Mbunge wa Songea Mjini (CCM), Leonidas Gama atafikishwa mahakamani wakati wowote kutokana na ufisadi, JAMHURI linathibitisha.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la JAMHURI umebaini kuwa Gama, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro atapandishwa kizimbani muda wowote kujibu tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi na kujipatia fedha isivyo halali. Leonidas ni mtoto wa mwanasiasa mkongwe nchini Laurence Gama, ambaye naye alipata kushika wadhifa wa ukuu wa mkoa katika mikoa mbalimbali nchini.

Taasisi  ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) imekamilisha uchunguzi juu ya tuhuma za Ghama kutumia ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kufungua Kampuni ya Kilimanjaro Uchumi Co. Ltd inayodaiwa kusajiliwa na maofisa wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kwa maelekezo yake kama kampuni binafsi ya kibiashara.

Gama na wenzake, walitumia anwani ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ambayo ni S. L. P. 3070 kufungua kampuni hii binafsi. Pamoja na Ghama, Afisa mwingine ambaye tayari amehojiwa na TAKUKURU ni Godbless Kimaro kwa tuhuma sawa na za Mkuu wa Mkoa mstaafu Gama.

Mkuu huyo wa mkoa mstaafu ambaye sasa ni Mbunge wa Songea Mjini, ukiacha kashfa ya Kampuni ya Kilimanjaro Uchumi Co. Ltd, pia anakabiliwa na shutuma za nyingine za kumiliki hisa kwa kutumia jina la mtoto wake katika Kiwanda cha Moshi Cement kilichopo Holili, Wilaya ya Rombo kinachomilikiwa na kampuni ya Kichina iitwayo Jun Yu Investment International.

Katika kampuni hii, Gama ametumia jina la mtoto wake Muyanga Leonidas kumiliki hisa katika kiwanda hicho, ila uchunguzi wa TAKUKURU umeonyesha kuwa mtoto wake huyo si mwanahisa baada ya kumhoji kwani anaonekana hajui lolote na wala hakuwa na taarifa kama baba yake alitumia jina lake kummilikisha hisa katika Kiwanda cha Moshi Cement.

Katika shutuma ya kwanza, Kampuni ya Kilimanjaro Uchumi Co. Ltd, ilisajiliwa kwa maelekezo ya aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama na kujimegea eneo zaidi ya ekari 2,800 za ardhi mali ya Chama cha Ushirika wa Wafugaji na Wakulima wa Lokolova kwa madai kuwa wangejenga Mji wa Kimataifa na Viwanda.

Gama na washirika wake ambao ni maafisa waandamizi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, walitumia nguvu kufuta Ushirika wa Wafugaji na Wakulima wa Lokolova kwa nia ya kujipatia ardhi hiyo, hali iliyozua mgogoro mkubwa.

Baada ya kuhisi joto kali la mgogoro kati ya ofisi yake na wananchi, Gama aliamua kujitumbua kwa kwenda kugombea ubunge kupitia CCM na Septemba 14, 2015, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alimteua Amos Makalla kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kililmanjaro kuchukua nafasi ya Gama.

Makalla alikuta fukuto kubwa kwa kiwango cha kutisha, kwani kila kona aliyopita wananchi walitumia rungu la mgogoro huo kueleza nia ya kukiadhibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa kuchagua upinzani, ambapo Makalla katika kuepusha balaa aliigiza TAKUKURU kufanya uchunguzi wa kina na wahusika kufikishwa mahakamani iwapo ingebainika walitenda makosa.

Kamanda wa Takukuru, Mkoa wa Kilimanjaro, Alexander  Kuhanda amelithibitishia JAMHURI kuwa ofisi yake tayari imeshawahoji maofisa walioshiriki kusajili kampuni hizo akiwamo Gama mwenyewe.

Amesema Kampuni ya Kilimanjaro Uchumi Co. Ltd ilisajiliwa kama kampuni binafsi kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), lakini ilikuwa ikitumia anwani na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, hatua ambayo imedaiwa kuwa matumizi mabaya ya ofisi.

Kuhanda amesema taasisi yake inachunguza maeneo manne, ambayo ni uhalali wa kampuni hiyo, uanzishwaji wake, majukumu yake na tuhuma zinazoikabili kampuni hiyo.

“Ninachoweza kukwambia hayo ndiyo maeneo tunayoyachunguza, lakini ni tuhuma zipi tunachunguza nadhani mtupe muda tukikamilisha uchunguzi wetu hayo yote tutayaweka wazi,” amesema Kuhanda.

Wakati Kamanda huyo wa TAKUKURU akikataa kuanika tuhuma dhidi ya kampuni hiyo, JAMHURI limebaini kuwa kampuni hiyo tangu kusajiliwa kwake ilikuwa ikitumia jengo la Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro kuendesha shughuli zake.

Mbali na hilo,watendaji na wanahisa wa kampuni hiyo ni watumishi wa Serikali na imekopa Sh milioni 600 kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) kwa ajili ya kuwekeza katika eneo la Lokolova bila kuweka dhamana yoyote. Fedha hizo nazo zimeyeyuka.

“Nakwambia huyu Mkuu wa Mkoa alikuwa balaa. Anasema fedha hizo zilitumika kufanya upembuzi yakinifu na kuandaa michoro, lakini tulipofanya uchunguzi ikabainika kuwa hata michoro aliichora Afisa wa Manispaa ya Moshi… Afisa huyu anasema yeye aliombwa kufanya kazi hiyo aliifanya bila malipo,” kinasema chanzo cha JAMHURI kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.

Kuna kila dalili kuwa Gama atafikishwa mahakamani kwa kutumia kifungu cha 31 cha Sheria ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU). Kifungu hiki kinahusiana na matumizi mabaya ya ofisi. Mtu akikutwa na hatia, analipishwa faini isiyozidi Sh milioni 5 au kufungwa jela kwa muda usiozidi miaka 3.

Kosa la pili, huenda akafunguliwa kosa la kula njama chini ya  Kifungu cha 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (kama ilivyorekebishwa mwaka 2002). Kifungu hiki kinategemea kosa la kwanza chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, ambapo kifungu hiki kinasema iwapo kwa mfano atatiwa hatiani chini ya kifungu hicho cha 31, basi kosa la njama nalo litathibitika hivyo kinatoa adhabu ya kifungo cha miaka 7 bila faini.

Kwa mantiki hiyo, kwa kuwa sheria zote zinatoa vifungo vya zaidi ya miezi 6 Kicungu cha 67 (2)(c) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinataja sifa ya mtu kupoteza ubunge kuwa ni; ikiwa mtu huyo amehukumiwa na Mahakama yoyote katika Jamhuri ya Muungano na kupewa adhabu ya kifo au ya kufungwa gerezani kwa muda unaozidi miezi sita kwa kukutwa na hatia ya kosa lolote.

Katika tuhuma ya pili, chanzo kingine kimeliambia JAMHURI maneno ya kutisha: “Mkuu wa Mkoa Makalla alipofika, alikuta moto unawake. Aliamua kwenda kwa wananchi kuuliza kulikoni na limalizweje. Akiwa huko kwa wananchi, akamuuliza mwekezaji wa Kichina kuwa halmashauri inafaidikaje na fedha ilizochangia kwa kulipa watu fidia?

“Kilichotokea ilikuwa ni aibu. Yule Mchina alisema ‘wanafaidika kwa kununua saruji na kupata ajira.’ Makalla akasema na fedha ilizochangia halmashauri zinahesabiwa wapi? Yule Mchina akasema alimpatia Gama Sh milioni 200 awalipe fidia wananchi, hivyo alinunua ardhi alipojenga kiwanda cha Moshi Cement.”

Chanzo chetu kinasema mbali na Mchina huyo kutaja kuwa alimpa Gama Sh milioni 200 akawalipe wananchi fidia, inaelezwa kuwa Gama aliielekeza Halmashauri ya Rombo kuwalipa fidia wananchi, ambapo halmashauri bila kuwa na mkataba au ubia na Mchina katika kiwanda hicho cha saruji ilitumia Sh milioni 260 kuwalipa fidia watu tisa. Diwani wa Kata ya Holili, Wilbard Cornel amethibitisha watu hao kulipwa fidia.

Kwa upande wake Gama alipoulizwa na JAMHURI juu ya tuhuma hizo, amejibu kwa ufupi kuwa “Taratibu zilizotumika kusajili kampuni hiyo ziko wazi,” lakini hakuwa tayari kuingia kwa undani juu ya dhamana waliyoweka TIB kukopa Sh milioni 200. Gama ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini (CCM), amesema wanaoweza kulizungumzia suala la kampuni hiyo ni maofisa waliopo mkoani Kilimanjaro.

Makalla alifanya uamuzi wa kurejesha eneo hilo kwa wananchi baada ya kubaini kuwa hakukuwapo dhamana yoyote na hadi sasa haijulikani TIB itarejeshewaje fedha zake, hivyo akaona bora lawama kuliko ardhi ya wananchi kuchukuliwa. JAMHURI lilipomuuliza mwishoni mwa wiki, Makala amesema yeye alishughulikia mgogoro huo kulinda mali ya wananchi na si vinginevyo na akashauri atafutwe Mkuu wa Mkoa aliyepo Kilimanjaro kwa sasa kwani anayo majibu.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Saidi Mecky Sadiki ameliambia JAMHURI kuwa kampuni hiyo kwa sasa haipo, kwani taratibu za kuisajili “zilikiukwa” na kuongeza kuwa mkoa ulisharidhia kuwa kampuni hiyo ni hewa.

Februari 12, mwaka jana, wajumbe wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro (RCC) kilichokuwa chini ya Mkuu wa Mkoa wakati huo, Amos Makalla ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, kwa kauli moja waliridhia kutoitambua kampuni hiyo na kuagiza eneo la Ushirika wa Lokolova lirejeshwe kwa wanahushirika.

Kutokana na maagizo hayo, Makalla akiongozana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa walifunga safari hadi Ushirika wa Lokolova uliopo Wilaya ya Moshi Vijijini na kukabidhi eneo hilo.

Hatua hiyo ilihitimisha mgororo wa ardhi baina ya wanaushirika na kampuni hiyo na kuanzia Machi, mwaka jana Ushirika wa Lokolova kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika wamekuwa katika mchakato wa kuendeleza eneo hilo.

Hata hivyo, taarifa zinasema Gama alikwenda kumshitaki Makalla hadi kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwa anachochea wananchi na kwamba anafanya mambo yenye lengo la kuharibu heshima na kazi yake iliyotukuka aliyoifanya akiwa Kilimanjaro na Pinda alimjibu kwa ufupi kuwa “Nimekusikia, tutalifanyia mchakato.”

 

Makalla alivyomaliza mgogoro

Februari 19, mwaka jana Makalla na Kamati ya Ulinzi na Usalama walihitimisha mgogoro wa Lokolova, huku akiwashukuru wanaushirika kwa kuipa Serikali eneo la ekari 140 kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Kimataifa la Nafaka.

“Ofisi yangu kwa dhati kabisa inawashukuru ushirika wa Lokolova kwa kuipa Serikali ekari 140, hivyo sioni sababu ya Serikali kuingia katika mgogoro na wananchi badala yake ofisi yangu inatakiwa kuwa kimbilio la wananchi,” alisema Makalla.

Makalla alisema nia ya Serikali ni kulinda na kuimarisha vyama vya ushirika na kuwataka wanaushirika kuitumia ardhi waliyorejeshewa kwa manufaa ya ushirika na kwamba Serikali itaendelea kutoa ushirikiano ikiwamo mafunzo.

Aliwaonya kuepuka migogoro kwa madai kuwa ushirika wenye migogoro hauwezi kupiga hatua yoyote kimaendeleo huku uongozi wa ushirika huo ukishutumu uongozi wa Gama kwa kumega eneo lao kwa mabavu.

Mwenyekiti wa ushirika huo, Samwel Lyimo alisema mbele ya Makalla kuwa mgogoro wa ushirika huo na Serikali ulianza baada ya Gama kuufuta ushirika huo na kutangaza kuchukua ardhi kwa madai ya kujenga Mji wa Viwanda.

Alisema uamuzi huo haukuwa sahihi kutokana na alichodai kuwa Ushirika wa Lokolova haukushirikishwa katika maamuzi hayo hivyo mgogoro ukadumu kwa muda wa miaka mitatu hadi ulipopatiwa ufumbuzi na Makalla.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia aliishukuru Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro na Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa busara na ujasiri katika kuingilia na kutanzua mgogoro huo ambao alidai ulikuwa ukihatarisha amani.

Akawataka wanaushirika wa Lokolova kukaa na kumaliza tofauti zao baina ya wakulima na wafugaji akisema kukabidhiwa ardhi ni hatua nyingine na kuliendeleza eneo hilo kwa amani na mshikamano ni jambo muhimu .

Afisa Mwandamizi wa TIB, aliyeomba asitajwe gazetini amesema wao wanachofahamu bado wanaidai Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro na hivyo deni linaendelea kukua. Benki imesema haina utaratibu wa kuzungumzia mikopo ya wateja wao hadi inapothibitika kuwa wameshinda au kukaidi kulipa, ila wakasisitiza kuwa deni linaendelea kukua.

By Jamhuri