahusisha
utafiti wa kutosha kabla ya kuanza
utekelezaji wake,

” anasema.

Furaha yake ni kuwa endapo mabadiliko
hayo yanalenga masilahi mapana ya nchi
na wananchi kwa kuboresha hali zao,
hakuna sababu ya kuwa na shaka.
Anaonya kwa kusema mpango huo
utekelezaji wake usilenge kuangalia kubana
matumizi tu na kusahau suala la maendeleo
kwa wananchi, kwa kuwafikishia huduma
muhimu kwa urahisi.
Anaona ukubwa wa baadhi ya halmashauri
na jiografia zake kama kikwazo cha mpango
wa kuzifanya halmashauri kuwa majimbo ya
uchaguzi.
Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto
(CCM), anasema mpango huo utakuwa na
mafanikio endapo utatekelezwa kwa
kuzingatia miundombinu, idadi ya watu na

kipato cha watu wa maeneo husika.
Anasema inamuwia vigumu kuwa na
msimamo kwa kuwa bado hajapata taarifa
za utafiti zinazoainisha faida na hasara za
hatua hiyo.
“Kama watu walibadilika kutoka kwenye
kilimo cha kutumia jembe la mkono hadi
kutumia trekta, kwa nini hata sisi tusifanye
mabadiliko yenye tija?
“Ni suala la kuzingatia tunalenga kupata nini
na faida zake kabla ya kuupitisha na
kutunga sheria,

” anasema Mwamoto.
Anashauri mjadala huu upelekwe kwa
wananchi ili wauelewe na hatimaye watoe
maoni yatakayokuwa mwongozo wa
utungaji sheria.
Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlinga
(CCM), anasema mpango huo unaweza
kuwa na tija, lakini anaonya kwa kusema
unahitaji umakini kwa kuangalia ukubwa wa
jimbo, idadi ya watu na huduma za kijamii.
Anasema wapenda maendeleo wanatakiwa
kuonyesha ushirikiano kwa serikali ili kufikia
malengo.
Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar
es Salaam (UDSM), Dk. Azaveli Lwaitama,
anasema siasa za Afrika Mashariki na Kati

ni kama maigizo yenye kujaa malengo ya
kisiasa kuliko ustawi wa wananchi.
Anasema hakuna badiliko linaloweza
kufanywa na watawala bila uwepo wa
manufaa ya kisiasa yanayolengwa
kupatikana kupitia mpango huo.
“Hapa nchini mpango huo una malengo
mapana yenye manufaa kwa chama kilicho
madarakani zaidi ya hicho kinachoelezwa
kuwa ni kupunguza gharama.
“Mabadiliko yote yanayofanywa sasa nchini
yanaweza kuwa na maana pale watawala
watakapoamua kuirejesha rasimu ya Katiba
mpya iliyokuwa imependekezwa chini ya
usimamizi wa Jaji mstaafu Joseph Warioba.
“Taifa linahitaji taasisi imara itakayokuwa na
uwezo wa kutoa dira ya kiuongozi na
mwelekeo wa kimaendeleo kwa kiongozi
yeyote atakayepewa majukumu ya
kuliongoza taifa,

” anasema.

Anasema taifa halipaswi kuhangaikia
uimara wa mtu mmoja mmoja kisiasa, bali
kinachotakiwa ni ujenzi wa taasisi imara
itakayoweka dira na misingi ya kiutawala
kwa ajili ya miaka mingi ijayo.

Mwisho……….

Please follow and like us:
Pin Share